2016-11-26 08:09:00

Papa Francisko: Lindeni na kudumisha mila, desturi na tamaduni njema za watu


Ilikuwa ni tarehe 29 Novemba 1986, miaka thelathini iliyopita, kwa mara ya kwanza katika historia, Mtakatifu Yohane Paulo II alikutana na kuzungumza na wenyeji wa Australia wanaojulikana kama Aborijeni kutoka kwenye Visiwa vya Alice Spring. Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu hii, amemtumia ujumbe wa matashi mema Bwana John Lochowiak, Rais wa Baraza la Waamini wa Kanisa Katoliki kwenye Visiwa vya Torres, akiwataka kusimama kidete kulinda na kudumisha utamaduni wao! Ujumbe wa Baba Mtakatifu umewasilishwa nchini Australia na Askofu mkuu Adolfo Tito Yllana, Balozi wa Vatican nchini Australia.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anapenda kuonesha uwepo wa karibu kwa njia ya maisha ya kiroho na wenyeji wote wa Australia na kwamba, anathamini sana utamaduni wao, kwani ni amana na utajiri unaofumbata upendevu na utu wa wananchi hawa.  Hii ni changamoto ya kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha na utamaduni wao, changamoto iliyotolewa pia na Mtakatifu Yohane Paulo II, miaka 30 iliyopita. Wenyeji hawa wanahimizwa kushirikishana tunu hizi kati yao pamoja na kuendelea kuwarithisha watoto wao.

Lengo ni kuhakikisha kwamba, mila, desturi, tamaduni na lugha yao vinaendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo! Kwa njia hii anasema, Baba Mtakatifu Francisko wanatamadunisha Injili na hivyo kuiwezesha nguvu ya Injili kusafisha na kutasa yote ili kutekeleza utashi wa Mungu katika historia ya maisha ya mwanadamu. Ikumbukwe kwamba, Injili ya Kristo inazungumza lugha zote na wala haiwezi kufungwa na lugha maalum ya binadamu. Ni jambo lisiloweza kukubalika kwamba, Australia haikuwa na wenyewe wakati wenyeji wapo na wanaendelea kuwepo.

Baada ya mapambano kwa muda wa miaka 40 hatimaye, kunako mwaka 1991 Mahakama kuu ya Australia ilifuta hukumu iliyokuwa inasema kwamba, “Australia haina mwenyewe” “Terra nullius”. Tarehe 21 Juni 2015 wenyeji wa Australia wakarudishiwa tena ardhi yao, Kaskazini mwa Australia. Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kusimama kidete kupinga utanadawazi unaotaka kusawazisha mambo yote, kwani mila na desturi njema, zinapaswa kulindwa na kuendelezwa kwa ajili ya vizazi vijavyo.

Wongofu wa watu uzingatie pia tunu msingi za maisha yao kama sehemu ya mwendelezo wa mchakato wa utamadunisho na kwamba imani ni zawadi kutoka kwa mwenyezi Mungu. Kumbe, si sahihi kuendekeza wongofu wa shuruti. Leo hii, kuna haja ya kuwathamini watu na tamaduni, mila, desturi na lugha zao. Mchakato wa utamadunisho anasema Baba Mtakatifu Francisko umepata mafanikio makubwa nchini China kutokana na  mang’amuzi ya Wajesuit kama akina Matteo Ricci na Roberto di Nobili nchini India. Hawa ni wamissionari waliojielekeza zaidi katika majadiliano na utamadunisho na mafaniko yake yanaonekana wazi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.