2016-11-26 15:39:00

Uwezo wa kiuchumi ujenge mshikamano na maskini!


Karama, Uaminifu na mwelekeo mpya wa uchumi ni mambo ambayo yamepembuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa kongamano la kimataifa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, lililoanza tarehe 25- 27 Novemba 2016. Kongamano hili limeandaliwa na Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, tema ambayo ni nyeti sana hasa wakati huu wa athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa.

Baba Mtakatifu anasema, karama ni mfano wa maji yanayobubujika mtoni kwa ajili ya kuboresha maisha ya watawa na kwamba karama daima inapaswa kupyaishwa na kamwe isibaki kuwa ni sehemu ya kumbu kumbu za kale. Karama ni uhalisia wa maisha unaopaswa kuzaa matunda yanayokusudiwa kwa kukua na kuongezeka; kwa kuzingatia uaminifu unaofumbatwa katika kipaji cha ugunduzi. Maisha ya kitawa ni alama ya kinabii katika ufalme wa Mungu.

Changamoto ni kuendelea kuwa macho na makini katika maisha ya kitawa, ili karama ambayo ni zawadi ya Mungu kwa waanzilishi wa Mashirika ya kitawa iweze kumwilishwa katika historia, mahali na nyakati, ili kuweza kuitolea ushuhuda na kuwashirikisha wengine uzuri wa kumfuasa Kristo katika maisha ya wakfu. Karama ni zawadi, neema na sadaka inayoangaza mzizi wa maisha ya watawa yaani upendo. Hata miongoni mwa Jamii, kama hakuna uchumi unaofumbatwa katika upendo, hapo kuna hatari ya kubeza utu na heshima ya binadamu. Uchumi unapaswa kufumbata tunu msingi za kiutu na kimaadili.

Watawa wanapaswa kutumia uwezo wao wa kichumi kwa ajili ya kujenga udugu, umoja na mshikamano na maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kusikiliza kwa makini ujumbe wa Neno la Mungu, tayari kushiriki katika mchakato wa kubariki, kuokoa na kuwasaidia wale wanaoteseka katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasema, lengo ni kuonja: matarajio, wasi wasi na matumaini yao kwa kutambua kwamba, mali na utajiri wa Mashirika ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, kama Wasamaria wema, mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu.

Watawa wawe na ujasiri wa kusikiliza maswali, ili kuyapatia majibu muafaka; kusikiliza kilio cha wale wanaoteseka, ili kuweza kuwafariji; kutambua ukosefu wa haki msingi za binadamu, ili kuzivalia njuga. Ni vyema ikiwa kama watawa watashirikisha pia uwezo wao wa kiuchumi ili kujenga na kudumisha amani, usalama na kuwaondolea watu hofu. Watawa watambue kwamba, hawana majibu ya maswali yote ya binadamu lakini ni matajiri wa matumaini.

Watawa wanapaswa kuwa waaminifu kwa kuwa na kutenda mintarafu karama ya Shirika, ili iweze kuwa ni chombo cha wema na huruma ya Mungu kwa watu wengi zaidi na kwamba, shughuli za kiuchumi zilenge kuendeleza karama ya Shirika kadiri ya maisha na utume wake ndani ya Kanisa. Uaminifu kwa karama ya Shirika unahitaji mang’amuzi makini, kwa kumwangalia Kristo Yesu, kwa kusikiliza kwa makini Neno lake na sauti ya maskini. Kwa njia hii, utume wa Shirika unaweza kuwa na mwelekeo mzuri kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa maskini.

Watawa wanapaswa kuwa na mang’amuzi mapya kuhusuiana na masuala ya kiuchumi anasema Baba Mtakatifu Francisko; kwa kusikiliza kilio cha maskini na kuwajibu kwa imani iliyooneshwa na waasisi wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume. Utume unaogusa shida na mahangaiko ya maskini, utu na heshima ya binadamu; maskini, wagonjwa, walemavu na wazee unapaswa kuendelezwa kwa kusoma alama za nyakati na kwa kushirikiana na Kanisa pamoja na Mashirika mengine ili kuondokana na ubinafsi unaoweza kujikita hata katika Mashirika ya kitawa.

Juhudi za makusudi zifanyike ili kutamadunisha karama za mashirika hata katika masuala ya kiuchumi kwa kutafuta majibu muafaka, kwa kuunganisha nguvu, ujuzi na weledi kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu na binadamu bila kusahau kujadiliana na Kanisa mahalia, kwami hata mali ya Mashirika ya Kitawa daima itaendelea kuwa ni mali ya Kanisa! Kuwa na mtazamo mpya kuhusiana na masuala ya kiuchumi kunalenga kuangalia mwelekeo, lengo na utekelezaji wa sera na mikakati mbali mbali ya shughuli za kiuchumi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume.

Huu ni utekelezaji makini wa sera zinazojikita katika rasilimali fedha na watu; kwa kuheshimu sheria sanjari na kusimama kidete kulinda na kuendeleza mazingira. Rasilimali fedha iwe ni chombo cha maendeleo na kamwe watawa wasigeuzwe kuwa ni watumwa wa fedha. Mwelekeo huu unafumbatwa katika mchakato wa kuwekeza katika wajibu wa pamoja, katika elimu na kanuni maadili ili kutambua Kondoo na mbwa mwitu kuhusiana na masuala ya fedha.

Uchu wa mali na fedha ni hatari sana kwa maisha ya kitawa anasikitika kusema Baba Mtakatifu Francisko. Watawa wawe waaminifu na waadilifu katika nadhiri ya ufukara kwa kujikita katika uaminifu, ukweli na uwazi kwa mali ya Shirika. Utajiri wa Mashirika uwe ni kwa ajili ya mchakato wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Katika uaminifu kwa karama, watawa wawe na ujasiri wa kuwa na mwelekeo mpya katika masuala ya kiuchumi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.