2016-12-12 15:13:00

Watanzania Roma washerehekea Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania kwa vifijo


Familia ya Mungu inayosoma na kuishi mjini Roma, Jumapili tarehe 11 Desemba 2016 imeadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbu kumbu ya miaka 55 tangu Tanzania ilipojipatia uhuru wake kutoka kwa Waingereza kunako mwaka 1961. Ibada hii ya Misa Takatifu imeongozwa na Padre Felix Luboya, moja ya Mapadre vijana kabisa kutoka Tanzania aliyepadrishwa wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, mwaliko kwa Wakleri kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa waja wake!

Itakumbukwa kwamba, tarehe 1 Oktoba 2016, huko Rubya, Jimbo Katoliki Bukoba, kumezinduliwa maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka wa Padre, kama kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Tanzania ilipojipatia kwa mara ya kwanza Mapadre wazalendo na huo ukawa ni mwanzo wa wito, maisha na wito wa Kipadre kutoka katika familia ya Mungu nchini Tanzania. Kumbe, Padre Felix Luboya ni kielelezo cha mwendelezo wa Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu na mwanzo wa mchakato wa Jubilei ya miaka 100 ya Padre nchini Tanzania. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari pia na Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, inaofanyika katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia sasa!

Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. ambaye kwa Mwaka 2016 anaadhimisha Jubilei ya Miaka 25 tangu alipopewa Daraja Takatifu ya Upadre na kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya miaka 50 ya uwepo na utume wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania, alitoa mahubiri katika Ibada hii ya Misa Takatifu iliyohudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Afrika Mashariki, kwani hawa ni watu wanaojisikia kuwa wamoja hasa wanapokuwa ugenini kwani kuishi ugenini kunataka moyo kweli kweli kama wanavyosema waungwana!

Padre Musbobozi katika mahubiri yake, amekazia kwa namna ya pekee ujumbe wa furaha unaofumbatwa katika Liturujia ya Neno la Mungu, Jumapili ya tatu ya Kipindi cha Majilio. Yohane Mbatizaji baada kutiwa gerezani kwa kwa sababu ya kusema na kushuhudia ukweli, anasikia matendo makuu ya Mungu yanayotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu, kiasi hata cha kutuma ujumbe kwa Yesu, ili kumuulizia ikiwa kama ndiye au wamsubiri mwingine? Hapa wataalam wa mambo wanasema, imani na matumaini ya Yohane Mbatizaji yalitikiswa na kwamba, Yesu anawahakikishia wajumbe wa Yohane, kumwelezea kile wanachosikia na kuona na kwamba, heri mtu yule asiyekuwa na mashaka ya imani kwa Yesu!

Nabii Isaya anatangaza kuhusu mpango wa Mungu kwa viumbe wake na kusema kwamba, Mwenyezi Mungu anataka kufanya yote mapya. Huu ni mwaliko kwa waamini kumwalika Mwenyezi Mungu ili awasaidie kufanya yote mapya pamoja na kumwalika Kristo Masiha kuja kuwaokoa kutoka katika mambo yote yanayokwamisha safari ya imani yao kama familia ya Mungu. Wanahimizwa kukuza na kujenga fadhila ya subira na uvumilivu; kwa kutenda na kushuhudia imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, hasa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Mashaka na wasi wasi ni sehemu ya mapito ya maisha ya waamini katika wito na imani; hapa ni mahali pa kujenga sera na mikakati ya kupambana ili kuondokana na mashaka yasiyokuwa na mvuto wala mashiko katika imani.

Padre Felix Mushobozi, C.PP.S. katika maadhimisho ya Miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania anapenda kuwauliza watanzania, Je, Masiha atakapokuja atawakuta wako namna gani katika masuala ya: Kisiasa, Kiuchumi, Kijamii na Kikanisa? Je, mambo yepi yanayowakwaza kiasi cha kundishwa kumwaminia na kumtumainia Kristo katika maisha yao kama Bwana na Mkombozi? Je, wanajiandaa namna gani kumpokea Kristo anayezaliwa kila siku ya maisha yao? Jambo la msingi ni kujikita katika: maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kuboresha maisha ya kisakramenti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.