2016-12-05 14:47:00

Tubuni dhambi zenu ili mwonje upya wa maisha kutoka kwa Yesu!


Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wakati huu wa Kipindi cha Majilio kumwachia nafasi Yesu Kristo ili aweze kuwaletea mageuzi katika maisha pamoja na kuwaondolea dhambi zao, lakini jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, wanaziungama dhambi zao kutoka katika undani wa moyo wao bila kuficha wala kuogopa, ili kweli waweze kuwa ni watu wapya wanaotembea katika mwanga wa maisha mapya.

Liturujia ya Neno la Mungu, inagusia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ambayo yanapaswa kufanyika wakati huu wa Kipindi cha Majilio kadiri ya Nabii Isaya, kama njia ya kumsubiria Masiha kama ilivyokuwa pia kwa Waisraeli katika Agano la Kale. Yesu katika maisha na utume wake, alikuwa anawaponya watu magonjwa na kuwaondolea dhambi zao, kiasi cha umati mkubwa wa watu kumfuasa ili kumsikiliza. Hii inatokana na ukweli kwamba, ujumbe wake, ulikuwa unagusa sakafu za maisha na mahangaiko ya watu! Yesu akawawezesha watu kuonja mabadiliko kutoka katika ubaya kuelekea katika wema kwa kufanya mabadiliko ya ndani kabisa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mwenyezi Mungu aliumba ulimwengu na vyote vilivyomo, lakini binadamu kwa kudanganywa na Shetani akatumbukia katika dhambi! Kumbe, ujio wa Kristo Yesu ni kutaka kumkomboa mwanadamu, kiini cha Habari Njema ya Wokovu, ili kuweza kumponya mtu kutoka katika undani wa maisha yake, kwa kumsamehe dhambi na kumwezesha kuwa tena mtu mpya, jambo ambalo lilionekana kuwa ni kikwazo kwa Mafarisayo waliohoji ukuu wa Yesu na uwezo wake wa kuwaondolea watu dhambi! Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Maria Madgalena alikuwa mrembo wa sura, lakini ndani mwake, alielemewa na dhambi!

Haya pia ndiyo yaliyomsibu yule mgonjwa aliyeletwa na Jumuiya yake mbele ya Yesu wakashindwa kuingia ndani kutokana na umati, lakini kwa imani yao juu ya nguvu na uwezo wa Yesu, wakatoboa paa na kumshusha mgonjwa mbele ya Yesu, akamwondolea dhambi zake na kumponya, kiasi cha kuwaacha watu waliokuwa wamemzunguka wakiwa wamepigwa bumbuwazi! Kunahitaji ujasiri wa imani, ili kuponywa magonjwa ya dhambi!

Baba Mtakatifu anawataka waamini kujiandaa kikamilifu ili kusherehekea Noeli kwa imani na matumaini kwamba, atawawezesha kuganga na kuwaponya magonjwa yao, lakini waamini waoneshe ujasiri na uthabiti wa imani. Yesu anawaponya waamini kutoka katika undani wao, ili waweze kuzaa matunda ya haki. Waamini wawe na ujasiri kutambua na kuonja ubaya wa dhambi katika maisha yao, tayari kumwendea Mwenyezi Mungu kwa ari na moyo; kwa toba na wongofu wa ndani, ili waweze kuwa kweli ni watu wapya. Wawe na ujasiri wa kutubu na kuungama dhambi zao zote, ili Yesu awasaidie kupunguza mzigo wa dhambi zao, tayari kutembea katika upya wa maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawataka waamini kumwomba Mungu aweze kuwakirimia ujasiri huu wa imani na maondoleo ya dhambi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.