2016-12-13 11:19:00

Watanzania dumisheni haki, amani na uhuru wa kuabudu!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa dini nchini kutimiza wajibu wao kwa kuwahimiza waamini wao kujiepusha na kauli na vitendo vitakavyopandikiza chuki na uchochezi miongoni mwa waamini wa dini moja na waamini wa dini nyingine . Ametoa kauli hiyo Jumatatu , Desemba 12, 2016 wakati akihutubia kwenye baraza la Maulid lililofanyika Shelui mkoani Singida, ambapo amesisitiza kwamba Serikali ya awamu ya tano ipo imara na haitayumba. "Ni vyema tukatambua kwamba katika mifarakano na uhasama wa kidini hakuna atakayeibuka mshindi bali wote tutakuwa ni watu tulioshindwa. Nyumba za ibada zisaidie kuunganisha waamini na kuwa mfano usoni kwa jamii,"

Amesema mara kadhaa watu wameshuhudia migogoro na mapigano kwenye Misikiti wakigombea uongozi na mali matukio ambayo hayana tija ndani ya Uislam, hivyo ni vyema wakafuata misingi ya dini ya kuheshimiana , kuelewana na kuvumiliana. Watumie mabaraza kukemea hali hiyo inayowagawa Waislam. Amesema Serikali itaendelea kuzitegemea dini zote nchini kujenga msingi imara wa kuleta amani miongoni mwa Watanzania. Serikali itaendelea kusisitiza na kuheshimu uhuru wa raia wa Tanzania kuabudu dini wanayoiamini kwa sababu ni moja kati ya haki za msingi za kila mwananchi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

"Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali itaendelea kufanya kila iwezalo kuhakikisha kwamba uhuru huo unaheshimiwa . Hii ni nyenzo muhimu iliyosaidia kulifanya Taifa letu kuwa ni mfano wa kuigwa kote ulimwenguni .Tutaendelea kushirikiana na viongozi wa dini zote nchini ili kuhakikisha kuwa tunu hiyo muhimu haichezewi na mtu au kikundi chochote," amesema .

Wakati huo huo, Waziri Mkuu alizungumzia suala la kuwepo kwa tishio la ugaidi duniani ambalo limegharimu maisha ya baadhi ya wananchi." Aidha , mmezungumzia kuhusu uwezekano wa baadhi ya watuhumiwa wa ugaidi kufunguliwa mashtaka kwa sababu ya chuki au kulipiza kisasi,”. “Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali iko macho katika kupambana na tishio lolote la kiusalama ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu. Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama viko katika hali ya utayari wakati wote ili kupambana na vikundi au watu na mtu yeyote mwenye nia ya kuhatarisha usalama wa nchi yetu,” amesema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwakukumbusha viongozi wa dini kwamba jukumu la ulinzi wa nchi yetu kwa mujibu wa Katiba ni jukumu la kila mwananchi. “ Yaani kila Mtanzania,". Waziri Mkuu ameongeza kuwa ni vyema viongozi wa dini wakatambua kwamba wao pamoja na waumini wanaowaongoza ndio walinzi wa Taifa hivyo wanalo jukumu la kuendelea kuwasihi waumini kuendelea kuwa raia wema na kutoa taarifa za dalili za uhalifu mapema iwezekanavyo.

"Mathalan, hawa watoto wanaojiita “Panya Road” huko Dar es Salaam au vijana wanaoteka magari pale mlima Sekenke, hawatoki kwenye sayari nyingine ni watoto wetu tunaishi nao majumbani, tunaabudu nao Misikitini au Makanisani. Ni jukumu la kila mmoja wetu kuwaripoti kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili watambulike na washughulikiwe ipasavyo. Wasiendelee kuleta madhara kwa raia wema ," amesema .

Kwa upande wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Abubakary Bin Zubeiry amewasihi waislam nchini kuishi maisha ya Mtume Muhammad (SWA) ambaye alisisitiza kupendana na kushikamana, kuwajali wengine bila kuwabagua kiimani, kupenda kufanya kazi halali na kujifunza. “Si jambo rahisi kupata kipato bila kufanya kazi ,tutalaumu kila siku kuwa hatuoni mabadiliko ya kipato wakati sisi wenyewe hatufanyi kazi. Uislam ni kielelezo tosha kwa mfano wa maisha bora, si kweli kuwa dini yetu inafundisha tuchukie wengine,” amesisitiza. Pia Sheikh Zubeir amewaasa waamini wa dini zote kushika imani iliyosahihi huku akiwaomba kupuuza kauli za badhi ya watu kudai magaidi hutokea katika dini ya kiislam kutokana kuwa na imani kubwa ya kiislam. Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba amesisitiza kupambana na watu ambao wamekuwa wakienda kinyume na sheria za nchi.

Wakati huo huo, Waziri mkuu  Kassim Majaliwa amewashukuru na kuwapongeza madaktari wa Taasisi ya Bilal Muslim Tanzania ambayo imetoa huduma ya matibabu ya macho kwa zaidi ya wananchi 4,000 wa mkoa wa Dodoma  Ametoa pongezi hizo Jumapili , Desemba 11, 2016 wakati akizungumza na madaktari waliotoa huduma hiyo walipomtembelea katika makazi ya Waziri Mkuu mkoani Dodoma

Waziri Mkuu alisema huduma wanayoitoa ni muhimu kwa kuwa imewezesha watu ambao walikata tamaa ya kuona wameona, hivyo aliwaomba waendelee kwenda katika maeneo mengine nchini ili Watanzania wengi zaidi waweze kunufaika. "Nawashukuru kwa mchango mkubwa mnaoutoa katika kuunga mkono jitihada za Serikali kwenye utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure na kuwawezesha hata wale wasiokuwa na uwezo kupata huduma ," alisema. Serikali ya awamu ya Tano ina dhamira ya dhati kuwatumikia wananchi na kutoa huduma kwa wote , hivyo tuko tayari kushirikiana na taasisi yeyote ambayo inakusudia kuwafikia wananchi.  Waziri Mkuu alisema “katika utoaji huduma za jamii , Serikali inathamini sana mchango wa taasisi binafsi na za dini ambazo ziko mstari wa mbele kushirikiana na jamii kwa ujumla,”.

Katika hatua nyingine Waziri Mkuu aliwakaribisha madaktari hao kuja kuwekeza katika sekta mbalimbali mkoani Dodoma. “Hapa ndio makao makuu ya Tanzania , hivyo nawakaribisha mje kuwekeza, ardhi ya kutosha ipo . Mnaweza kuja kujenga hospitali kubwa ya macho," alisema. Naye Naibu wa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mheshimiwa, Anthony Mavunde alisema jumla ya watoto 250 wamefanyiwa upasuaji wa macho na madaktari hao ambao walianza kutoa huduma hiyo Desemba 8, 2016 na kumaliza Desemba 12, 2016. "Nawashukuru kwa moyo wenu wa kujitolea kuja kusaidia watu wenye mahitaji ya matibabu ya macho . Mkoa wa Dodoma una changamoto kubwa ya matatizo ya macho. Nimefarijika sana kuona baadhi ya akinamama waliokuwa wamekata tamaa ya kuona wameweza kuona tena,” alisema.

Naye Mtaribu wa taasisi hiyo, Noorelain Sharrif alimuahidi Waziri Mkuu kwamba wataendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma za matibabu ya macho bure kwa wananchi wenye mahitaji na wako tayari kwenda popote nchini kutoa huduma hiyo.“Tuko tayari kushirikiana na Serikali katika kutimiza wajibu wetu kwa jamii , tutafanya hivyo wakati wowote na kwa wananchi wote,” alisema.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.