2016-12-01 14:27:00

Kanisa linataka kuwajengea vijana nguvu ya utandawazi wa mshikamano!


Kongamano la IV la shughuli za kichungaji kimataifa ni muda muafaka wa kutafakari kuhusu changamoto za kimaadili ili kujenga jamii bora zaidi, mwaliko kwa vijana wa kizazi kipya kuchukua mwelekeo huu kwa kutambua wajibu wao katika uhalisia wa maisha, tayari kuwa wajenzi wa jamii bora zaidi kwa siku za usoni! Vijana wanapaswa kuwa ni kielelezo cha ushuhuda kwa wale wanaoamini katika usemi na mwenendo; na katika upendo, imani na usafi na kamwe wasithubutu kuwaachia watu kuchezea wala kudharau ujana wao.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 1 Desemba 2016 alipokutana na kuzungumza na washiriki wa kongamano la IV la shughuli za kichungaji kimataifa linaloendelea mjini Vatican. Ulimwengu mamboleo una changamoto nyingi zinazopaswa kufanyiwa kazi hasa na vijana wa kizazi kipya ili kujikita katika ukweli na tunu msingi za maisha. Kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na utashi wa kutenda mema, vijana wenyewe wanaweza kuvuka vikwazo vinavyojitokeza katika maisha yao, kwani kamwe vikwazo si tishio katika mchakato wa ujenzi wa dunia inayojikita katika ubinadamu. Kamwe vijana wasikate wala kukatishwa tamaa, kwani Roho wa Kristo atawaongoza ikiwa kama watasikiliza sauti yake!

Baba Mtakatifu anasema kwa bahati mbaya ulimwengu wa akili na maarifa unawaelekeza wasomi kujitafuta wenyewe bila kuzingatia uwepo wa jirani zao, changamoto ni kujenga mtindo wa maisha ambao unajikita kwa namna ya pekee katika mshikamano, kwa ajili ya mafao ya wengi, haki na amani. Kwa njia hii wasomi wanaweza kujenga jamii safi zaidi, kwani fursa ya kusoma inawawezesha kuwajibika kwa ajili ya mafao ya binadamu wote.

Elimu ni njia makini inayomwezesha mwanadamu kupata maendeleo endelevu katika jamii. Kupata fursa ya kusoma nje ya nchi yako anasema Baba Mtakatifu ni nafasi ya kupanua wigo wa utamaduni kwa kufahamu lugha mpya, mapokeo, mila na desturi za watu wengine, changamoto kwa wanafunzi ni kujifunua na kujiweka wazi kwa wengine, hali inayowataka wenyeji pia kuwa na wakarimu na watu wa maridhiano. Kwa njia hii, kutaongezeka uwezo wa mahusiano, hali ya kujiamini pamoja na kuwaamini wengine; kwa kuwa na mwono mpana zaidi kwa siku za usoni na hapo unakua ni mwanzo wa hamu ya kujenga kwa pamoja mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu anasema, shule, taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu ni mahali muafaka wa ujenzi wa mchakato wa maendeleo yanayojikita katika mshikamano kama sehemu ya Uinjilishaji katika taaluma kama hali ya kukamilisha. Kumbe, ni wajibu wa walezi na wadau wa shughuli za kichungaji kuhakikisha kwamba, wanawajengea vijana upendo wa Injili, ari na hamu ya kutaka kuimwilisha, kuishuhudia na kuwatangazia vijana wengine. Wanafunzi wanaosoma nje, ni fursa ya kukua na kukomaa kiutu na kitamaduni, tayari kurejea nchini mwao ili kuchangia katika mchakato wa kutangaza na kuwashirikisha wengine furaha ya Habari Njema ya Wokovu. Elimu iwawezeshe wanafunzi kuwa na mawazo yakinifu, kwa kufikiri kwa makini ili kuwa na uhamasishaji wa ukuaji wa tunu msingi za kimaadili. Vijana wafundwe kuwa na kiu ya ukweli badala ya uchu wa madaraka; wawe tayari kusimama kidete kutetea tunu msingi za maisha na kumwilisha huruma na upendo, mihimili mikuu ya jamii iliyo bora zaidi.

Utajiri mkubwa wa wanafunzi unawawezesha kuingia kwa urahisi zaidi katika ulimwengu wa kazi, kwa kuwa na nafasi katika jumuiya na kuwa ni sehemu ya jamii husika. Jamii inahamasishwa kuhakikisha kwamba, inatoa fursa za ajira kwa vijana wa kizazi kipya badala ya kuendelea kuwalaumu vijana wanaokimbia nchi zao ili kutafuta malisho ya kijani kibichi zaidi. Kwa kijana anayeamua kwenda kuongeza ujuzi na maarifa nje ya nchi yake, liwe ni jambo bora na la busara, lakini inasikitisha na kuumiza sana, kuona vijana waliosomeshwa na nchi wanazikimbia nchi zao kwa sababu hawana fursa ya kuweza kushirikishwa!

Baba Mtakatifu anasema, wanafunzi wa kimataifa ni sehemu ya utandawazi wa kimataifa unaovuka mipaka na muda, kiasi cha kuwawezesha wanafunzi kukutana na kubadilishana tamaduni. Lakini pia, kwa bahati mbaya wanakutana na watu wanaojihami na kuta za ndani zinazowatenga watu kiasi cha kushindwa kuangalia mahitaji ya jirani zao, hali ambao inapelekea utandawazi wa kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kanisa linataka kuwajengea vijana nguvu ya utandawazi wa mshikamano unaofumbatwa katika uhalisia wa maisha, ujasiri wa Kiinjili pamoja na kuwafunda vijana wa kizazi kipya kuwa wainjilishaji watakaoshirikisha furaha ya Injili ya Kristo hadi miisho ya dunia.

Mwishoni Baba Mtakatifu anawaambia vijana watambue kwamba, wao ni sehemu ya mapambazuko ya asubuhi, wawe na ujasiri wa kumwangalia Kristo na historia, ili kutangaza na kushuhudia wokovu wa Yesu Kristo na kuwapelekea wengine mwanga wake ili uweze kuwaangazia wale wale ambao wamegubikwa katika giza la kutojali, ubinafsi na vita.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.