2016-12-05 13:37:00

Mamlaka kwa mapadri waungamishi kuondoa adhabu ya utoaji mimba


Katika barua yake ya kitume Misericordia et misera, yaani Huruma na amani, Baba Mtakatifu Francisko kaeleza kuwapa mamlaka mapadri waungamishi wote kuondoa adhabu na kusamehe dhambi ya kutoa mimba. Kufuatia utaratibu huo mpya, baadhi wametoa taarifa mkanganyiko juu ya suala hilo katika maeneo mbali mbali duniani. Askofu Marcello Semeraro, wa Jimbo Katoliki Albano, Italia, amepeleka barua ya kichungaji kwa mapadri na watawa, akitoa maelekezo ya kuwasaidia waamini kuelewa tofauti kati ya dhambi na adhabu mintarafu Waraka wa wa kitume wa Huruma na amani.

Kanuni sheria za Kanisa, zinaitambua dhambi ya utoaji mimba kuwa ni moja ya makosa makubwa dhidi ya uhai wa mwanadamu, hasa katika hali ya unyonge wake. Kwa sababu hiyo adhabu iliyopo ni kwa wahusika kujitenga na Kanisa, hivyo kujizuia kupokea Sakramenti yeyote mpaka adhabu hiyo iondolewe. Adhabu ya namna hiyo katika Kanisa, ni Askofu au padri aliyeteuliwa na Askofu ndiye mwenye mamlaka wa kuiondoa adhabu hiyo, sio katika taratibu za mahakama kikanisa, bali katika Sakramenti ya kitubio. Mamlaka ya kuitoa adhabu hiyo kimahakama, nje ya Sakramenti ya Upatanisho, ni mahakama kuu ya Kanisa.

Tangu mwaka 1983 adhabu hiyo ilipowekwa na sheria kanuni za Kanisa, kumekuwa na magumu mengi na mahangaiko kwa upande mwingine, pale ambapo inakuwa vigumu kumpata Askofu kwa wakati au mapadri wachache walioruhusiwa kutoa adhabu hiyo. Hali kama hii ilipelekea waamini waliojutia dhambi hiyo, kujikuta wakikaa muda mrefu kabla ya kupata kuondolewa adhabu hiyo.

Kilichofanyika katika barua ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, Misericordia et misera, Huruma na amani, ni kurahisisha namna ya kuiondoa adhabi hiyo, kupitia Sakramenti ya Upatanisho. Kumbe Mama Kanisa sasa anawapatia mamlaka kisheria mapadri wote waungamishaji, kuweza kuondoa adhabu hiyo, na kisha kumuungamisha mhusika. Ieleweke vizuri hapa kuwa, kuna tofauti kati ya dhambi na maungamo, na kosa na adhabu.

Yeyote mwenye kuhusika katika harakati za utoaji mimba, kwa ushauri, kwa kuchangia fedha, kwa kuhudumu kwa namna yeyote, anakuwa ametenda kosa dhidi ya uhai wa kitoto hicho, na adhabu yake ni kujitenga na kujizuia kupokea Sakramenti yeyote, ikiwemo ya Upatanisho. Tendo hilo linabaki kuwa ni dhambi mbele ya Mungu. Lakini ili aweze kuondolewa dhambi hiyo, mhusika au mshiriki yeyote anapaswa kwanza aondolewe adhabu iliyomfunga kuungama, ndipo aungame. Awali kama ilivyoelezwa, adhabu hii iliondolewa na Askofu au mapadri wachache walioteuliwa. Kwa sasa adhabu hiyo inaweza kuondolewa na padri yeyote muungamishi, na kisha kumuondolea dhambi.

Sheria kanuni za Kanisa zina lengo kubwa la kuokoa roho za waamini, na sio kulipiza kisasi. Kila utaratibu, mazuio au adhabu zilizowekwa zina lengo la kumsaidia mwamini, kumrekebisha, kumtakasa, ili aweze kuirithi mbingu. Katika hali hii, utaratibu wa kuondoa adhabu ya wale walioshiriki katika utoaji mimba umerahisishwa, ili kuepuka mwamini aliyejutia kweli kweli kosa hilo kukaa na dhambi muda mrefu, na kuhatarisha wokovu wa roho yake.

Utaratibu huu haupunguzi uzito wa dhambi wala uzito wa kosa wala uzito wa adhabu. Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza juu ya uthabiti wa mafundisho ya Kanisa kwamba, ni dhambi na kosa kubwa kutoa uhai wa mwanadamu, na zaidi uhai wa mtoto aliye mnyonge au mzee au mgonjwa aliye katika mateso au kufani. Adhabu ya kosa la utoaji mimba inabaki kuwa ni ile ile ya kujifungia nje ya Kanisa na neema zinazoshirikishwa kupitia Kanisa. Kwa mwamini anayejutia rohoni mwake kosa na dhambi hiyo, na kudhamiria kutorudia na kuwa tayari kwa malipizi, Kanisa linamwekea sasa urahisi wa kufikia lengo hilo.

Kwa upande wa mapadri waungamishi, wakumbuke kuwa katika utume wao huo, wanao wajibu kujiandaa vema kuwasaidia kweli waungamaji kupata neema, kubadili mwenendo wao ili waweze kuokoka. Kwa sababu hiyo watawasindikiza kwa upendo katika safari yao ya kujipatanisha na Mungu. Kila Padre muungamishaji ni daktari wa kuiponya roho ya muungamaji, lakini pia ni hakimu wa haki, anayepaswa kutoa malipizi ya kumfaa muungamaji kutakasika kutoka kwenye makosa aliyotenda (Rej., Sheria Kanunbi za Kanisa, n. 978).

Mapadri wawabebe kondoo wa Kristo waliopotea, wawahangaikie ili waweze kurudi kundini baada ya kuwatoa katika hali ya upotevu na kuwaosha makosa yao. Wawafariji kwa upendo wa kibaba na utambuzi wao kuwa binadamu ni dhaifu na anahitaji msaada wa wengine, hasa walioandaliwa ili kuweza kupiga hatua. Hivyo ndivyo wataweza kuushinda uovu na udhaifu wao, kama asemavyo Mtakatifu Paulo: nayaweza yote kwake yeye anitiaye nguvu (Rej., Wafilipi 4:13). 

Kwa utaratibu huu mpya wa kuondoa adhabu ya utoaji mimba, uwe fundisho kwa kila mmoja kuiona huruma ya Mungu na kuepuka dhambi. Isidhaniwe hata mara moja kana kwamba imehalalishwa au imerahisishwa utendaji dhambi huo. Hapana, dhambi hiyo ni kubwa na ya kuogopwa, na kila mmoja aepuke kabisa kujiingiza katika mazingira ya utendaji dhambi hiyo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.