2016-12-17 09:30:00

Colombia kipaumbele: haki, amani na upatanisho wa kitaifa!


Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 16 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na viongozi wa ngazi ya juu kutoka nchini Colombia. Kwanza kabisa amekutana na Rais Juan Manuel Santos Calderòn ambaye baadaye alipata bahati ya kukutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameongozana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa.

Baadaye kidogo, Baba Mtakatifu alikutana pia na Senate Alvaro Uribe Vèlez, Rais mstaafu wa Colombia. Mazungumzo kati ya viongozi hawa wawili yamedumu kwa takribani dakika 20 hivi! Mazungumzo ya viongozi hawa yamefanyika katika hali ya utulivu na amani, kwa kukazia mahusiano mazuri ya nchi hizi mbili. Viongozi wa Colombia wamempongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kusaidia kusukuma mbele mchakato wa amani ya kudumu nchini mwao. Kwa sasa changamoto ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo umoja na mshikamano wa kitaifa miongoni mwa wanasiasa wa Colombia pamoja na nafasi ya FARC-EP ili kuanzisha mchakato wa upatanisho wa kitaifa, majiundo makini ya msamaha na maridhiano, dhamana inayoweza kutekelezwa vyema zaidi na Kanisa mahalia.

Mwishoni, Baba Mtakatifu wakati wa majira ya mchana amekutana na kuzungumza kwa ujumla na viongozi wa Colombia waliomtembelea mjini Vatican, Ijumaa tarehe 16 Desemba 2016, wakati wa mkesha wa kumbu kumbu ya Siku yake ya kuzaliwa anapomshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 80 tangu alipozaliwa. Mkutano wa Baba Mtakatifu na viongozi wa Colombia umedumu kwa takribani dakika 25 na kwamba, wamegusia masuala ya kitaifa, kikanda na kimataifa! Wamekazia umuhimu wa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana; majadiliano katika ukweli na uwazi nchini Colombia, hususani wakati huu wa kipindi cha mpito na muhimu katika historia ya wananchi wa Colombia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.