2016-11-28 14:26:00

Serikali Uingereza yaombwa ulinzi na utetezi zaidi kwa familia maskini


Ombi maalumu limetolewa na makanisa nchini Uingereza, yakiiomba serikali kuzijali kwa namna ya pekee na ukaribu sana familia zilizo maskini ambazo sasa zina mahangaiko mengi kutokana na myumbo wa uchumi uliosababishwa na nia ya Uingereza kujiengua kutoka Umoja wa Ulaya, Brexit. Viongozi wa makanisa wametoa angalisho na ombi hilo kufuatia taarifa za Bank ya Uingereza kwamba, hali kiuchumi sio nzuri sana na kwamba serikali itajikita kuhangaikia mahitaji msingi kama chakula.

Hali ya myumbo wa uchumi inazigusa hata nchi nyingine za Ulaya, takribani watu milioni 119, ambao ni sawa na robo ya wakazi wa Ulaya wamo hatarini kuangukia kwenye umaskini na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Kupanda kwa bei za bidhaa kutazidi kuwafanya watu wengi wakose chakula cha kutosha kwa siku, ameeleza mchungaji Richard Frazer, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanisa na Jamii, kwa Kanisa la Scozia.

Makanisa hayo ya kiprotestanti yameonesha wasiwasi wao wa hali za maisha kwa familia nyingi kutokana na uamuzi wa serikali kupunguza matumizi kwenye huduma za jamii, jambo ambalo litapelekea mmomonyoko mkubwa wa hali ya maisha kwa familia nyingi. Hali hii sio ya kufanyia mzaha sababu familia hizo ni milioni 4, na ndani ya familia hizo kuna watoto takribani milioni 7.5, ambao muda sio mrefu wataumizwa sana na myumbo wa uchumi nchini Uingereza. Ni muhimu kulitazama suala hilo kwa karibu na kulitafutia ufumbuzi wa haraka.

Makanisa hayo tangu mwanzo mwa mwaka huu 2016, yalichapisha waraka yaliouita enough, juu ya hali ya umaskini nchini Uingereza. Wito wake ni kuomba shughuli za serikali zitatue mahitaji halisi ya familia. Jambo ambalo kwa serikali linaonekana kuwa tofauti, ukizingatia serikali ya Uingereza ilipitisha sheria ya kujali watoto wawili tu wa kwanza kwenye kila familia, katika huduma za jamii.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.