2016-11-26 16:47:00

Ni wakati wa kushuhudia matendo ya huruma katika maisha!


Kanisa Katoliki Barani Ulaya limeadhimisha kwa furaha na matumaini Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu ambao umefikia kilele hivi karibuni. Kumekuwa na neema nyingi ambazo waamini wamezipokea na kushirikishana. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, linatumaini kwamba matunda ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu yataendelea kutajirisha hija ya imani kwa waamini wa Bara la Ulaya. Kelele na kero za vita, kinzani za nadharia za usawa wa kijinsia, ukosefu wa maelewano, kukengeuka kwa tamaduni na ukuaji wa mifumo ya utengano kijamii na umaskini unaokithiri, vinazidi kukuza hali ya kutojitambua na kupotea kwa jamii nyingi Barani Ulaya. Haya yote yanatokana na kupoteza fadhila za msingi zinazotokana na mafundisho ya Injili, fadhila ambazo ndizo zilijenga utamaduni wa Ulaya.

Kuna umuhimu sasa wa kudumisha matumaini, kuwa na imani thabiti na mshikamano ili kurejesha utamaduni wa Kikristo ambao ulikomaza jamii na historia ya Ulaya. Hili litakuwa jibu linaloendana na wito wa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa kwenye Barua yake ya kitume, Misericordia et misera, iliyotafsiriwa kama Huruma na amani; wito wa kuongeza juhudi kwenye kutafakari Neno la Mungu, kuchota neema za Sakramenti, kwa namna ya pekee kutambua umuhimu na thamani ya Sakramenti ya Upatanisho. Kwa siku za usoni Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, litajikita katika kutafuta mbinu za kuhakikisha kwamba mapendekezo ya Barua ya kitume Misericordia et misera yanazaa matunda kwa maisha ya waamini katika jumuiya mahalia, kwa namna ambayo itaangaza ule utamaduni wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika maisha ya watu!

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.