2016-12-15 15:14:00

Mungu yu pamoja nasi!


Jambo moja ambalo lipo wazi katika masomo yote ya leo ni habari ya kuzaliwa mtoto. Kwamba tazama Bikira atachukua mimba na atamzaa mtoto na jina lake ni Emmanuel – Mungu pamoja nasi. Katika somo la kwanza tunaona Mwenyezi Mungu akitangaza habari njema ya ujio wa mtoto. Katika somo la pili tunaambiwa kuwa Yesu Kristo alizaliwa kutoka ukoo wa Daudi kadiri ya mwili na katika injili Matayo anaandika habari ya kuzaliwa kwake Bwana kulivyokuwa. Aidha katika somo la pili tunasoma sehemu ya ufunguzi wa barua ya Paulo kwa Warumi. Katika sehemu hii, Mtume Paulo anaongea juu yake, juu ya Warumi na pia lengo la barua yake. Kwa kifupi barua hii ni juu ya habari njema kwa aliyofanya Mungu kwetu sisi katika Mwanae, Yesu Kristo. Hiki ndicho tunachoadhimisha katika sikukuu ya Noeli. Noeli ni sikukuu ya kuzaliwa kwake Bwana.

Ni nani huyu mtoto? Ni yule aliyeshuka toka ukoo wa Daudi. Tunakumbushwa kuwa Mungu kwa kupitia watu wake hutenda makuu. Habari ya noeli si tu ya Mungu na Yesu Kristo ila pia ni habari ya Maria na Yosefu, juu ya wachugaji na mamajusi na zaidi sana juu ya jinsi mwanadamu anavyoshirikishwa makuu ya Mungu. Ni juu ya mtoto aliyetangazwa kuwa mpendwa wake na ambaye kwa namna ya pekee alimfufua toka wafu.

Ni yule anayeongea mambo ya Mungu, ambaye sisi tunamsikiliza. Ni mtoto ambaye kwake yeye tunapata neema. Katika Yoh. 1:17 tunasoma kuwa sheria ililetwa na Musa, neema na ukweli kwa njia ya Kristo. Kwa njia yake sisi tunapokea neema juu ya neema. Kwake yeye sisi tunapokea utume, yaani wito kama watumishi wa Mungu. Kwake yeye tunapokea utajiri na neema na pia hupata wito wa kumtumikia yeye. Tunaposali kwa ajili ya neema za mtoto anayezaliwa kwetu, tuombe pia atuoneshe namna ya kumtumikia Mungu kwa furaha na amani siku zote za maisha yetu.

Ni kwa namna gani tunamsubiria Bwana? Wale Wayahudi walikuwa na namna yao ya kumtarajia Bwana na hivyo ikawa vigumu hata alipokuwepo wakashindwa kabisa kumtambua. Tunasoma katika Yoh. 7:27 – lakini huyu tumejua ametoka wapi, bali atakapokuja Masiya hakuna atakayejua alikotoka. Je, Mungu anafanyaje kazi ndani yetu? Kwa hakika Mungu yupo. Katika Mat. 17:28 tunasoma hivi – kwa maana, ndani yake yeye sisi tunaishi, tunajimudu na tumo.

Tunafundishwa toka Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, katika kipengele ‘Ufunuo’  kuwa Mungu, mwanzo na mwisho wa yote, anaweza kufahamika kwetu kwa njia ya viumbe tukitumia mwanga wa akili ya mwanadamu. Bila shaka katika hali hii tunaona uwezo wa mwanadamu kutambua nafasi ya muumbaji na uwezo wa kuendelea kutambua ukuu huo wa Mungu. Hatuna budi kujua au kuutambua uwepo wa Mungu kati yetu. Neno la Mungu siku ya leo laongea wazi kuhusu uwepo wa Mungu kati yetu kwa njia ya mwanae. Hatuna budi kufanya bidii ya pekee ili huyu Mungu na ufalme wake uendelee kuenea duniani. Hatuna budi kumtumikia ili tusije kukumbwa na duwaa kama Yakobo pale Betheli kama tusomapo katika kitabu cha Mwanzo 28:16 – Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, kweli, Bwana yupo mahali hapa, nami sikujua’.

Ndugu wapendwa, sherehe ya noeli huendana na kutoa zawadi. Noeli ni kutoa. Mtoaji wa kwanza na mtoa chema ni Mungu mwenyewe.  Katika sikukuu ya noeli tunamsherehekea Mungu anayemtoa mwanawe – Yoh. 3:16 kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amsadikiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Mungu anatoa na watu wake wanatakiwa kutoa, hiyo ndiyo noeli. Kama noeli ni sherehe au kipindi cha kutoa, na Mungu ametoa utukufu wake, je sisi tunampatia nini Mungu kama shukrani? Changamoto hii itufikirishe sana.

Ni kitu gani cha kutoa na namna gani tutoe ili tumrudishie Mungu utukufu na sifa? Mama Bikira Maria anatuongoza vizuri sana na kutusaidia kuishi maisha ya shukrani na kujitolea. Yeye alipokea kwa shukrani zawadi ya Mungu na akamrudishia Mungu sifa kwa kumzaa Bwana wetu Yesu Kristo. Tulipotindikiwa, tukazidiwa na dhambi, Mungu Baba alimtuma mwanae ili atukumboe. Hii ndiyo zawadi ya kweli na hai. Hakika ni rahisi kutoa zawadi ya maua, keki, fedha n.k. Mtu si kitu na kitu si mtu. Zawadi zetu kipindi hiki cha noeli hazina budi kuwa na mtazamo tofauti na tulivyozoea. Mungu anahitaji sadaka safi, hai na takatifu.

Tunajiuliza leo ni kwa kiasi gani tunatambua thamani ya upendo huu wa Mungu kwetu. Ni kwa jinsi gani tunathamini maisha yetu, zawadi ya imani yetu ya kikristo, uwepo wa Mungu kwetu. Majilio hutupa nafasi ya kukumbuka matendo makuu ya Mungu na kutumainia upendo wake mkuu ambao kwetu sisi ni wokovu wa milele. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu aendelee kutufunulia upendo huo na sisi tuwe tayari kuishi wito aliotujalia Mungu Baba na noeli yetu mwaka huu ituwezeshe kumpokea Mungu kwa moyo wa shukrani.

Tumsifu Yesu Kristo.

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.