2016-12-12 10:24:00

Mihimili ya majiundo na malezi ya Kipadre!


Utambulisho wa maisha na utume wa Kipadre unafumbatwa katika ufuasi wa Kristo, huduma makini ndani ya Kanisa na ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa maisha! Haya ni kati ya mambo msingi yaliyofafanuwa kwa kina na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Jumuiya ya Seminari ya Kanda ya Pio XI, ilipokutana naye mjini Vatican, tarehe Jumamosi, tarehe 10 Desemba 2016. Baadaye, Baba Mtakatifu aliamua kuzungumza na wanajumuiya hawa hili kuwashirikisha yale yaliyokuwa yamefichika katika sakafu ya moyo wake!

Baba Mtakatifu ameelezea kwa namna ya pekee, umuhimu wa wanawake watakatifu katika malezi na majiundo ya Kipadre kama ilivyotokea kwa Sr. Bernadetta aliyemsaidia sana katika malezi na majiundo ya Wanovisi nchini Argentina. Alikuwa ni mwanamke wa shoka aliyebahatika kuwa na heshima, akawasaidia majandokasisi katika safari ya maisha yao ya kiroho. Akiwa ni umri wa miaka 85 akabahatika kumpatia Mpako wa wagonjwa na baadaye, akafariki dunia. Baba Mtakatifu anapenda kuwashuruku wanawake wote wanaojisadaka kwa ajili ya malezi, majiundo na maisha ya kipadre; kwa ushauri na huduma yao ya kimama.

Baba Mtakatifu anasema, seminari ni mahali pa majiundo, lakini wakati mwingine ni mahali ambapo kumekuwa ni “kichaka” cha kashfa zinazovutia “magazeti ya udaku” ili yaweze kuuza magazeti yao! Malezi na majiundo ya kipadre ni changamoto pevu inayomtaka Jandokasisi kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake, daima akijitahidi kuwa ni Baba mwema na mhudumu wa Jumuiya inayomzunguka. Hiki ni kielelezo cha Ubaba katika maisha ya Kipadre kwa ajili ya kusaidia mchakato wa ukuaji wa maisha sanjari na kudumisha umoja na mshikamano katika maisha ya Kijumuiya, dhamana inayotekelezwa kwa ujasiri, nguvu na upendo.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, majandokasisi hawa ni 180 kutoka katika Majimbo ya Kanisa Katoliki, Kusini mwa Italia, changamoto ya kuendelea kujikita katika imani kutoka kwa wazazi wao ni mifano bora iliyoachwa na Maparoko wao wema na watakatifu; daima wakiwa na kumbu kumbu ya historia ya Kanisa, kwani historia ya wokovu ina Mapokeo yake. Kuna Mapadre wema na watakatifu ambao wameshiriki kikamilifu katika mchakato wa historia ya wokovu ambayo inaendelea hadi leo hii, changamoto ni kuhakikisha kwamba hata wao wanarithisha kwa wengine utamaduni huu, kwa kutambua majina ya watu wao!

Baba Mtakatifu anawataka majandokasisi katika malezi na majiundo yao, kuhakikisha kwamba, wanajiandaa kuwa karibu na watu, kwa njia ya unyenyekevu ili kweli ujumbe wa Habari Njema ya Wokovu uweze kuwafikia watu na hivyo kuwa ni sehemu ya maisha yao! Familia ya Mungu inakabiliwa na changamoto nyingi za maisha, kumbe ni wajibu wa Mapadre kuwasaidia watu wao.

Majandokasisi wasikimbilie Seminarini ili kupata elimu bora zaidi itakayowasaidia kuupatia umaskini kisogo, kwani mwelekeo huu ni potofu! Wanapaswa kujisadaka na kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza, kwa kuwa maskini kwa ajili ya maskini; Mama na kuta za kulinda wito na maisha yao ya Kipadre; kwani umaskini unakuwa ni chemchemi ya maisha na ngao ya maisha na utume wa Kipadre. Mapadre wajifunze na kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kukaa na watu wao; kwa kuwajali na kuwahudumia wagonjwa, wazee, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ukaribu wa wakleri kwa watu wao ni msaada mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Kanisa mahalia! Changamoto hii inakwenda sanjari na kujitaabisha kumfahamu Kristo Yesu kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Sala binafsi na za Kijumuiya kama sehemu ya mwendelezo wa maisha hata katika hali ya mchoko! Mtakatifu Theresa wa Mtoto Yesu anasema ni vyema kusinzia mbele ya Tabernakulo kuliko kupitiliza siku bila ya kwenda kumsalimia Yesu wa Ekaristi Takatifu, anayewaita na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji haina budi kujikita katika mchakato wa majadiliano endelevu kwa kumtumainia Roho Mtakatifu mhimili mkuu katika azma ya Uinjilishaji, tayari kung’amua kile ambacho Roho Mtakatifu anataka kwa ajili ya watu wake. Wakleri wanapaswa kujenga fadhila ya unyenyekevu mbele ya Roho Mtakatifu. Kumbe, Seminari iwe ni mahali pa kujifunza: kusoma na kusali ili kupata ujuzi, maarifa na stadi za maisha. Majandokasisi wajitahidi kusoma kwa bidii ili kujiandaa kikamilifu na changamoto zilizoko mbele yao kama Mapadre! Maisha ya Kijumuya na kazi za kitume ni mambo muhimu sana katika majiundo ya Kikasisi; mihimili hii mikuu ya maisha na wito wa Kipadre ipewe uzito unaostahili.

Baba Mtakatifu anawataka Majandokasisi kumkimbilia Roho Mtakatifu ili aweze kuwajalia karama zake, ari na moyo wa kimissionari, tayari kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Mapadre wawe na ujasiri wa Kibaba, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wazee na wagonjwa walioko kufani; kwa ajili ya kuwapatia Sakramenti wanaohitaji! Huu ni ushuhuda wa Padre anayejisadaka kwa ajili ya huduma kwa jirani zake. Baba Mtakatifu mwishoni, anawataka Majandokasisi kuwa wakomavu na kamwe wasiwe ni watu kupiga majungu, kwani kama majungu si mtaji, yangekuwa mtaji, wengi wangetajirika wengi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.