2016-12-15 14:53:00

Umoja wa Mataifa unalipongeza Kanisa nchini DRC


Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon analipongeza Kanisa Katoliki nchini DRC kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa upatanisho, haki, amani na ujenzi wa umoja wa kitaifa nchini DRC, wakati huu, wananchi wanapojiandaa kwa ajili ya uchaguzi mkuu. Bwana Ban Ki-Moon analiomba Kanisa kuendeleza juhudi hizi ili hatimaye, ziweze kufanikisha mchakato wa Uchaguzi mkuu unaopaswa kuwa wa kweli na haki, chachu muhimu sana katika kukuza na kudumisha misingi ya demokrasia, haki, amani, upatanisho na umoja wa Kitaifa.

Hivi karibuni, Baraza la Maaskofu Katoliki DRC lilisema, amani na utulivu wa kisiasa nchini humo ni jambo linalowezekana kabisa ikiwa kama, viongozi wa kisiasa pamoja na vyama vyao, wataonesha utashi wa kisiasa na kimaadili kwa ajili ya kutekeleza maamuzi yaliyofikiwa ili kufanikisha mchakato wa Uchaguzi mkuu. Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linasema, liko tayari kusaidia mchakato wa haki, amani, upatanisho na ujenzi wa umoja wa kitaifa. Hayo yalisemwa na Askofu mkuu Marcel Utembi Tapa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC.

Rais Joseph Kabila aliwaomba Maaskofu kuwa daraja la upatanisho kati ya Serikali na Vyama vikuu vya Upinzani nchini humo, ili kufanikisha mchakato wa demokrasia katika ukweli na uwazi. Maaskofu wanakaza kusema, kuna mambo mengi yanayowaunganisha wananchi wa DRC kiasi kwamba, wanaweza kushinda na kuvuka kasoro zao kwa kuzingatia Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni sheria mama!

Kalenda ya uchaguzi, Tume huru ya uchaguzi, Baraza huru la mawasiliano na rasilimali fedha kwa ajili ya kugharimia mchakato mzima wa uchaguzi ni kati ya changamoto kubwa zilizoko mbele ya wananchi wa DRC kwa sasa. Uundwaji wa Serikali ya mpito ni muhimu sana wakati huu Rais Joseph Kabila anapohitimisha awamu yake ya uongozi mwishoni mwa Mwezi Desemba 2016. Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anawataka wadau wote nchini DRC kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika mchakato wa upatanisho na umoja wa Kitaifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Uchaguzi mkuu nchini DRC unatarajiwa kufanyika kunako mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.