2016-11-28 15:37:00

P. Peter Hans Kolvenbach, SJ., amefariki dunia!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Padre Peter Hans Kolvenbach, SJ., aliyefariki dunia, Jumapili tarehe 25 Novemba 2016 huko Lebanon. Aliwahi kuwa Mkuu wa Shirika la Wayesuit. Baba Mtakatifu katika salam za rambi rambi alizomwandikia Padre Arturo Sosa Abascal. SJ, Mkuu wa Shirika la Wayesuit, amemkumbuka Marehemu Kolvenbach kwa uaminifu wake kwa Kristo na Injili yake sanjari na ukarimu katika utekelezaji wa dhamana na majukumu yake ya kuongoza kwa ajili ya mafao ya Kanisa.

Baba Mtakatifu anapenda kumtolea Mwenyezi Mungu sala, ili kumwombea Marehemu Padre Kolvenbach huruma ya Mungu, amani na pumziko la milele. Baba Mtakatifu anasema, yuko pamoja wale wote wanaosikitika na kuomboleza kifo cha Padre Kolvenbach. Itakumbukwa kwamba, Padre Kolvenbach alizaliwa huko Holland kunako mwaka 1928. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako Mwaka 1961 huko Lebanon.

Alikuwa mkuu wa Shirika la Wayesuit kuanzia mwaka 1983 hadi mwaka 2008 alipong’atuka kutoka madarakani. Ameliongoza Shirika katika kipindi kigumu na chenye changamoto nyingi kama anavyokumbuka Padre Federico Lombardi, lakini alijielekeza kwenye utume wa kimissionari sehemu mbali mbali za dunia. Alikuwa ni mtu wa sala, mwenye kipaji cha akili na mtu wa watu kwa ajili ya watu, aliyependa kujadiliana na watu katika maisha yao.Alipenda kusoma na kuwaona watu wakipata ujuzi na maarifa ili kupambana na changamoto za maisha. Alikuwa ni kiongozi aliyebahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maisha ya kiroho na mtaalam mahiri wa Maandiko Matakatifu. Ni kiongozi ambaye kwa muda wa miaka 25 amewasaidia Wayesuit kujisikia kuwa ni sehemu ya Kanisa pamoja na Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.