2016-12-09 15:07:00

Roho Mtakatifu na karama ya mang'amuzi katika maisha!


Roho Mtakatifu ni chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu inayoongoza tafakari za kipindi cha Majilio zinazotolewa na Padre Raniero Cantalamessa kwa Baba Mtakatifu Francisko, viongozi waandamizi na wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume mjini Vatican. Baada ya kutafakari kuhusu “Nafsi ya tatu ya Fumbo la Utatu Mtakatifu” Yaani Roho Mtakatifu, Ijumaa, tarehe 9 Desemba 2016, Padre Cantalamessa ameendelea kufafanua kuhusu Roho Mtakatifu na Karama ya Mang’amuzi katika maisha ya Kikanisa, maisha ya mtu binafsi pamoja na kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza watu wake!

Roho Mtakatifu na mang’amuzi ni mchakato unaomwezesha mwamini kuwa na mang’amuzi sahihi ikiwa kama kweli ni maneno ya Kinabii yanayotoka kwa Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu, kiasi hata cha kukiri kwamba Yesu Kristo ni Bwana aliyetungwa mimba na kuzaliwa kwake Bikira Maria. Hiki ni kipaji cha kuweza kung’amua kweli za kiimani zinazopaswa kuendelezwa au uzushi kudhibitiwa.

Mang’amuzi ya maisha ya Kikanisa anasema, Padre Cantalamessa ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na viongozi wa Kanisa kwa uaminifu mkubwa kwa kuzingatia “ufahamu wa waamini” “Sensum fidelium” kwa kusoma alama za nyakati na kuzifafanua katika mwanga wa Injili kwa kulingana na kila kizazi pamoja na kujibu maswali yanayojirudia rudia kuhusu maana ya maisha ya sasa na maisha yajayo. Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro wanapotangaza kweli za imani wanaongozwa na Roho Mtakatifu na kwamba, ukweli uliofunuliwa na Mungu, ambao umo katika Maandiko Matakatifu, umekabidhiwa kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu.

Kanisa linaweza kufundisha kwa mamlaka kamili kuhusu maisha ya uzima wa milele, kanuni maadili na utu wema, changamoto kwa waamini kuendelea kumwilisha tunu msingi za Kiinjili kwa kuikataa dhambi na kumkumbatia mdhambi anayetubu na kuongoka kama ilivyokuwa kwa Zakayo mtoza ushuru mbele ya Yesu au yule mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi akasamehewa dhambi zake, akarejeshewa utu, maisha na matumaini mapya. Hiki ni kielelezo cha mshikamano kati ya Fumbo la Umwilisho na maisha ya binadamu isipokuwa katika dhambi.

Umoja na mshikamano kati ya viongozi wa Kanisa ili kutafuta suluhu za matatizo na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa ni muhimu sana kama ilivyojitokeza katika Mtaguso wa kwanza wa Yerusalemu, kwa kuamua kumsikiliza kwa makini Roho Mtakatifu anayeliongoza Kanisa kwa njia mbali mbali. Kuna haja ya kuwa na imani kwa Roho Mtakatifu ili kuweza kufikia maamuzi mazito ndani ya Kanisa, daima Kanisa lisisite kumwalika Roho Mtakatifu katika maisha na utume wake.

Padre Cantalamessa anasema, mang’amuzi katika maisha ya mtu binafsi yanamsaidia mwamini kuweza kutambua karama zake na kwamba, hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu ambayo mwamini anakirimiwa kwa ajili ya kutoa ushauri kwa wengine kwa kuzingatia hekima na busara katika mwanga wa imani kama zawadi ya Roho Mtakatifu. Hapa kuna haja ya kuwa makini ili kuweza kung’amua kile ambacho Mwenyezi Mungu anataka kutoka katika maisha ya waja wake kwa kuwa na nia njema katika kutoa maamuzi yanayofumbatwa katika fadhila.

Jambo hili linawezekana katika mazingira ya sala, kwa kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha pamoja na kujiachilia mikononi mwa Roho Mtakatifu kama anavyokazia Mtakatifu Inyasi wa Loyola. Amani na utulivu wa ndani ni kigezo muhimu sana kinachofumbatwa pia katika mazingira ya sala endelevu, kwani Roho Mtakatifu ni wakala wa kwanza wa mchakato wa mang’amuzi ya maisha kwani hii ni Karama ya Roho Mtakatifu anayetakasa akili ya mwanadamu, ndiyo maana waamini wanaalikwa kuwasha daima taa ya uwepo wa Roho Mtakatifu katika maisha yao kwa njia ya kusikiliza, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu kama walivyofanya Mtakatifu Anthony na Francisko wa Assisi.

Neno la Mungu ni chemchemi ya ushauri makini unaopaswa kusindikizwa na utamaduni wa kuchunguza dhamiri, ili kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuzungumza na mja wake kutoka katika undani wa maisha yake, tayari kutubu na kumwongokea Mungu! Matunda ya tafakari hii anasema Padre Cantalamessa ni upyaisho wa maamuzi ya kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuongoza safari ya maisha ya waamini wake, ili waweze kusali na kujisadaka kwa Baba yao wa milele! Huu ni mwaliko wa kuondokana na kishawishi cha waamini kujifanya kutoa ushauri kwa Roho Mtakatifu badala ya wao kupokea ushauri huo, kwani Roho Mtakatifu anaongoza, kumbe, waamini wamwachie nafasi kwani wakiongozwa na Roho Mtakatifu, hawapo chini ya sheria!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.