2016-12-05 08:56:00

Jiandaeni kuadhimisha Siku kuu ya B. Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili


Mwishoni mwa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 4 Desemba 2016 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana naye katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 8 Desemba.

Kadiri ya mapokeo tangu mwaka 1953 kwa mara ya kwanza Papa Pio XII alikwenda kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria mkingiwa dhambi ya asili iliyoko kwenye Uwanja wa Spagna, Roma. Mtakatifu Yohane XXIII akarudia tena tukio hili kunako mwaka 1958. Tangu wakati huo, viongozi wakuu wa Kanisa wameendeleza utamaduni wa kuweka shada la maua kwenye mnara uliojengwa na Kikosi cha zimamoto Italia na kuzinduliwa kunako tarehe 8 Desemba 1857.

Maadhimisho ya Mwaka huu ni mwendelezo wa utenzi wa sifa na shukrani kwa Bikira Maria mkingiwa dhambiu ya asili, Lango la huruma ya Mungu, aliyewawezesha waamini kuadhimisha kwa kishindo kikuu Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Kwa mwaka huu, siku hii itapambwa kwa sala, tafakari, maungamo. Jioni, Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kwenda kuweka shada la maua kwenye Sanamu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya asili, tukio ambao litahudhuriwa na viongozi wakuu wa Kanisa na Serikali mjini Roma.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.