2016-12-17 15:51:00

Waziri mkuu Majaliwa atema mkwara wa nguvu Arumeru!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali itawanyang’anya ardhi wamiliki wote wa mashamba makubwa wilayani Arumeru ambao hawajayaendeleza kwa sababu wamekiuka mkataba wa umiliki. Amesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mheshimiwa William Lukuvi atakuja mkoani Arusha kwa ajili ya kufanya mapitio ya mashamba yote makubwa ambayo hayajaendelezwa na kuyarudishwa Serikalini. Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumamosi, Desemba 17, 2016 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Arumeru na wananchi wa kijiji Bwawani na kitongoji cha Mapinu katika kata ya Nduruma akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Arusha.

“Tufanya mapitio ya kila shamba ili kujua linamilikiwa na nani na alipewa lini na tangu alipokabidhiwa amefanya nini. Shamba lisiloendelezwa litarudisha kwa wananchi. Kama mtu ameshindwa kupata mtaji kwa muda wa miaka 10 atapata leo,” amesema. Serikali haiko tayari kuona wananchi wakinyanyaswa kwa kukosa ardhi ya kilimo kwa sababu ya watu wachache kumiliki maeneo makubwa bila ya kuyaendeleza.. "Ninataarifa kwamba hapa Arumeru kuna baadhi ya wawekezaji wanamiliki mashamba makubwa na hawajayaendeleza. Wengine wanakodisha kwa wananchi ili kujipatia fedha kinyume na mikataba yao ya umiliki. Hatutawavumilia,” amesema.

Amesema wilaya ya Arumeru inaongoza kwa migogoro ya ardhi na maeneo mengi yametwaliwa na mtu mmoja mmoja na baadhi yao wamekuwa wakilitumia vibaya Jeshi la Polisi kwa kuwanyanyasa wananchi wanaokatiza au kulima kwenye maeneo hayo. “Kuanzia leo marufuku Jeshi la Polisi kutumiwa na mtu binafsi kuwanyanyasa wananchi. Mtafanya hivyo kama kuna uvunjifu wa amani na si vinginevyo,” amesema.

Awali, akisoma taarifa ya wilaya mkuu wa wilaya ya Arumeru Bw. Alexander Mnyeti alimweleza Waziri Mkuu kwamba wilaya hiyo ina mashamba makubwa yanayomilikiwa na wawekezaji ambayo hayajaendelezwa. Mkuu huyo wa wilaya amesema kitendo cha kutoyaendeleza mashamba hanayo kisababisha wananchi kuyavamia hali inayochangia kushamiri kwa migogoro ya ardhi katika wilaya hiyo. Amesema tayari ofisi yake imefanya uhakiki wa mashamba hayo na kumuomba Mheshimiwa Rais, Dk. John Magufuli kufuta hati za mashamba 12 ambayo hayajaendelezwa kwa muda mrefu.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu amesema Serikali imepeleka sh. bilioni 800 katika halmashauri mbalimbali nchini kwa ajili ya ujenzi wa nyumba za walimu. Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo wakati akizindua nyumba ya walimu na vyumba vinne vya madarasa katika shule ya sekondari ya Orjolo, hatua ambayo inalenga kuboresha mazingira ya kufanyiakazi na kupunguza changamoto ya makazi kwa walimu. Amesema changamoto ya makazi imekuwa ikiwakabili walimu kwa mrefu hivyo Serikali imeamua kujenga nyumba za gharama nafuu ambazo zinawezesha familia sita kuishi pamoja.

Pia amewataka wazazi kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kuboresha miundombinu ya shule na kuhakikisha wanafuatilia miendendo ya elimu kwa watoto wao.  “Tumeondoa ada na michango yote iliyokuwa inawakera na kusababisha mshindwe kuwapeleka watoto shule. Jukumu lenu kwa sasa ni kufuatilia mienendo ya watoto wenu hadi kwa walimu ili kuhakikisha wanaingia darasani na wanasoma,” amesema. Awali, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Dk, Wilson Mahera alisema mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari ya awamu ya pili (SARPCCO II) umewezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 4,vyoo 20 pamoja na vyumba vya madarasa 6 vyenye jumla la Sh. milioni 289.52.

Wakati huo huo, Waziri mkuu amemsimamisha kazi aliyekuwa Mwekahazina wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido, Bw. Issai Mbilu ambaye kwa sasa amehamishiwa Wilaya ya Bahi mkoani Dodoma na kuagiza arudishwe haraka na kuja kujibu tuhuma za ubadhilifu sh. milioni 642.4 za miradi zinazomkabili. “Tunaendelea kudhibiti na kuweka nidhamu ndani ya Serikali. Ukiharibu Longido usitegemee kuhamishiwa wilaya nyingine tunamalizana hapa hapa. Hatuwezi kuhamisha ugonjwa hapa na kuupeleka wilaya nyingine hivyo Mwekahazina huyu arudishwe haraka Longido,” amesisitiza. Waziri Mkuu ametoa agizo hilo  Ijumaa, Desemba 16, 2016 wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Longido kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Arusha.

Pia amemwagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Richard Kwitega kumwandikia barua Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) akimwomba amrudishe Mweka hazina huyo katika kituo chake cha kazi cha zamani ili aweze kujibu tuhuma zinazomkabili. Amesema Serikali haitamvumilia mtumishi wa idara yoyote atakayeharibu jambo halafu kuhamishwa sehemu nyingine, “hivyo naagiza kuanzia sasa nimemsimamisha kazi Mwekahazina huyu na arudi hapa kujibu kwanini ameleta hasara ya hizi fedha. Na nyie watumishi wengine hili liwe funzo kwenu,” amesema. Miradi mingi ya maendeleo inakwama kwa sababu ya baadhi ya watumishi kuweka mbele maslahi binafsi badala ya kuzingatia maadili ya utumishi, hivyo amewaagiza Wakuu wa Idara wafuatilie kwa makini miradi inayotekelezwa katika maeneo yao kama inalingana na thamani halisi ya fedha zilizotolewa.

Akizungumzia kuhusu kushamiri kwa biashara haramu ya dawa za kulevya wilayani Longido, Waziri Mkuu amewaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya kufanya kufanya msako wa nyumba hadi nyumba na kuwakamata wote watakaokutwa wanafanya biashara hiyo. “Wilaya hii ina sifa mbaya ya kuwa kitovu cha kusafirisha dawa ya kulevya zikiwemo bangi na mirungi. Hivyo nawaagiza wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama waendeshe msako kwa kila nyumba na atakayekamatwa achukuliwe hatua. Dawa za kulevya zinadhohofisha nguvu kazi ya Taifa,”. “Ukivuta bangi unapishana na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu kwani unakwenda kulala jambo ambalo hatuwezi kulikubali. Watakaokutwa wanauza au kununua mirungi na bangi wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria ikiwa pamoja na kutaifisha magari yanayotumika kubeba bidhaa hiyo haramu,” amesema.

Awali, Mkuu wa Wilaya hiyo Bw. Daniel Chongolo akisoma Taarifa ya Wilaya amesema Longido inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo kutumika kama njia kuu ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi kwenda nchi jirani ya Kenya ambako biashara hiyo imehalalishwa. Changamoto nyingine ni ukosefu wa hospitali ya wilaya hali inayofanya wananchi kwenda kutibiwa Kenya, ambapo Waziri Mkuu alisema haiwezekani wakakosa hospitali ya wilaya hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo kuhakikiusha anatenga fedha za ujenzi huo.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ipo mbioni kujenga kiwanda cha kuchakata madini ya magadi soda ili yawe na ubora na thamani kubwa. Ametoa kauli hiyo aliposimamishwa na wananchi katika kijiji cha Loonolwo kilichopo Kata ya Gelai Merugoi Wilayani Longido akitokea wilayani Ngorongoro. Amesema lengo la kujenga kiwanda hicho ni kuwawezesha wananchi wa wilaya hiyo hasa akinamama wanaoishi karibu na Ziwa Natron linalotoa magadi hayo waweze kunufaika na uwepo wa ziwa hilo.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utawezesha vijana na akinamama hao wanaouza magadi maeneo ya pembezoni mwa barabara katika ziwa Natron kupata ajira kwa kuwa kitazalisha ajira zaidi ya 500 katika wilaya hizo mbili za Longido na Ngorongoro. Pia amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Bw. Mrisho Gambo kushirikiana na wataalam wake kufanya tathimini ya uhaba wa chakula katika wilaya za Longido na Ngorongoro ili Serikali ijue Mkoa wa Arusha una ukosefu wa chakula kwa kiasi gani. "Gambo fanya tathimini ya hali ya njaa katika wilaya hizi mbili ili tuweze kuwasaidia wananchi hawa. Hata hivyo nawaomba wananchi mtunze kiasi cha chakula mlichonacho na marufuku tumia nafaka kwa ajili ya kupika pombe,” amesema.

Awali, wananchi hao waliokuwa na mabango mbalimbali walilalamikia kero ya mipaka ya ardhi kati ya vijiji vya wilaya za Longido na Ngorongoro, ambapo Waziri Mkuu alimuagiza Afisa Ardhi Mkoa wa Arusha, Bw. Hamdoun Mansour kwenda katika vijiji hivyo vya mpakani na kukutana na viongozi wa kimila ili kumaliza mgogoro huo.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.