2016-12-09 15:35:00

Mchango wa Vatican katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Ebola!


Ubalozi wa Marekani mjini Vatican kwa kushirikiana na Baraza la Kipapa la haki na amani pamoja na Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis kuanzia tarehe 9 - 10 Desemba 2016 wanafanya mkutano wa kimataifa ili kupembua kwa kina na mapana mchango wa Vatican katika kupambana na mlipuko wa Ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi, kama mfano bora wa kuigwa katika mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Zika.

Mkutano huu unahudhuriwa na mabalozi na wanadiplomasia wanchi mbali mbali hapa mjini Vatican. Lengo ni kuimarisha mahusiano kati ya Kanisa na wahudumu wa sekta ya afya katika maeneo yaliyoathirika na mlipuko wa magonjwa haya ambayo yameacha madonda makubwa katika maisha ya familia na jamii nyingi huko Afrika Magharibi. Wawezeshaji wakuu wa mkutano huu ni Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani, Balozi Ken Hackett pamoja na Suzanna Tkalec kutoka Caritas Internationalis.

Katika utangulizi, Kardinali Peter Turkson amejikita zaidi katika huduma ya afya, uwajibikaji uliooneshwa na Vatican kwa waathirika; shughuli na mikakati ya kichungaji iliyoibuliwa ili kupambana na Ugonjwa wa Ebola. Kuibuka kwa mlipuko wa ugonjwa wa Ebola Afrika Magharibi na athari zake katika maisha na maendeleo ya watu wengi, kulimsukuma Baba Mtakatifu Francisko kuchukua hatua za haraka kwa kushirikiana na Makanisa Mahalia pamoja na Makanisa mbali mbali.

Makanisa yakafanikiwa kutoa huduma katika maeneo yao watu, kupata fedha na vifaa tiba; kutoa faraja na upendo kwa waathirika pamoja na familia zao pamoja na kutoa mwongozo kwa Shirika la Afya Duniani, WHO, ili wagonjwa waliofariki dunia kwa ugonjwa wa Ebola waweze kuzikwa kwa heshima kwa kuzingatia utu wa binadamu. Baraza la Kipapa la haki na amani kwa kushirikiana na wadau mbali mbali likaweza kuweka sera na mikakati ya kupambana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola. Kanisa lilitoa kipaumbele cha pekee kwa afya katika ujumla wake na Serikali pamoja na Mashirika ya misaada kimataifa wakasaidia kutoa tiba kwenye nchi zilizokua zimeathirika vibaya.

Maambukizi ya Ebola yalizuiwa kwa kuwa na vifaa tiba, magari ya kubebea wagonjwa, majengo maalum ya tiba pamoja na kutoa motisha ya malipo ya ziada kwa wahudumu wa sekta ya afya waliokuwa wanakabiliwa pia na uwezekano wa kuambukizwa ugonjwa wa Ebola. Kulikuwepo na ushirikiano wa hali ya juu kabisa na familia ya Mungu katika maeneo husika na fedha ikatolewa kwa ajili ya elimu, chakula na vifaa tiba kwa watoto wa shule na familia zao; msaada wa mambo msingi ulitolewa kwa familia zilizokuwa zimeathirika pamoja na kutoa huduma msingi kwa watoto yatima.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zilifanywa na Kanisa katika kudhibiti ugonjwa wa Ebola kwa kuliwezesha Kanisa kuwa ni mganga wa maisha ya kiroho na kimwili kwa watoto wake; kwa kuonesha ukaribu kwa waathirika na familia zao pamoja na kufundisha mambo msingi ya kiimani katika kukabiliana na ugonjwa wa Ebola. Wadau mbali mbali walishirikisha ushauri wao katika kupambana na hatimaye, kutokomeza ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi. Ili kufanikisha shughuli hii pevu, Baba Mtakatifu alipokea msaada mkubwa wa hali na mali kutoka kwa Wasamaria wema sehemu mbali mbali za dunia na hasa zaidi kutoka kwa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume yenye utume maalum kwa wagonjwa. Kanisa lilionesha ushuhuda wa Imani, matumaini na mapendo kwa waathirika wote katika kipindi hiki kigumu katika historia ya watu wa Afrika ya Magharibi anasema Kardinali Peter Turkson.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.