2016-12-10 14:21:00

Majandokasisi wafundwe kumfuasa Kristo, kulitumikia Kanisa na Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 10 Desemba 2016 amekutana na kuzungumza na wanajumuiya ya Seminari ya Kanda ya Pio XI, kutoka Mkoani Puglia, Kusini mwa Italia waliokuwa wameongozana na Maaskofu wa Majimbo Katoliki Kusini mwa Italia. Amewapongeza kutokana na wingi wao na ametumia nafasi hii kupembua kwa kina na mapana utambulisho na utume wa Kipadre unaofumbatwa katika kumfuasa Yesu Kristo, utume katika Kanisa na Ujenzi wa Ufalme wa Mungu; mambo msingi yanayopaswa kumwilishwa katika majiundo ya majandokasisi tangu mwanzo kabisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hii ni dhamana inayopaswa kukuzwa, kudumishwa na kuendelezwa kwa umakini mkubwa sanjari na kuwajibika barabara. Mambo haya ni msingi kwa waseminari wanaojiandaa kuwa ni Mapadre wa kesho! Kwanza kabisa waseminari wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya Kristo, Kanisa na wadau katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, dhamana inayoanzwa kutekeleza tangu pale jandokasisi anapotinga seminari ndogo, kwa kuwa na mwelekeo mpana badala ya mtu kujitazama na kujitafuta ili kushinda ubinafsi, kishawishi ambacho ni hatari sana kwa maisha na utume wa Kipadre.

Kwa njia hii, majandokasisi wataweza kuona na kung’amua uzuri wa mafumbo yanayowazunguka, maisha ya juu zaidi, imani kwa Mwenyezi Mungu anayevitegemeza vitu vyote na kuwaenzi binadamu wote. Kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi watafanikiwa kumwona Kristo Yesu na kufurahia uzuri wa Kanisa, tayari kushiriki kikamilifu katika kazi ya ukombozi wa binadamu na ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani, tayari kujimanua na mambo yote yanayokwamisha mchakato huu. Kipindi cha Majilio ni mwaliko kwa waamini kukesha ili wasije wakatumbukia katika ubinafsi, kwani bila kukesha safari na maishana utume wa kipadre inakuwa ni bure na ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu!

Baba Mtakatifu anawataka majandokasisi kuwa ni watu wenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano mema na Kristo Yesu, wenzao wanaoshirikishana utume na imani pamoja na wale wote wanaokutana nao katika hija ya maisha yao ya kila siku, changamoto na dhamana inayoanza kufanyiwa kazi tangu seminari ndogo, kwa kuwa na maamuzi makini kutoka katika undani wa sakafu ya moyo wa mtu kwa kutaka kuwa ni mtu mwenye mahusiano mema.

Dhamana hii inaweza kupimwa na kuchunguzwa kadiri muda wa kupewa Daraja Takatifu ya Upadre unavyokaribia ikiwa kama unaongezeka na kukomaa. Ujenzi wa maisha ya Kijumuiya ni mchakato unaotekelezwa kila siku ya maisha seminarini kati yao na wale wote wanaokutana nao katika safari yao ya malezi. Waseminari wasidhani wala kujidanganya kuwa wao wako tofauti sana na vijana wenzao au kwamba, ni bora zaidi kuliko vijana wengine, bali wawe tayari kujifunza kwa kushirikiana na watu wote, kwani kama Mapadre wataishi na kufanya utume wao kati ya familia ya Mungu. Kumbe, huu ni mwaliko wa kujifunza kuishi na kujifunza kutoka kwa wengine, kwa unyenyekevu, akili na busara kwa kutambua kwamba msingi wa mahusiano yote haya ni Kristo Yesu. Majandokasisi wajitahidi kumfahamu, kumsikiliza na kujishikamanisha naye katika imani na mapendo yanayofumbatwa katika mahusiano yenye mashiko na ukomavu, ili kweli wawe ni vyombo na mashuhuda wa upendo wa Kristo kwa jirani zao. Mahali muafaka pa kukuza urafiki na mahusiano mema na Kristo Yesu ni katika sala na ukomavu wa sala unaojionesha katika upendo.

Baba Mtakatifu anawataka majandokasisi kujenga utamaduni unaowakumbatia na kuwafumbata wote pasi na ubaguzi; dhamana wanayopaswa kuanza kuitekeleza wakiwa seminarini, kwa kuwasaidia wale wote wanaojisikia kuwa wapweke, ili wao pia waweze kupelekwa na kuwa ni sehemu ya maisha ya Jumuiya. Katika ukuaji wao, watambue na kuonja uzuri wa udugu, changamoto ya kutoa na kupokea msamaha katika mambo madogo madogo na makubwa. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawataka wajitahidi kuwa na sura ya huruma, kama Baba wao wa mbinguni alivyo na huruma. Seminari hii ya Kanda imebahatika kutembelewa na neema na baraka ya Mungu kwa kuwa na majandokasisi wengi, kielelezo cha uwajibikaji, kwa kuzingatia ubora wa malezi na majiundo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.