2016-12-05 09:42:00

Mauaji ya kimbari Rwanda! Kanisa: kumbu kumbu na msamaha!


Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa ya kutafakari kwa kina na mapana kuhusu Kanisa Katoliki na mauaji ya kimbari nchini Rwanda, ili kuomba msamaha, tayari kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujikita katika huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya majereha ya maisha ya mwanadamu, tayari kuanza upya katika haki, amani, upendo na msamaha wa kweli.

Askofu Philippe Rukamba, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kwa niaba ya Kanisa Katoliki, lakini zaidi kwa wakleri, watawa na waamini walioshiriki kwa namna mbali mbali kwenye mauaji ya kimbari nchini Rwanda yaliyotokea kati ya Mwezi Aprili hadi Julai 1994 na kupelekea zaidi ya watu laki nane kupoteza maisha yao. Hii ni kumbu kumbu yenye machungu makubwa kwa maisha na utume wa Kanisa, lakini inawakumusha waamini na watu wote wenye mapenzi mema hasa wale walioguswa na kutikiswa na mauaji ya kimbari kuanza mchakato wa huruma, ili kuambata upendo wa Mungu unaoganga na kuponya machungu ya ndani yanayomsibu mwanadamu!

Askofu Rukamba ameyasema haya kufuatia waraka wa kichungaji uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Rwanda kama sehemu ya hitimisho la Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kwa kuomba msamaha kwa niaba ya Kanisa kutokana na baadhi ya watoto wake kushiriki katika mauaji ya kimbari nchini humo! Maaskofu wanasema, lengo la waraka huu wa kichungaji ni kusaidia mchakato wa uponyaji wa madonda ya vita ya wenyewe kwa wenyewe na hatimaye, mauaji ya kimbari.

Maaskofu wanaomba msamaha kutokana na mauaji haya ya kimbari ambayo kimsingi yalikwenda kinyume cha amri ya upendo kwa Mungu na jirani. Ni mauaji ambayo yamefumbatwa katika ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko, changamoto kwa sasa ni kujenga umoja na mshikamano wa familia ya Mungu nchini Rwanda. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa kukimbilia na kuambata msamaha na huruma ya Mungu kwa njia ya toba na wongofu wa ndani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.