2016-12-10 15:29:00

OSCE tekelezeni majukumu yenu kwa kuonesha utashi wa kimaadili!


Mawaziri wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa kutoka katika nchi 57 wanachama wa Shirikisho la Kimataifa la Usalama na Maendeleo, OSCE wamehitimisha mkutano wao wa siku mbili uliofunguliwa tarehe 8 hadi 9 Desemba 2016 huko Amburg, Ujerumaini. Masuala ya kiuchumi na kisiasa kimataifa yalipewa msukumo wa pekee sanjari na mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi kimataifa pamoja na vita inayoendelea nchini Siria. Wamejadili pia kuhusu rufuku ya utengenezaji, ulimbikizaji na utumiaji wa silaha ya kinyuklia bila kusahau umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu!

Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican aliiwakilisha Vatican kwenye mkutano wa OSCE kwa kukazia umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani, usalama, ustawi, urafiki na maendeleo ya Jumuiya ya Kimataifa na kamwe raia wa OSCE wasiwe ni wahanga wa vitendo vya kigaidi, vita na ukosefu wa haki msingi za binadamu.

Nchi wanachama wa OSCE zinapaswa kuzingatia makubaliano ya itifaki ya Helsink yanayokazia pamoja na mambo mengine, haki, amani, usalama pamoja na kujikita katika mchakato wa majadiliano, kwa kuaminiana na kujizatiti katika usalama. Haya ni mambo makuu ambayo Ujerumani katika uongozi wake kama Rais wa OSCE inataka kuyapatia kipaumbele cha pekee kwa wakati huu. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, makubaliano haya yatatekelezwa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi kama sehemu ya wajibu wa wajumbe wa OSCE kimaadili.

Askofu mkuu Gallagher anakaza kusema, amani ni matunda ya zawadi ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inawajibika kimaadili kuhakikisha kwamba misingi ya haki, amani na usalama inalindwa na kudumishwa na wote, ili kuokoa maisha ya watu kutokana na vita pamoja na vitendo vya kigaidi. Inasikitisha kuona kwamba nchi wanachama wa OSCE zilishindwa kufikia maamuzi ya pamoja ya kusitisha vita huko Ukraine kwa kuhakikisha kwamba, sheria za kimataifa zinalindwa na wote.

Vatican kwa upande wake, itaendelea kuunga mkono sera na mikakati inayopania kudumisha amani, ushirikiano, maendeleo na utulivu pamoja na kuhakikisha kwamba, vita, kinzani na migogoro mbali mbali inasitishwa na amani inaanza kutawala kati ya watu. Ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama, kuna haja kwa wanawake kushirikishwa kikamilifu katika kuzuia pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu kwani hawa ndio waathirika wakuu wa vita, kinzani na migogoro ya kijamii. Dini zinaweza kuchangia kuzua vita na pale inaposhindikana basi zinaweza kusaidia mchakato wa upatanisho na kwamba, Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia limesaidia kuwapatanisha watu waliokuwa wanasigana na kukinzana. Ukanimungu na misimamo mikali ya kidini na kiimani ni hatari kwa mafungamano na ushirikiano wa kimataifa, kumbe inapaswa kudhibitiwa kwa kuzingatia uhuru wa kuabudu.

Katika masuala ya uchumi na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, uzoefu unaonesha kwamba: vita, kinzani na mipasuko ya kijamii inarutubishwa zaidi na woga pamoja na wasi wasi usiokuwa na mashiko; hali ya kutoaminiana na kukata tamaa; mambo ambayo ni matokeo ya umaskini wa hali na kipato. Kumbe, hapa kuna haja ya kujikita katika sera na mikakati ya uchumi shirikishi inayoheshimu utu wa binadamu na kusaidia ujenzi wa mafungamano ya kijamii.

Rushwa na ufisadi ni saratani mbaya inayoendelea kukwamisha mchakato wa maendeleo endelevu na matokeo yake ni kushamiri kwa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Pale ambapo rushwa na ufisadi vinashamiri, hapo maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi wanaumia na kuteseka zaidi anasema Askofu mkuu Gallagher. Haki msingi za binadamu zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote bila ubaguzi hata kidogo kwani huu ni msingi thabiti wa haki, amani na maridhiano kati ya watu. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki msingi za binadamu zinafumbatwa katika utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Ubaguzi wa kidini, rangi, jinsia na mahali anapotoka mtu ni hatari sana kwa amani, usalama na maendeleo ya kijamii. Matokeo yake ni: utumwa mamboleo; biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; biashara haramu ya silaha na matumizi yake; vitendo vya kigaidi na uhalifu wa magenge. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete ili kuhakikisha kwamba, vitendo hivi vinavyoruga na kudhalilisha utu na heshima ya binadamu vinatokomezwa kwa kuonesha utashi wa kimaadili na kisiasa.

Askofu mkuu Gallagher amezipongeza Serikali zote zinazoendelea kuwapokea na kutoa hifadhi kwa wakimbizi na wahamiaji, kwani hawa ni matokeo ya vita, kinzani, athari za mabadiliko ya tabianchi, dhuluma na nyanyaso za kidini na kikabila. Wakimbizi na wahamiaji kamwe wasiangaliwe kuwa ni kero kwa mataifa hisani, bali waheshimiwe, wasaidiwe na haki zao zilindwe, ili waweze kuchangia vyema katika ustawi na maendeleo ya nchi husika. Majadiliano katika ukweli na uwazi kwa kuzingatia haki za wakimbizi na wahamiaji, ili waweze kuwa kweli ni wakala wa maendeleo endelevu: kiuchumi na kitamaduni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.