2016-11-30 15:42:00

Wanasiasa kiteni mchango wenu katika uhuru, usawa na udugu kati ya watu!


Familia ya Mungu nchini Ufaransa ina utajiri na uwezo mkubwa unaofumbatwa katika utofauti wake, fursa ambayo ikitumiwa vyema, itawezesha tunu msingi za maisha ya hadhara kama vile: uhuru, usawa na udugu kuchanua na kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa kujenga na kuimarisha jamii katika mambo msingi. Hizi ni tunu ambazo zinafahamika na wengi na sasa zinapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 30 Novemba 2016 alipokutana na kuzungumza na kundi la Maaskofu Katoliki kutoka Ufaransa lililokuwa linaongozwa na Kardinali Philippe Barbarin pamoja na wabunge 260 waliochaguliwa hivi karibuni katika Mkoa wa Rhòne- Alpes, huko Ufaransa. Ujumbe huu ulikuwepo mjini Vatican kwa hija ya maisha ya kiroho, kama sehemu pia ya mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, Jumuiya ya Kimataifa kwa sasa inakabiliwa na hofu, wasi wasi na vitisho vya mashambulizi ya kigaidi ambayo kwa siku za hivi karibuni, yameitikisa Ufaransa, lakini sasa kuna umuhimu wa kujizatiti kikamilifu kutafuta ustawi na mafao ya wengi hasa katika ulimwengu huu unaokabiliwa na mabadiliko makubwa, ili kuweza kupata maana ya siasa.

Hii ni tema iliyopembuliwa na kutolewa Waraka na Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa kwa siku za hivi karibuni, lakini Baba Mtakatifu anasema, yeye anapenda kufanya rejea kwenye Waraka wa Maaskofu wa Ufaransa uliochapishwa takribani miaka ishirini iliyopita “Rèhabiliter la politique” unaokazia: uhuru,usawa na udugu. Katika majadiliano ya kisiasa, wanasiasa Wakristo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika majadiliano na waamini wa dini nyingine duniani pamoja na watu wenye mapenzi mema ili kujenga na kudumisha ulimwengu ulio bora zaidi, kwa kujikita katika kutafuta mafao ya wengi na huduma kwa wakimbizi na wahamiaji.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hawa ni watu wanaokimbia vita, hali ngumu ya maisha kwa kutafuta ulinzi, usalama na maisha bora zaidi. Kumbe, wanapaswa kusaidiwa kwa hali na mali. Huu ni uwajibikaji wa kisiasa unaoweza kusaidia mchakato wa ujenzi wa jamii mpya inayosimikwa katika haki, utu, ukarimu na udugu. Baba Mtakatifu amewatakia heri, baraka na mafanikio mema wanasiasa hawa wanapotembea kufuata nyayo za Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini na dhamana yao ya huduma kwa mafao ya wengi.

Wakati huo huo, Siku ya Jumatano asubuhi, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na kuzungumza  kwa faragha na Bwana Martin Scorsese, mcheza filamu mashuhuri kutoka Amerika. Hivi karibuni amemaliza kucheza filamu inayokwenda kwa jina “Silence” itakayooneshwa mjini Vatican, siku ya Alhamisi tarehe 30 Novemba 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.