2016-11-25 12:14:00

Msithubutu kujadiliana na Ibilisi!


Kwa wale watakaokengeuka na kuamua kwenda mbali na upendo na huruma ya Mungu, ndio watakaolaaniwa milele. Shetani na Ibilisi mwenye kudanganya watu ana nguvu zaidi, kumbe, kamwe waamini wasijidanganye kujadiliana naye, atawabagwa chini na hapo watakiona che mtema kuni! Changamoto ni kuhakikisha kwamba, waamini wanamfungulia Kristo Yesu nyoyo zao, ili aweze kuwashirikisha furaha na maisha ya uzima wa milele na hivyo watairithi nchi mpya na mbingu mpya!

Kwa muhtasari hayo ndiyo mafundisho makuu yaliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican, Ijumaa tarehe 25 Novemba 2016, wakati huu Mama Kanisa anapojiandaa kufunga rasmi mwaka wa Liturujia ya Kanisa kwa kutafakari mambo ya nyakati, yaani Siku ya Hukumu ya mwisho, Yesu atakapokuja kuwahukumu wazima na  wafu na wala ufalme wake hautakuwa na mwisho, kama Kanisa linavyokiri na kuungama katika Kanuni ya Imani.

Baba Mtakatifu anasema, kadiri ya Maandiko Matakatifu kwenye Ufunuo wa Yohane, atakayehukumiwa wa kwanza ni Shetani, Ibilisi na nyoka atakeyefungwa milele na kutiwa muhuri juu yake asipate kuwadanganya mataifa tena. Ni baba wa udanganyifu na chanzo cha vishawishi na matokeo yake ni binadamu kukengeuka, kuasi na kupoteza maisha ya uzima wa milele. Waamini kamwe wasikubali kudanganywa na kurubuniwa na Shetani na Ibilisi. Yesu amewafundisha njia makini ni kutofanya majadiliano na Shetani hata kidogo! Ndiyo maana hata Yesu mwenyewe alimfukuzia mbali na watu!

Yesu Kristo alipokuwa Jangwani alipambana kufa na kupona na Ibilisi kwa kumpangulia hoja zake kwa njia ya Maandiko Matakatifu. Hii inatokana na ukweli kwamba, Ibilisi anatafuta kwa bidii zote kumwangusha mwanadamu katika dhambi, ndiyo maana atatupwa kuzimu, ili kusitisha kazi yake hapa duniani. Baba Mtakatifu anasema, katika kitabu cha Ufunuo wa Yohane kunatajwa Mashuhuda wa imani walioteswa na kudhulumiwa kwa ajili ya Kristo, Injili na Kanisa lake. Hao ni wenyeheri na watakatifu wa Mungu, ambao walisimama kidete kumshuhudia Kristo, hao sasa watakuwa ni makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja na Mwenyezi Mungu milele yote!

Hawa ni watu ambao kamwe hawakumezwa na malimwengu, uchu wa mali na madaraka wala utukufu kwa mambo ya kidunia, kiasi cha kuwa tayari kujisadaka kwa ajili ya Habari Njema ya Wokovu! Wataendelea kutawala na Mwenyezi Mungu, chanzo na hatima ya furaha ya maisha ya uzima wa milele; matumaini yanayohitimisha Kitabu cha ufunuo wa Yohane anasema Baba Mtakatifu Francisko! Matumaini yanafungua nyoyo za waamini ili kukutana na kumwambata Kristo Yesu katika hali yaunyenyekevu na mengine yote atayatekelezwa a Yesu Kristo mwenyewe!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.