2016-11-28 15:12:00

Jibidisheni kukutana na Kristo Yesu katika maisha yenu!


Imani ya kikristo sio kanuni, sio falsafa wala sio nadharia, imani ni kukutana na Kristu Yesu, Mungu kweli na Mtu kweli. Katika kukutana na Kristu mwanadamu lazima ajiweke kwenye hija ya imani kwa njia ya sala, ukarimu na kumsifu Mungu. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahuburi kwenye Misa Takatifu katika Kikanisa cha Mt. Martha, kilichoko mjini Vatican tarehe 28 Novemba 2016, kawaalika waamini kutumia kipindi cha majilio ili kukutana na Kristo maishani mwao. Kipindi hicho cha majilio kina masimulizi mazuri ya jinsi Kristu anavyokutana na mama yake tokea tumboni alipotungwa mimba, anavyokutana na Yohane mbatizaji, wachungaji kondeni, na mamajusi.

Waamini wazame kwenye sala ya kweli na ya rohoni, wahudumie watu wote hasa wahitaji kwa ukarimu, wachukuliane katika magumu na mapungufu, huku wakisaidiana kukua kwa pamoja kwa uvumilivu, na katika yote wampe sifa na utukufu Mwenyezi Mungu, ambaye Yeye huanzisha safari ya kukutana na mwanadamu, ili kumkomboa. Maisha ya kikristu yasiwe ufahamu tu wa mafundisho tanzu ya Kanisa, bali mafundisho ya imani yamsaidie mwamini kukutana na Mungu wake, amehimiza Baba Mtakatfu Francisko.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.