2016-11-29 13:57:00

Kardinali Fiorenzo Angelini mfano wa Injili ya ukarimu na upendo


Tangu akiwa padre kijana, Fiorenzo Angelini, aliwajali sana wale waliokuwa hawana makazi, akiwa Kardinali, utendaji wake wa msaada na ukarimu ulipanuka kwa dunia nzima, kiasi cha kuanzisha uchungaji wa huduma za afya. Kardinali Pietro Parolini, Katibu mkuu wa Vatican, kaongoza Misa Takatifu, tarehe 22 Novemba 2016, kumkumbuka Kardinali Fiorenzo Angelini aliyefariki dunia miaka miwili iliyopita.

Kuongoka na kumfuata Kristo ndicho kinachomletea mwanadamu wokovu, na sio ukubwa au ufahari wa mambo mengi anayofanya duniani. Hivi ndivyo Kardinali Angelini alifanya, akitambua umuhimu wa kuongoka, alimshuhudia Kristo kwa matendo ya imani na ukarimu, na hivyo kuiweka hai Injili ya upendo. Kwa hakika utendaji wake ulijikita katika bidii ya kumshuhudia Kristo, na alikuwa na nguvu ya aina yake katika kushughulikia miradi na mipango ambayo Mungu aliiweka mbele yake.

Kardinali Fiorenzo Angelini alikuwa mtii kwa shughuli alizopewa na wakubwa wake, lakini pia alijua namna ya kukabiliana na kujibu changamoto zilizojitokeza katika utendaji wake wa kila siku, kiasi kwamba kwa kila aliyemhitaji, alikuwa na uhakika atapata kusikilizwa na kusaidiwa. Kwa kweli alikuwa ni mtu wa Injili, kwa maneno na kwa matendo.

Lengo la utendaji wa Kardinali Fiorenzo Angelini, lilikuwa kuinjilisha jamii kupitia huduma za afya, huduma ambazo alizipa kipaumbele moyoni mwake. Katika huduma zake na utendaji wake, aliwashirikisha wote kadiri ilivyowezekana, akijitahidi kuonesha mfano wa Kristo, msamaria mwema, kwa kujali wanyonge zaidi. Ndivyo alivyoanzisha utamaduni wa utendaji kikristo kwa madaktari, akawatia moyo mapadri walezi katika hospitali na akatoa mchango mkubwa katika kukuza utafiti wa kisayansi unaojali zaidi utu wa mwanadamu. Kati ya kumbukumbu kubwa za Kardinali Angelini ni kuanzishwa kwa Taasisi ya Kipapa ya huduma za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta za afya, ambapo akawa Mwenyekiti wake wa kwanza.

Akiwa na mtazamo wa Kanisa la kilimwengu, alipania kutembelea Cuba na Umoja wa Kisovieti. Itakumbukwa pia Hospitali iliyojengwa Moscow ili kutetea utu wa mwanadamu mbele ya magonjwa. Hospitali zingine ni pamoja na zile zilizojengwa India, Poland, Romania na katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu wa Congo.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.