2016-12-14 09:25:00

Papa Francisko anaguswa na mateso ya wananchi wa Siria


Mateso na mahangaiko ya wananchi wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati, lakini kwa namna ya pekee nchini Siria ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa, kuhakikisha kwamba, inajifunga kibwebwe ili kusitisha vita na hatimaye, kuanza mchakato wa ujenzi wa misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa; kwa kukataa kumezwa na misimamo mikali ya kidini na kisiasa ambayo imekuwa ni chanzo kikuu cha maafa kwa wananchi wa Siria.

Uharibifu wa mazingira na kumbu kumbu za kihistoria ni jambo ambalo kamwe aliwezi kuvumiliwa na kuacha liendelee kutokea kwani huu ni urithi mkubwa wa binadamu. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu Francisko anaguswa na mahangaiko ya wananchi wa Siria. Anasikitishwa sana na hali ngumu ya maisha na uharibifu mkubwa wa makazi ya watu na kumbu kumbu za kihistoria zinavyoendelea kutoweka huko Aleppo na Palmira.

Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria anasema, hivi karibuni amewasilisha barua ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Rais Bashar Al Assad pamoja na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa ili kusitisha vita, chuki na uhasama kwa kujikita katika njia ya majadiliano, maridhiano, amani na utulivu.  Kardinali anasema, amerejea nchini Siria kama Kardinali lakini anaendelea na utume wake kama Balozi wa Vatican nchini Siria ili kuonesha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa wananchi wa Siria wanaoteseka sana kutokana na madhara ya vita.

Anasema, Rais Assad ameipokea barua ya Baba Mtakatifu kwa heshima na taadhima pamoja na kutambua uwepo wake wa karibu kwa watu maskini na wale wanaoteseka. Ufumbuzi wa mgogoro wa Siria si rahisi, lakini kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kukomesha vita nchini Siria; kuendelea kutoa msaada wa hali na mali na kuanza mchakato wa upatanisho, haki na amani kwani wanaoteseka ni raia wa kawaida. Uwepo wa nchi kama Russia, Iraq na Marekani ni kwa ajili ya mafao ya biashara ya nchi zao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.