2016-12-02 15:15:00

Yeeewoomi! Yohane Mbatizaji anatembeza mkong'oto pasi na huruma!


Pazia la Injili ya leo linapofunguliwa tunamwona Yohane mbatizaji – “Siku hiyo alikuja Yohane mbatizaji na alihubiri katika jangwa la Yudea.” Mtu huyu alikuwa na maisha safi ya kumcha Mungu na anawaalika watu waishi maisha safi ya kumcha Mungu. Kwake ubatizo ulikuwa alama ya mabadiliko ya akili na ya kiroho. Mtu huyu alitokea Jangwani ambako  Mungu aliwaongoza na kuwaandaa Wayahudi kuingia nchi Takatifu. Miaka arobaini ni kizazi kimoja cha binadamu, lakini ilikuwa ni miaka ya shida, mahangaiko na majaribu makubwa. Huko Wayahudi wengi walikiona cha mtema kuni.

Yohane Mbatizaji anatualika kukatafakari mang’amuzi waliyoyapata Wayahudi walipokuwa jangwani. Sifa mojawapo ya jangwani ni ukimya na hakuna makelele kama mijini na vijijini. Hayo ni mazingira mazuri ya kutafakari Neno la Mungu na juu ya maisha binafsi. Jangwani ni  mahali pa mapambano na ni mahali patupu, mwaliko wa kuingia katika undani wa maisha na kujianika mbele ya Mungu, tayari kutumbuliwa kwa yale yasiyofaa tayari kuvaa utu mpya unaojikita katika tunu msingi za Kiinjili na utu wema!

Aidha jangwani unahitaji mambo muhimu tu ya maisha, kila kitu kina thamani yake. Jangwani hakuna kubadilisha mitindo ya viwalo, hakuna vipodozi, hakuna luninga, nk. Hali hiyo inasaidia kutafakari vizuri bila kuelemewa na mambo mengi. Sifa ya tatu jangwani husafiri pamoja bila kutengana kuchelea kupoteana. Nasi tunaalikwa kusafiri pamoja bila kutengana katika maisha yetu. Yohane mbatizaji mwenyewe alilingana kabisa na madai ya kuishi jangwani kwani, ‘‘Alivaa vazi lililotengenezwa kwa singa za ngamia na mkanda wa ngozi kiunoni mwake, chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwitu” Mavazi na chakula cha Yohane yalilingana na ya manabii wa kale, yaani Yohane aliacha mambo ya yasiyo ya maana ya ulimwenguni na kuridhika na mambo muhimu ya maisha. Yohane alisema: “Tubuni, kwa maana Ufalme wa Mbinguni u karibu.” Neno “tubuni” kwa kigiriki metanoeite lina maana ya ongokeni au badilikeni. Huko ni kuongoka au kubadilika fikra na namna ya kuwaza. Kwa hiyo tukitaka kupokea ujumbe utokao kwa Kristo tunaalikwa kubadili fikra kwa sababu, “Ufalme wa mbinguni u karibu.” Kwa Kigiriki kukaribia ni Eggiken yaani kukaribia kiasi cha kuweza kuugusa au kuushika kwa mikono.

Hebu sasa tuangalie sehemu walizotoka watu waliomwendea Yohane Mbatizaji:“Watu walimwendea kutoka Yerusalemu, Uyahudi yote na nchi zote za kando kando ya mto Yordani.” Inatajwa nchi ya Yuda (Uyahudini) iliko Yerusalemu. Nchi hii ilijiona imejikomboa. Wananchi wake waliridhika na hali ya maisha hasahasa ya mambo ya dunia.

Watu hao walialikwa kufika mto Yordani. Mto huu haukuwa mkubwa na maarufu kiuchumi kama ilivyokuwa mito kama Nile, au Tigri na Eufrate kwa sababu hakukuwa hata mji mmoja mkubwa au mdogo uliojengwa kandokando yake. Umuhimu pekee wa mto Yordani ni kwamba, ulikuwa ni mpaka unaotenganisha nchi ya utumwa na nchi huru. Taifa la Waisraeli pamoja na Yoshua walivuka mto huo wakitokea utumwani na kuingia nchi huru ya ahadi ndiyo maana walijisikia wameshakombolewa. Kuvuka mto maana yake ni kuacha ya kale na kuanza kuambata maisha mapya! Ni sawa na Kisima cha Ubatizo kinachowakirimia Wakristo maisha mapya katika Fumbo la Pasaka!

Tuangalie sasa aina ya watu waliomwendea Yohane kule mpakani kama walikuwa huru au la: “Walikuja kuungama dhambi zao.” Watu hawa walijitambua kuwa wamekamatika, wamenasika, wanajisikia kuwa ni watumwa pengine hata wengine waliogopa “kutumbuliwa na Yohane Mbatizaji”. Kumbe, hatua ya kwanza ya kufanya ukitaka kubadili fikra ni kujitambua kuwa u mtumwa yaani mkosefu, mtu unayehitaji kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Kama hujijui kuwa u mtumwa wa miungu wako wadogo wadogo, huwezi kubadilika, badala yake utaridhika na hivi huwezi kuingia katika nchi ya uhuru. Utaendelea kutenda kwa mazoea na kushindwa kusoama alama za nyakati! Hapa unaweza kujikita ukisoma namba hadi ile ya mwisho yaani 1 hadi 0!

Halafu sasa tuangalie tabia ya makundi mawili ya watu wanaomjia Yohane na mtazamo wao: “Mafarisayo na Masadukayo wengi walikuja ili kubatizwa.” Makundi haya mawili yalikuwa miamba ya taifa lakini yalitofautiana itikadi.  Wasadukayo: walijikita katika mambo ya ulimwengu huu hasa katika masuala ya uchumi. Walisharidhika na maisha. Kwa hiyo wanaenda kwa Yohane kwa ajili ya kumsanifu tu na kujua anaongea kitu gani. Sana sana wanataka kutafuta kitu kinachoweza kuwasadikisha na kuwafanya wabaki katika maisha yao. Kwa namna fulani watu hawa ni watumwa wa utajiri wao na hawahitaji ulimwengu mpya.

Wafarisayo wao walijikita katika masuala ya imani na dini. Hakuna Mungu mwingine isipokuwa Yahwe aliye Bwana na mtawala anayetoa amri nao wakitii wako salama. Kumbe, watu hawa hawakujua kwamba walikuwa watumwa wa fikra zao zilizokuwa kinyume cha Mungu mleta uhuru wa kweli na wa upendo, ambaye ni Yesu mwenyewe. Yohane Mbatizaji anapowaona tu akawalipua: “ Enyi wazao wa nyoka, ni nani aliyewaonya ninyi kuikimbia hasira itakayokuja?” Wanalinganishwa na nyoka wanaotoroka kichaka kinapoungua moto yaani wanautoroka moto wa upendo wa Mungu unaoteketeza fikra na mawazo wanayoyatetea na kuyalinda. Chachu ya Wafarisayo ni uovu ule unaotusahaulisha na Neno la Mungu. Sumu ya Wasadukayo ni utajiri wa ulimwengu huu. Yohane anatumia lugha ya kutisha ya moto na hasira ya Mungu. Hizo ni picha za upendo wa Mungu anapoona watoto wake wako katika hatari ya kugongwa na nyoka wenye sumu yaani dhidi ya uovu, anauwakia hasira na kuuteketeza kwa moto ili kumwepusha na hali mbaya ya dhambi.

Anawaagiza kwa nguvu zote: “Zaeni matunda yapasayo toba; wala msiwaze mioyoni mwenu kwamba, Tunaye baba, ndiye Ibrahimu; kwa maana nawaambia ya kwamba Mungu aweza katika mawe haya kumwinulia Ibrahimu watoto.” Yesu hajali hadhi ya ubaba wa kibaolojia wa waana wa Abrahim kwani inabidi waana wawe na imani inayopokea mwito wa Mungu wa kuongoka. Yaani kupokea mwito unaotujia kwa njia ya manabii walio kati yetu wanaowakilisha ujumbe wa ukombozi. Siyo ukombozi wa kwenda paradisini, bali ukombozi unaotufanya tuishi sasa maisha halisi na ya kweli. Aidha picha ya shoka siyo la kukata watu bali linakata miti na mizizi ya uovu iliyo ndani ya moyo wa binadamu inayomzuia asizae matunda. Injili au Neno la Mungu linafika kuchenga na kung’oa mizizi ile yote inayotufanya tuchague mambo ya ovyo na kutuzuia tusizae matunda mema. Aidha Yohane anasema: “Mimi nawabatiza kwa maji. Lakini nyuma yangu anakuja Yeye anayekuja atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” Maana yake huyo ana nguvu ya mbingu ambayo ni upendo unaotusukuma kuishi kadiri ya msukumo wa mpango wa Mungu.

Picha nyingine, ni ya mazingira ya wakulima wa Uyahudi, kwamba “Ameshika pepeto mkononi mwake, naye Atatapepeta ngano na kuziweka ghalani na makapi yataunguzwa kwa moto usiozima.” Upepo unaopeperusha ni Neno la Injili na makapi au mapetelo ni maganda, uchafu au takataka za ngano. Makapi hayo ni mambo yasiyo ya maana. Kuna baadhi ya mambo tunayoyapatia thamani kubwa kumbe hayana maana, ni mapepeto tu. Kwa hiyo Neno la Injili linapuliza takataka zote.  Tunaalikwa kulipokea Neno hilo tuliache lipulize takataka zote za maisha yetu. Tuuache upepo wa Injili upulize akili zetu, upepete namna yetu ya kufikiri, na ya kuwaza, ipulize mitindo potovu ya maisha, ipulizie mbali hekima ya ulimwengu. Injili ipulize mawazo ya majivuno, ya dharau na ya kukandamiza inayotuzuia tusiishi kama binadamu kweli.

Neno la Mungu lipulize takataka za hasira, za chuki, za wivu, za ubinafsi unaotufanya tuuone ulimwengu wetu mdogo na kujifungia ndani yetu. Huu ndiyo upepo ambao Yohane mbatizaji anatualika tuache upulize kila sehemu, hata kwenye makabati mlimolundikana mali kama vumbi tusizohitaji kabisa, ambazo zingeweza kuwafaa wengine, hizo zipepetwe na Neno la Injili. Wakati huu wa Majilio tunaalikwa kutathmini maisha yetu kati ya kile kinachofaa na kisichofaa dhidi ya upepo huo sanjari na kuwathamini jirani zetu kwa kutambua utu na heshima yao kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.