2016-11-28 08:19:00

Uchumi usaidie ujenzi wa maisha na utume wa Kanisa mahalia!


Umefika wakati kwa Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kufanya upembuzi yakinifu kuhusu sera na mikakati ya kiuchumi; rasilimali fedha pamoja na utekelezaji wa shughuli za kitume zinazofanywa na Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kama sehemu ya umwilishaji wa karama hizi katika maisha na utume wa Kanisa. Utekelezaji huu unahitaji kwa namna ya pekee, uaminifu kwa karama ya Shirika husika. Ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume, wakati akichangia mada kwenye Kongamano la Pili la Kimataifa lililofunguliwa, tarehe 25 Novemba na kuhitimishwa rasmi, Jumapili tarehe 27 Novemba 2016 mjini Roma.

Itakumbukwa kwamba, wajumbe wa Kongamano hili, Jumamosi tarehe 26 Novemba 2016, Baba Mtakatifu Francisko aliwatumia ujumbe uliopembua kwa kina na mapana kuhusu: Karama, uaminifu na uchumi kama nyenzo msingi za huduma ya upendo na mshikamano kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Rasilimali fedha na watu daima ni mali ya Kanisa ili kusaidia mchakato wa Uinjilishaji unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko kwa jirani!

Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo anayataka Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume kuwa aminifu kwa Injili ya Kristo kwanza na pili aminifu kwa karama ya Mashirika yao, ili kuweza kuwa na uhusiano bora zaidi katika kutumia, kuratibu na kuendeleza rasilimali fedha na vitu vinavyomilikiwa na Mashirika haya kama sehemu ya Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Watawa wasiwe ni watazamaji wa matatizo, changamoto na fursa mbali mbali za uchumi na maendeleo, bali wanapaswa kujisikia kuwa ni sehemu ya chagamoto hizi, tayari kusimama na kujizatiti zaidi katika uaminifu kwa Injili na Karama za Mashirika yao. Watawa pia ni sehemu ya mchakato wa utandawazi wa kimataifa, wasipokuwa makini wanaweza kujikuta wamesombwa na maji, huku wakibaki wameshika tama kwa huzuni na masikitiko makubwa! Watawa wanapaswa kuwa pia makini kwani kuna wajanja wachache ndani ya jamii wanaweza kuwatumia kwa ajili ya kujinufaisha wenyewe na matokeo yake ni kuwatumbukiza kwenye kashfa na kilio cha mwaka!

Watawa katika masuala ya kiuchumi wanaweza kusaidia kubadilisha mwelekeo wa utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kwa kujikita katika utandawazi wa upendo, haki na mshikamano wa dhati. Katika historia ya maisha na utume wa Kanisa watawa daima wamekuwa mstari wa mbele kufanya maamuzi magumu katika masuala ya kiuchumi, mintarafu huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Watawa wakatumia rasilimali fedha kwa ajili ya kuinua utu na heshima ya maskini duniani, dhamana ambayo inapaswa kusimamiwa kidete na watawa wa nyakati zote.

Majiundo makini na endelevu ya watawa kuhusiana na sera na mikakati ya uchumi mintarafu karama ya Mashirika yao, ni muhimu sana, ili kuendeleza ushuhuda wa kinabii katika ulimwengu mamboleo. Haya ni mang’amuzi ambayo yanayopaswa kutekelezwa katika ngazi ya mtu binafsi na Shirika katika ujumla wake. Nadhiri ya ufukara iwe ni kielelezo na utambulisho wa jinsi ambavyo Shirika linatumia rasilimali fedha na watu katika maisha na uutume wake unaopania kumwilisha karama ya Shirika katika uhalisia wa maisha ya watu husika.

Askofu mkuu Josè Rodriguez Carballo anaendelea kufafanua kwamba, ili kufikia lengo hili nyeti katika maisha na utume wa watawa kuna haja ya kuwa na wongofu wa ndani unaogusa akili na nyoyo za watawa; mageuzi ya miundo mbinu, sera na mikakati ya utekelezaji wa utume wa Shirika husika, daima utu na heshima ya binadamu, ustawi na mafao ya wengi vikipewa kipaumbele cha kwanza. Kuwepo na ushirikiano wa karibu na Makanisa mahalia na kwamba, maamuzi makini kuhusu usimamizi, uchumi na uendeshaji wa miradi ni maamuzi yanayopaswa kufanywa na Shirika na wala si walei wanaowasaidia katika utekelezaji wake.

Miradi ya watawa iwe ni kielelezo cha sadaka, umoja na udugu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Nadhiri ya ufukara iwe ni chachu ya ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa Jumuiya. Uchumi unapaswa kujikita katika ukarimu na ushirikishi, unaowaunganisha watu wengi zaidi, badala ya mwelekeo wa sasa kuwekwa chini ya wajanja wachache ambao mara nyingi wamekuwa ni sababu ya kilio na maombolezo ya Mashirika mengi ya kitawa. Uchumi uwawezeshe watawa kuondokana na ubinafsi na hali ya kujitafuta wenyewe na badala yake, uwe ni chachu muhimu sana katika ujenzi wa maisha na utume wa Kanisa mahalia.

Ikumbukwe daima kwamba, rasilimali na utajiri wa Mashirika ya kitawa ni mali ya Kanisa. Watawa wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanakuwa makini katika kusimamia, kuendeleza pamoja na kufanya tathmini ya mafanikio, matatizo na changamoto zinazowasibu katika kuendesha miradi yao, ili kuchukua hatua madhubuti. Mambo haya yasimamiwe na kanuni maadili, ukweli na uwazi; uaminifu, ustawi na mafao ya wengi. Sheria za nchi na za Kanisa, ziwe ni dira na mwongozo thabiti katika kusimamia rasilimali za Mashirika ya kitawa sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Francesco Montenegro, Rais wa Tume ya huduma ya upendo na afya kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia amekazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kufanya mang’amuzi ya kina na kila wakati ili kupata suluhu muafaka ya changamoto zinazoendelea kujitokeza katika sera za uchumi na maendeleo. Hii inatokana na ukweli kwamba, rasilimali na utajiri wa Mashirika ya kitawa ni kichocheo muhimu katika maisha na utume wa Kanisa mahalia, sanjari na ujenzi wa umoja wa watu wa Mungu. Watawa watambue udhaifu wao, matatizo na changamoto walizokumbana nazo katika historia na maisha yao na kutafuta msaada wa changamoto hizi, kwa kushirikiana na wataalam ili kuamua na kutenda kwa kusoma alama za nyakati.

Kwa upande wake Professa Luigino Bruni, kutoka Chuo kikuu cha LUMSA, Roma, amewataka watawa kutekeleza sera na mikakati yao ya shughuli za kiuchumi kwa kuwa na ari na moyo wa kinabii unaoshuhudia tunu msingi za Kiinjili zinazomwilishwa kwenye karama ya Mashirika haya. Rasilimali na utajiri wa Mashirika ya kitawa unapaswa kutumiwa vyema kama ushuhuda wenye mvuto na mashiko na urithi kwa siku za usoni.

Naye Professa Pierluigi Nava, amekazia umuhimu wa kuwa na utawala bora na makini wa rasilimali na utajiri wa Mashirika ya Kitawa, kwa kuzingatia maisha na utume wa Kanisa na kwamba, viongozi wa Mashirika wasitumbukie katika kishawishi cha kutumia rasilimali na utajiri wa Mashirika kwa ajili ya mafao yao binafsi au pengine na ndugu zao. Vinginevyo, huduma yao ni hatari kwa ustawi na maendeleo ya Shirika na Kanisa katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.