2016-12-15 07:01:00

Mshikamano wa huduma na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji


Baba Mtakatifu Francisko anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni dhamana nyeti na endelevu kwa familia ya Mungu duniani kwani athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi duniani; vita na kinzani za kijamii; mambo yanayohatarisha haki msingi za binadamu, utu na heshima yake. Takwimu zinaonesha kwamba, duniani kuna zaidi ya wakimbizi millioni 125 wanaohitaji msaada wa hali na mali. Wengi wao ni wahanga wa vita, kinzani na mipasuko ya kijamii; baa la njaa na ukame wa kutisha na kwamba, sehemu kubwa ni waathirika wa majanga asilia!

Vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inasababishwa kwa sehemu kubwa na uchu wa mali na madaraka; ubinafsi. Haya ni mambo yanaweza kupewa kisogo, ikiwa kama familia ya Mungu itajikita katika fadhila za kibinadamu; utawala bora unaojikita katika misingi ya sheria, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote sanjari na kilimo cha kisasa na kwamba, changamoto ya kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu inayovaliwa njuga na Mama Kanisa!

Hivi karibuni, Wastahiki Mameya wa Majiji mbali mbali Barani Ulaya, walikutanika mjini Vatican ili kujadili pamoja na mambo mengine changamoto ya wakimbizi na wahamiaji Barani Ulaya kwa kutambua kwamba, hawa ni binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; wana haki zao msingi, utu na heshima yao inayopaswa kuendelezwa na kudumishwa na wote. Katika mkutano huu, Mameya waliazimia kuunda mtandao utakaosaidia mchakato wa kuwapokea na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi, usalama na maisha kwenye Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa kama njia ya kuonesha mshikamano wa dhati na watu hawa wanaoteseka sana na kuonekana kuwa kero kwa Jumuiya ya Kimataifa.

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi ilitoa changamoto ya wakimbizi kwa Wastahiki Mameya kutambua kwamba, hata wakimbizi katika shida na mahangaiko yao, bado wanabaki kuwa ni ndugu zao, walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Hapa kuna haja ya kuunda mtandao mkubwa wa ukarimu na upendo, utakaosaidia kutoa huduma makini kwa wakimbizi na wahamiaji; uamuzi wa busara uliofikiwa na Mameya hawa baada ya mkutano wao uliokuwa unafanyika mjini Vatican. Lengo ni kujielekeza kwenye majiji yenye ukarimu na mshikamano wa upendo kwa wahamiaji na wakimbizi, kuliko ilivyo kwa wakati huu!

Utawala bora unaojali na kuzingatia utu na heshima ya binadamu; utawala huu unagusa uongozi wa kitaifa, kikanda na kimataifa. Kumbe, ujenzi wa mitandao hii ufanyike kwa njia ya mafungamano ya kijamii yanayofumbatwa na jamii pamoja na dini mbali mbali, ili kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu; haki zake msingi; uhuru, haki, amani na mwingiliano wa kijamii pamoja na kuondokana na maamuzi mbele. Jumuiya ya binadamu iwe na ujasiri wa kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana badala ya mwelekeo wa sasa wa kutaka kujenga kuta za utengano!

Mtandao wa mshikamano wa upendo iwe chachu ya kuwasaidia waathirika wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Utumwa mamboleo unaojidhihirisha kwa namna ya pekee kwa kazi za suluba na ukahaba kwa wanawake na wasichana. Hizi ni kati ya tema tete zinazoendelea kuvaliwa njuga katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Mshikamano huu uwe ni chachu ya kukuza na kudumisha haki na amani; iwe ni fursa ya kuwashirikisha wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa kutunga sera na mikakati ya uchumi shirikishi bila kuwasahau vijana wanaoteseka kutokana na ukosefu wa fursa za ajira.

Hati ya mwisho ya Mameya hawa inazitaka Serikali kutenga fungu maalum kwa ajili ya huduma ya afya, elimu na ruzuku kwa familia, ili kweli ziweze kutekeleza dhamana na majukumu yake barabara! Familia zinazoogelea katika dimbwi la umaskini si rahisi kuweza kutekeleza dhamana yake vyema ndani ya jamii. Wimbi la wakimbizi na wahamiaji kwa sasa linawakumba watu zaidi ya millioni 65, mwaliko wa kuwa na mabadiliko katika sera na mikakati ya maendeleo. Badala ya kutenga kiasi kikubwa cha fedha ya bajeti kwa ajili ulinzi na usalama, sasa mwelekeo uwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi.

Kuta za utengano zinazojengwa na baadhi ya wakuu wan chi kama njia ya kujibu changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi, haziwezi kufua dafu kwa watu wanaotafuta hifadhi, usala na maisha bora zaidi Barani Ulaya. Hawa ni watu wanaothubutu hata kama kifo wanakiona mbele ya macho yao kila siku! Baadhi ya miji ya Bara la Ulaya ina historia na mapokeo makubwa hata kabla ya Ukristo! Hii ni miji kama vile Roma, Athens Lesbov ambayo imekuwa mstari wa mbele kujenga na kudumisha mtandao wa mshikamano wa upendo na mafungamano ya kijamii. Miji hii inaweza kuwa ni mfano bora wa kuigwa. Mji wa Athens ni chimbuko la demokrasia wakati ambapo Florence ni chimbuko la mchakato wa kupinga adhabu ya kifo duniani iliyopitwa na wakati kwani inadhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.