2016-12-14 08:44:00

Watu zaidi ya 30 wamefariki kwa ajali ya barabarani Naivasha, Kenya


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linapenda kuungana na familia ya Mungu nchini humo kuomboleza vifo vya watu zaidi ya 30 waliofariki hivi karibuni kwenye ajali ya barabarani baada ya Lori la mafuta kuwaka moto na kuunguza pia magari kadhaa, eneo la Naivasha. Salam hizi za rambi rambi zimetolewa na Askofu Philip Anyolo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya. Wanawaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito faraja na neema ya ujasiri kutoka kwa Mwenyezi Mungu ili waweze kuubeba msiba huu kwa imani na matumaini. Wanawaombea majeruhi wote ili waweze kupona na kurejea tena katika shughuli zao za kawaida.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaitaka Serikali pamoja na mawakala wa barabara, vyombo vya ulinzi na usalama wa raia na mali zao, kuhakikisha kwamba, vinaweka alama za barabara pamoja na kuondoa matuta barabarani kwani yamekuwa ni kati ya vyanzo vya ajali mbaya za barabarani nchini Kenya. Maaskofu wanasikitika kusema, mara nyingi matuta haya yanaondolewa baada ya ajali kutokea katika eneo la tukio.

Maaskofu wanawataka wananchi wote kuwa makini zaidi hasa wakati huu wa pilika pilika za Siku kuu ya Noeli na Mwaka Mpya 2017. Vyombo vya ulinzi na usalama viendelee kuweka sera na mikakati ya kudhibiti ajali barabarani ili kuokoa maisha ya raia kwa kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani. Kipindi cha Siku kuu kisiwe ni muda muafaka kwa baadhi ya askari wa usalama barabarani kutaka kujineemesha kwa kupokea rushwa kutokana na makosa ya usalama barabarani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.