2016-12-06 11:39:00

Huruma, upendo na faraja ya Mungu ni kiini cha Mafundisho ya Kanisa


Mafundisho tanzu ya Kanisa yanafumbata huruma, upendo na faraja ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kujibidisha kuyafahamu Mafundisho ya Kanisa, ili kuonja furaha, huruma na upendo wa Mungu kwa wale wanaotubu na kumwongokea Mungu katika maisha yao. Tangu pale mwanadamu alipokengeuka na kuanguka dhambini, Mwenyezi Mungu ameendelea kumtafuta kama Mchungaji mwema anavyomtafuta Kondoo aliyepotea na anapomwona anafurahia na jirani zake.

Mwenyezi Mungu ni hakimu mwenye haki, faraja na mapendo anayetamani kila mwanadamu aokoke na kupata maisha ya uzima wa milele. Mwenyezi Mungu anamtambua kila mtu kwa jina na anawapenda na kuwathamini jinsi walivyo hata pale wanapokengeuka na kutoweka mbele yake, bado anajibidisha kuwatafuta, ili kuwaondolea giza linalofunika nyoyo zao, kiasi cha kushindwa kuona na kutambua huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Anatambua udhaifu na mapungufu ya binadamu kama ilivyokuwa kwa Kondoo aliyepotea! Mwenyezi Mungu anataka kuyaongoza maisha ya mwanadamu ili kumkirimia maisha yenye uzima wa milele!

Kwa ufupi, haya ndiyo yaliyosemwa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 6 Desemba 2016. Kondoo aliyepotea ni sawa na Yuda Iskariote aliyemsaliti Yesu kutokana na udhaifu wake wa ndani. Hawa ni sawa na watu wanao wakosoa jirani zao, kiasi cha kushindwa kutambua na kuonja maisha na sadaka inayotolewa na wengine. Hawa ni watu wasiotosheka wala kuridhika katika maisha; ni watu wanaotafuta njia za mkato katika maisha; ni wezi na mafisadi wa mali ya umma; wanafiki wanaoishi maisha ya ndumilakuwili.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, hali kama hii inajionesha wakati mwingine hata miongoni mwa Wakristo,  lakini kwa uchungu mkubwa anasema Baba Mtakatifu hata miongoni mwa watawa na wakleri. Kondoo aliyepotea anaonesha dalili za ugonjwa wa moyo kwani ni mtu anayembeba Shetani moyoni mwake, kiasi cha kupandikiza chuki, uhasama na mipasuko ndani ya Jumuiya, hali inayotengeneza giza katika maisha ya watu. Ni sawa na Yuda Iskariote, mtu aliyetangatanga kutafuta mwanga wa maisha lakini kwa bahati mbaya hakufanikiwa na matokeo yake ni kujikatia tamaa ya maisha. Yuda Iskariote akajinyonga, maana yake akatubu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, daima upendo na huruma ya Mungu katika maisha ya mwanadamu vitashinda giza na ubaya wa dhambi, kielelezo makini cha Mchungaji mwema na Kondoo aliyepotea. Noeli ni sherehe ya mwanga inayofukuza giza katika maisha ya mwanadamu, ili kuweza kumshangilia Neno wa Mungu kwa kishindo, baada ya toba na wongofu wa ndani. Kwa njia hii waamini wataweza kuonja faraja kutoka kwa Mungu na kamwe wasithubutu kwenda kutafuta faraja hii nje kwani huko watakiona cha mtema kuni na mpasuko wa maisha ya ndani.

Mdhambi anapotubu na kumwongokea Mungu, anaonja faraja, upendo na huruma ya Mungu, kwani hiki ndicho kiini cha mafundisho makuu ya Kanisa, mwaliko kwa waamini kukimbilia furaha na faraja ya Mungu katika maisha yao. Kipindi cha Majilio, kiwawezeshe waamini kumngoja Kristo Yesu ili aje kuwaokoa na kuwarudisha tena kwenye zizi lake yaani Kanisa. Waamini wamwombe Mungu neema ya kungoja nguvu ya Kristo anayekuja kuwafariji ili kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na mipaka na kufurahia maisha yanayobubujika kutoka katika Moyo wake Mtakatifu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.    








All the contents on this site are copyrighted ©.