2016-11-24 14:30:00

Wayesuit iweni na ujasiri na ushujaa wa kinabii katika maisha na utume!


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Oktoba 2016 alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa 36 wa Shirika la Wayesuit na kujibu maswali mbali mbali. Kwa ufupi aliwataka Wayesuit kuwa na ujasiri na ushujaa wa kinabii katika maisha na utume wao wa kutangaza, kushuhudia na kufundisha kweli za Kiinjili kati ya watu bila woga wala wasi wasi kama alivyokaza kusema Mtakatifu Yohane Paulo II. Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika majadiliano, diplomasia, ustawi, maendeleo na utawala wa sheria.

Amewataka Wayesuit kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tamaduni na mapokeo mazuri ya watu mahalia, kama mbereko muhimu ya tunu msingi za Kiinjili kama mwanzo wa mchakato wa Utamadunisho, ili Injili iweze kuingia katika mila na desturi za watu. Huu ni utandawazi unaoheshimu mila na desturi za watu, utu na heshima yao kama binadamu. Mtume Paulo, mwalimu wa Mataifa na akina Matteo Ricci na Roberto di Nobili wamissionari wa kweli ni mifano bora ya kuigwa katika maisha na utume wao kwa watu mahalia.

Kuna umuhimu wa kuendelea kujikita katika kanuni maadili na utu wema ili kufanya maamuzi sahihi katika maisha ya watu! Majiundo makini kwa majandokasisi ni muhimu sana ili kuwasaidia katika kujenga dhamiri nyofu na adilifu. Shirika la Wayesuit limebahatika kuwa na kurasa safi katika maisha na utume wake, lakini pia, limechafuka katika baadhi ya maeneo, kumbe linahitaji kufanya toba na wongofu wa ndani, ili kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi. Taalimungu maadili iwasaidie watu kuishi kweli za Kiinjili kama inavyofafanuliwa na Katekisim Mpya ya Kanisa Katoliki. Taalimungu inafundishwa kwa njia ya ushuhuda wa maisha ya sala.

Uwepo wa Mabruda ndani ya Shirika la Wayesuit na Kanisa katika ujumla wake ni changamoto kubwa inayopaswa kufanyiwa kazi! Ni mwaliko wa kuendelea kusoma alama za nyakati ili kusikiliza kile ambacho Roho Mtakatifu anawataka kufanya katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Bado kuna umuhimu wa Kanisa Barani Afrika kujikita katika mchakato wa ujenzi wa misingi ya haki, amani na upatanisho kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika na huko Mashariki ya kati.

Rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika viwe ni kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Siasa liwe ni jukwaa na sanaa ya ujenzi wa umoja na mshikamano wa kitaifa; upendo, haki na amani; mambo yanayofumbatwa katika majadiliano katika ukweli, haki na usawa! Tunu msingi za Kiinjili ni jukwaa muhimu sana la ustawi na maendeleo endelevu Barani Afrika.

Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni changamoto ya kimaadili, kijamii na kidini kwani binadamu amekabidhiwa dhamana ya kulinda na kudumisha mazingira kama sehemu ya kazi ya Uumbaji! Hii ni changamoto kwa Wayesuit kuwa maskini pamoja na maskini kwa ajili ya maskini, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake! Kanisa linapaswa kuwa ni chemchemi ya faraja, wema, huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!  Maskini ni amana, utajiri na rasilimali ya Kanisa, lakini uchu wa mali na madaraka ni hatari kwa maisha na utume wa Kanisa; mwaliko wa kuendelea kujifunza Heri za Mlimani kama muhtasari wa Mafundisho makuu ya Yesu kwa wafuasi wake.

Furaha ya Injili ni matunda na mwendeleo wa changamoto zilizotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika mchakato mzima wa Uinjilishaji wa watu unaopaswa kujikita katika furaha, ushuhuda, imani na matumaini sanjari na kuendelea kuhamasisha miito mbali mbali kwenye Makanisa mahalia, ili Kanisa liweze kupata watenda kazi: watakatifu, wachapakazi, watu wenye bidii, juhudi na maarifa, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu katika maisha ya watu!

Uinjilishaji huu unafumbatwa katika furaha ya upendo ndani ya familia pamoja na utunzaji wa mazingira nyumba ya wote kwani waathirika wakuu wa mabadiliko ya tabianchi ni familia maskini na akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi! Huu ni ushuhuda ambao ni mfumo mpya wa Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kupungua kwa miito mitakatifu ndani ya Kanisa ni tema itakayopembuliwa kwa kina na mapana na Sinodi ya Maaskofu kwa Mwaka 2018. Miito inapaswa kupandikizwa, kupaliliwa na kukuzwa, ili iweze kuzaa matunda ya utakatifu wa maisha, ari na moyo wa shughuli za kichungaji. Wakleri wajenge utamaduni wa kufundisha na kusikiliza; kuwaongoza na kuwaelekeza vijana katika maisha. Vijana washirikishwe kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, ili kujiandaa kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya jirani zao. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, lakini kuna haja ya kuwa makini kwa kusoma alama za nyakati, kwa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu, upendo na mshikamano, ajira na matumaini katika maisha, hasa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya: kiroho na kimwili.

Mwishoni mwa majadiliano haya kati ya Baba Mtakatifu Francisko na wajumbe wa mkutano mkuu wa 36 wa Shirika la Wayesuit, Padre Arturo Sosa, SJ. Mkuu wa Shirika alimshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kuwachangamotisha kuendelea kuishi kikamilifu karama ya Shirika, kutokutumbukia katika vishawishi na hatimaye kumezwa na malimwengu, bali kuendelea kutembea katika ukweli na haki kama watoto wateule wa Mungu, vyombo vya faraja, matumaini na majadiliano kwa jirani zao ili kukuza na kudumisha imani, haki, amani na maridhiano kati ya watu. Wataendeleza mchakato wa Uinjilishaji, Utamadunisho na ushuhuda wa tunu msingi za Kiinjili pamoja na kutekeleza ushauri wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Wayesuit ili kweli waweze kushiriki utume wa Injili ya Kristo kwa kuwa wamissionari wenye ari na furaha ya Injili inayomwilishwa katika maisha ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.