2016-12-09 16:21:00

Vituko vya Yesu vilivyotikisa imani na matumaini ya Yohane Mbatizaji


Ndugu yangu msikilizaji wa Radio Vatican waswahili wana vituko eti “Mfungwa hachagui gereza”. Leo tunatembelea gereza moja lililoko kwenye kilima kidogo ndani ya ngome kamambe ya Makerus aliyoijenga Herode. Humo gerezani tunakutana na mfungwa Yohane Mbatizaji. Mwinjili Marko anasimulia vizuri kisa kilichompelekea Yohane kuswekwa lumande hebu tumsikilize. “Herode alituma watu kumkamata Yohana, akamfunga gerezani, kwa ajili ya Herodia, mkewe Filipo ndugu yake, kwa kuwa amemwoa; kwa sababu Yohane alimwambia Herode, Si halali kwako kuwa na mke wa nduguyo. Naye yule Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate. Herodia akawa akimvizia, akataka kumwua, asipate nafasi. Maana Herode alimwogopa Yohana; akimjua kuwa ni mtu wa haki, mtakatifu, akamlinda; na alipokwisha kumsikiliza alifadhaika sana; naye alikuwa akimsikiliza kwa furaha” (Mk. 6:17-20). Kwa hiyo kwa hoja za kisiasa na kimaadili, Herode alifadhaika sana, ili asiuawe akamsweka Yohane gerezani ili kumwepusha na ushabiki wa watu na pia kumlinda dhidi ya Herodia.

Mle gerezani Yohane alikuwa anapata taarifa ya mambo yanavyoendelea huko uraiani kutoka kwa waliokuwa wanamtembelea. Sanasana alikuwa anafuatilia kinachoendelea juu ya Yesu mnazareti. Kutokana na taarifa alizosikiasikia kwa watu, Yohane akatuma wanafunzi wake wakamwulize Yesu mwenyewe laivu: “Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine?” Swali hili limekuna vichwa vya wengi na yabidi tulitafakari kwa kina. Wahubiri wengi wanamsafisha Yohane Mbatizaji kwamba hakuwa na wasiwasi juu ya umasiha wa Yesu isipokuwa wanafunzi wake, ili kuwaondoa wasiwasi wao akawatuma kwa wakashuhudie wenyewe laivu. Maelezo haya ni potovu. Ukweli wa mambo ni kwamba, Yohane Mbatizaji mwenyewe ndiye aliyekuwa ametikisika kiimani. Kwa vyovyote Yohane alimtambua Yesu kuwa ni Masiha kwani ndiye aliyembatiza Yordani. Aidha, alimwonesha kwa wanafunzi wake na kusema: “Tazameni Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za dunia.” Hebu tuangalie vituko vya Yesu vilivyomtia mashaka Yohane Mbatizaji.

Kituko cha kwanza cha Yesu kilichoyumbisha imani ya Yohane ni kutokana na picha ya Masiha aliyofundishwa na wahenga wake hasahasa watawa wa jangwani Qumran alikolelewa. Yohane alifundishwa kuwa kuna mapambano kati ya waana wa mwanga (wema) na waana wa giza (waovu). Ndiyo maana alihubiri kwamba Masiha ajaye ni mcha Mungu, hana mchezo atafifisha waovu wote: makapi yatachomwa; shoka limewekwa kwenye shina la miti mibovu tayari kukatwa. Kumbe sasa anasikia kuwa Yesu anafanya kinyume chake. Badala ya kuwafifisha wadhambi, malaya, watoza ushuru, walevi ndiyo kwanza anaenda hadi majumba kwao kula na kunywa. Halafu alijisifia kwamba ni rafiki wa wadhambi. Yarabi tobaaa! Kwa kweli kwa wengi hii ilikuwa ni kufuru ya mwaka, lakini wakasahau kwamba, Yesu alikuwa ni ufunuo wa huruma ya Baba wa milele!

Kituko cha pili kinatokana na mafundisho ya Manabii juu ya Masiha ajaye kuwa angewahubiria na kuwakomboa wafungwa: “Roho wa Bwana yu juu yangu; kwa sababu amenituma kuwatangazia mateka uhuru wao, na waliofungwa habari za kufunguliwa kwao” (Isaya 61:1). Yohane aliye gerezani alisubiri kuhubiriwa na kokolewa. Kumbe, anajiona bado anasota tu kifungoni.

Ndugu zangu, endapo Torati na Manabii wote wa kale hadi watawa wa Qumrani walimwandaa vizuri Yohane mbatizaji kumwelewa Masiha, na ndiye aliyembatiza na kumshuhudia, lakini hata hivyo anakuwa na wasiwasi, hapo ujue pamelala siri ya fundisho la leo. Fumbo ni kwamba mawazo ya Mungu ni tofauti na ya kibinadamu. Kwa hiyo, endapo masiha hashangazi na hatufanyi kumstaajabia na kutuyumbisha kiimani, hapo ujue Masiha huyo hatoki kwa Mungu. Masiha wa Mungu ni tofauti sana na yule tunayemdhani kuwa ni mwenyewe. Masiha anayetujia anafanya mambo kadiri ya maagizo ya Mungu na siyo kadiri ya matakwa ya kibinadamu. Kutokana na swali la Yohane tunapata ujumbe mbalimbali kutoka kwa Masiha. Mosi, licha ya kwamba anafahamika kwa Yohane Mbatizaji kuwa ni Masiha, lakini Yesu hajibu kwa maudhi swali la wanafunzi wa Yohane, bali anakuwa mwema. Kumbe tunapokuwa na mashaka juu ya Yesu, yeye anakuwa mwema tu.

Pili, imani kwa Mungu anayefunuliwa kwetu na Yesu haituondolei mashaka na wasiwasi. Yohane mbatizaji ndiye mfano wa imani ya kweli na aliyejaa mashaka na maswali mengi, lakini hamkani Masiha, eti kwa sababu tu haingii kwenye vigezo alivyo navyo juu ya masiha. Tatu tunafundishwa kwamba imani inaendana na mashaka. Kama katika imani hakuna wasiwasi hapo ujue hujatambua bado jinsi Mungu anavyofanya mambo yake. Kumbe tunapoutambua uso kweli wa Mungu, sura ya mtu Yesu anayetuonesha, hapo kutaibuka mashaka, wasiwasi, na maswali kama ya Yohane Mbatizaji. Jibu la Yesu: “Nendeni mkamweleze Yohane yale mnayoyasikia na kuyaona.” Kisha anaorodhesha alama sita zinazoonesha kufika kwa ulimwengu mpya na kwa Masiha wa Mungu.

Alama ya kwanza: “Vipofu wanapata kuona.” Ujumbe huu ni alama tu ambayo Yesu anamkumbusha Yohane mambo yaliyoandikwa katika manabii juu ya masiha. Kwamba viziwi watasikia, viweze watatembea, vipofu wataona. Vipofu hawa ni wale waliokosa mwelekeo wa maisha kwani hawaoni hivi wanajikwa na kuwakwaa wengine. Kumbe wanapoangazwa na Injili  wanaweza kuona njia na kuendelea vyema na safari ya maisha kweli.  Alama ya pili, viwete wanakwenda, yaani baada ya kupokea Injili wanaweza kuanza tena kutembea.

Alama ya tatu wakoma wanatakaswa. Ukoma ni alama ya dhambi na watu wanawakimbia. Wanapokutana na Injili wanaponywa na kuwa wazuri tena na kurudi katika jamii zao.  Alama ya nne viziwi wanasikia. Hawa ni wale waliojifunga ndani yao wenyewe, wabinafsi, na wanajisikia wenyewe tu. Wanapoonana na Yesu wanasikia ujumbe mpya na wanaweza kuwasikiliza wengine. Alama ya tano wafu wanafufuliwa. Hapa haina maana ya kufa kibaolojia bali kufa kiutu. Utu wa kweli umelala katika kupenda, kwani tumeumbwa ili kupenda na kuwasaidia wenye shida. Mtu mbinafsi ni mfu lakini anapoonana na Injili anafufuka anakuwa mt una kupenda. Alama ya sita maskini wanahubiriwa habari njema. Watu hawa waliokata tamaa, sasa wanamsikiliza Yesu.

Kisha Yesu anasema: “Mwenye heri ambaye hakwazwi nami.” Hapo kwazo ni lile la upendo usio na mipaka, ndilo lililoyumbisha pia imani ya Yohane. Kipengee hicho kinayumbisha pia imani ya wakristu walio na fikra zao juu ya Mungu mwenye haki. Kumbe tunaposema kwamba Mungu ni wa haki na huruma ni kwa sababu hatamwadhibu yeyote kwa vile Yeye ni upendo tu. Mafundisho mengine mazuri ya Yesu tunayapata wanapoondoka wanafunzi wa Yohane, Yesu anaeleza juu ya Yohane: “mlienda jangwani kuangalia unyasi ukitikiswa na upepo.” Unyasi au tete ni ni alama ya kukosa msimamo. Unyasi unainama na kuinuka kadiri ya mwelekeo wa upepo. Kumbe Yohane anao msimamo imara. Tujifunze kujua na kupambanua kile kinachokuja kutoka kwa Masiha na kile kinachofika kutokana na vigezo vyetu na siyo pendera fuata upepo. “Mlienda kumwona mtu anayevaa mavazi meroro na laini? Wanaovaa nguo laini ni wale waliokufa kiimani, wanataka kufaidi mitindo ya maisha. “Mlienda kumwona Nabii, naamu ni mkuu zaidi ya nabii” kwani yeye ndiye aliyeandaa ujio wa Masiha.

Hatimaye Yesu anasema: “hakuna mtu aliyezaliwa kati ya wanawake ambaye ni mkuu kupita Yohane. Yule aliye mdogo katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko yeye.” Yaani hakuna nabii aliyepata kazi nzito kama Yohane. Aidha ukuu unamaanisha yule aliyeingia katika ufalme wa Mungu anakuwa katika nafasi ya pekee. Yule aliyepokea sura mpya ya Mungu, kadiri alivyopendekeza Yesu, huyo huona mambo mbele zaidi kuliko Yohane Mbatizaji. Tunamshukuru Yohane Mbatizaji kwa ujumbe aliotupatia hasa katika mashaka yake, kwa ushahidi wa maisha. Masiha aliyetuonesha sasa tunayo fursa ya kumtafakari vizuri, kumwona vizuri na kumpokea katika maisha yetu, tayari kumshuhudia kwa wengine kama chemchemi ya furaha, imani na matumaini!

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.