2016-12-09 15:19:00

Mti wa Noeli mjini Vatican ni kielelezo cha mahangaiko ya watu!


Baba Mtakatifu Francisko amekutana na wadau mbali mbali walioshiriki kutoa Mti wa Noeli pamoja na Pango la Noeli ambalo limezinduliwa rasmi, Ijumaa tarehe 9 Desemba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Ni pango ambalo ni kivutio kikuu kwa waamini na watalii wanaotembelea Roma wakati wa kipindi cha Majilio na Noeli. Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, amewashukuru viongozi wa Kanisa na Serikali kutoka Malta, Trento na Bassa Valsugana.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee kabisa, amewashukuru watoto waliojisadaka kwa ajili ya kupamba Mti wa Noeli huku wakisaidiwa na “Mfuko wa Lene Thun” pamoja na vitengo vya tiba kutoka hospitali mbali mbali kama ushuhuda wa tunu msingi za maisha, upendo na amani, zawadi ambazo Kristo anawakirimia waja wake wakati wa Sherehe ya Noeli! Mti wa Noeli uliosimimamishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ni kazi ya Msanii Gozo Manwel Grech kutoka Malta anayeonesha mateso na mahangaiko ya wakimbizi na wahamiaji wanaotaka hifadhi, usalama na ustawi wa maisha nchini Italia. Hawa ni watu wanaokumbana na kifo machoni pao wanapokuwa njiani. Lakini, ikumbukwe kwamba, hata Yesu Kristo alipozaliwa hakupata nafasi kwenye nyumba za wageni na matokeo yake akazaliwa Pangoni Bethlehemu, akalazimika kutafuta hifadhi nchini Misri baada ya Mfalme Herode kutishia usalama wa maisha ya Mtoto Yesu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mti wa Noeli uliowekwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro ni kielelezo cha udugu, ushirikiano, ukarimu na mshikamano. Mapango ya Mtoto Yesu sehemu mbali mbali yawe ni kielelezo cha maisha ya waamini na jamii mbele ya Mungu; maisha ambayo pengine yamefichwa machoni pa watu wengi kutokana umaskini, hali ngumu ya maisha pamoja na mahangaiko ya ndani.

Mti wa Noeli ni mwaliko wa kumtafakari Muumba na hivyo kujikita katika mchakato wa kutunza mazingira kazi ya mikono yake. Mti na Pango la Noeli ni kielelezo cha ujumbe wa imani, matumaini na mapendo yanayofumbatwa katika Fumbo la Umwilisho, pale Yesu Kristo alipowajia watu wake katika hali ya unyenyekevu na upole pasi na makuu. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujifanya kama watoto wadogo ili waweze kung’amua wema wa Mungu na kutafakari Huruma yake iliyomwilishwa katika hali ya ubinadamu ili kuyaongoza macho yao! Mwishoni, amewatakia wote heri na baraka katika maadhimisho ya Sherehe ya Noeli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.