2016-12-01 06:50:00

Vyuo vikuu ni mahali pa kukutana na kuonja huruma na upendo wa Yesu


Vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwa hakika ni mahali panapofaa sana kuwa nyumba ya Zakayo, mahali ambapo watu wanaonja: huruma, ukarimu na kupata nafasi ya kukutana na Kristo Bwana. Yeyote anayejikuta sehemu za vyuo vikuu, hasa wanafunzi wanaotoka sehemu tofauti na wenye tamaduni tofauti, inafaa wajisikie nyumbani na kuonja upendo kutoka kwa majalimu na wahudumu wengine mahali wanapojikuta ugenini. Akifungua kongamano la nne la kimataifa la huduma za kichungaji kwa wanazuoni, siku ya Jumatatu tarehe 28 Novemba 2016, Kardinali Antonio Maria Vegliò, Mwenyekiti wa Baraza la ya Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum, ameelezea umuhimu wa kuwajali kwa ukarimu wa kifamilia wanafunzi wanaosoma mbali na nchi zao.

Kongamano hilo linalofanyika kwa siku tano, linatoa fursa ya majadiliano ya Barua ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko, Evangelium gaudium, yaani Furaha ya Injili, na changamoto za kimaadili kwa vijana wasomi, katika harakati za kutengeneza jamii bora. Katika ufunguzi wake, akiwakaribisha washirki wa kongamano hilo kutoka mabara yote matano, Kardinali Antonio Maria Vegliò, kasisitiza kutafuta mbinu mpya za kichungaji na ufundishaji ujumbe wa Kristo, zinazoweza kukabili mabadiliko ya kasi katika jamii yanayotokana na utandawazi, ambapo kizazi kipya kimo hatarini zaidi kuyumba kimaadili. Baadaye Kardinali Antonio Maria Vegliò, aliwasilisha mada juu ya furaha ya Injili inayojaa mioyoni na maishani mwa wale wote wanaokutana na Kristo Yesu. Akitolea mfano wa Zakayo, Kardinali Vegliò anaeleza kwamba, kila mkristo ni mjumbe wa Kristo na anapaswa apokelewe hivyo.

Zakayo anatafuta kumuona Kristo, anaufungua moyo wake na nyumba yake ili kumkaribisha. Ukarimu ni hatua ya kwanza ya kufahamiana, jambo ambalo linahitaji ujasiri. Kwa upande mwingine, wanafunzi wanaojikuta ugenini, wajifunze pia kufunguka na kupokea tamaduni mahalia, na mambo mapya. Kila mmoja akiwajibika namna hiyo watajenga mahusiano mazuri, na kujisikia kweli ndugu wanaoshirikishana fadhila na karama mbali mbali. Kama ambavyo anafundisha Mtakatifu Yohane Paulo II, shughuli za fikra, lazima zijengwe katika fadhila za kimaadili kama vile uwazi, ukweli, ujasiri, na haki. Hekima ya kweli ni ile inayoleta furaha, na kumfanya mwanadamu kuingia katika umoja na Mungu ndani ya Utatu Mtakatifu.

Katika fadhila za maadili na umoja na Mungu, mwanadamu atasaidiwa kuepuka kutenda mabaya, naye atakuwa chombo cha furaha na amani kwa wengine. Kumbe ni lazima wakristo katika kujifunza mambo na kufanya utafiti, wajikite katika hekima ya kimungu ili kuwa na ufahamu wenye misingi ya kweli, na sio fikra au tamaa binafsi zinazomwangusha mwanadamu katika makosa. Kardinali Antonio Maria Vegliò, ametoa angalisho kwa vijana wa leo kutofuata mkumbo na kuvutiwa na mambo yanayopita, mambo yanayoonekana kuwapatia furaha, lakini ni furaha isiyodumu, na zaidi sana huwaharibia maisha, bali katika elimu wapate mwanga wa kuwasaidia kuepuka mmonyoko wa maadili, na kuwapa fursa ya kuishi na kumshuhudia Kristo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.