2016-12-19 10:37:00

Iweni wasanii na wajenzi wa huruma ya Mungu


Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru wasanii, mafundi mitambo na kwa namna ya pekee, Kikosi cha ulinzi na usalama cha Vatican, kwa kuandaa tamasha la muziki kwa ajili ya kuchangia fedha ili kugharimia huduma ya watoto wagonjwa nchini Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na kuwasaidia waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea hivi karibuni nchini Italia. Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa njia ya video uliorushwa moja kwa moja wakati wa tamasha la muziki, Jumamosi, tarehe 17 Desemba 2016 kwenye ukumbi wa Paulo VI anasema, “wote ni wasanii wa huruma ya Mungu” kwani matendo ya huruma kiroho na kimwili yanapata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu na yanafanyiwa kazi na binadamu!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu amelikabidhi Kanisa Waraka wa kitume, “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” kwa kusisitiza kwamba, utamaduni wa huruma unajengwa katika mazingira ya sala endelevu kama njia ya kushinda kishawishi cha maneno tupu bila matendo pamoja na nadharia ya huruma ya Mungu. Kumbe, kuna haja ya kumwilisha huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya watu kila siku, maisha yanayogeuzwa na kuwa ni shirikishi na yanayojikita katika upendo.

Tamasha la muziki limekuwa ni nafasi ya kuweza kupanua wigo wa maadhimisho wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kushiriki na kuguswa na umaskini na mahangaiko ya watoto wa Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati pamoja na watu walioguswa na tetemeko la ardhi hivi karibuni nchini Italia. Kwa ushiriki wa wote waliohudhuria tamasha hili la muziki, Baba Mtakatifu anasema, kwa hakika wanashiriki kwa ukarimu katika kuchangia ujenzi wa hospitali kwa ajili ya huduma kwa watoto wagonjwa, kielelezo hai cha Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma, huduma ambayo itaacha chapa ya kudumu ya ushiriki wao.

Baba Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, Mwenyezi Mungu amejifunua kwa walimwengu katika hali ya umaskini, akawaonesha Uso wa huruma ya Baba wa milele. Noeli ambayo kwa sasa inabisha hodi malangoni ni ukumbusho wa jinsi ambavyo Neno wa Mungu alivyoingia ulimwenguni, akazaliwa na Bikira Maria, lakini ikumbukwe kwamba, Maria na Yosefu hawakupata nafasi kwenye nyumba ya wageni, ndiyo maana Mtoto Yesu alizaliwa katika hali ya umaskini.

Taarifa ya Habari Njema ya kuzaliwa kwa Mkombozi, Yesu Kristo Mwana wa Mungu, kwanza kabisa wanahabarishwa wachungaji waliokuwa kondeni wakichunga mifugo yao. Hawa walikuwa ni watu maskini na wadhambi wa kutupwa, lakini hawa ndio waliohabarishwa Habari Njema ya furaha! Hivi ndivyo anavyotenda Mwenyezi Mungu, kuonesha kwamba, yuko kati na kwa ajili ya watu wake. Hii ni changamoto ya kuwa kweli ni wasanii wa upendo na wajenzi wa huruma ya Mungu, ili kuwekeza katika hazina ya maisha ya uzima wa milele yanayofumbatwa katika upendo na huruma ya Mungu Baba! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko kwa niaba ya watoto wa Bangui na wale wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko la ardhi nchini Italia, anapenda kuwashukuru kutoka katika undani wa sakafu ya moyo wake, kwani utekelezaji wa miradi ni chapa ya upendo na ushuhuda wa Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.