2016-11-24 15:34:00

Waathirika wa dawa za kulevya wasaidiwe kuanza upya maisha yao!


Tatizo la dawa za kulevya ni jeraha kubwa kwa jamii ya leo, ni mtego unaonasa watu wengi katika nyavu zake. Walionaswa katika mtego na kuhangaika na maumivu ya jeraha hilo, ni wahanga waliopoteza uhuru wao, na kutumbukia katika utumwa wa dawa za kulevya. Watu hao wamejikuta katika hali tegemezi ya kemikali za aina hiyo. Hii ni aina mpya ya utumwa, na kama vile utumwa mwingine, ni bakora inayomtandika na kumjeruhi sana mwanadamu na jamii kwa ujumla. Akitoa hotuba yake kwa washiriki wa mkutano mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi, Baba Mtakatifu Francisko amechanganua changamoto na uhitaji wa haraka wa kukabiliana na suala la madawa ya kulevya na kuwakomboa wahanga wa utumwa huo.

Ni wazi kuwa hakuna chanzo kimoja kinachopelekea matumizi mabaya na utegemezi wa dawa za kulevya. Vyanzo ni vingi ikiwa ni pamoja na kukosekana kwa maisha stahiki ya ndoa na familia, na ukosekanaji wa malezi bora kwa watoto, mahangaiko ya maisha katika jamii, ushawishi wa wafanyabiashara wa dawa hizo, tamaa ya kujaribu mambo mapya na kadhalika. Kwa kila mtu aliyeathirika na madawa ya kulevya, lazima kufahamu historia yake binafsi, lazima kumsikiliza, kumuelewa, kumpenda, na kadiri inavyowezekana atibiwe na kutakaswa kabisa kutoka kwenye dawa za kulevya. Kila mmoja awe makini asianguke kwenye mtego usio haki, wa kuwatazama waathirika wa dawa za kulevya kana kwamba ni vitu au vifaa vilivyovunjika na kukosa thamani katika jamii. Watu hao ni binadamu, wanastahili heshima, kuthaminiwa na kupewa hadhi ya binadamu ili waweze kuhudumiwa na kuponywa, kwani wanabaki kuwa ni viumbe na wana wa Mungu.

Sio jambo geni kufahamu kwamba wengi wameanguka kwenye matumizi ya dawa za kulevya kutokana na mtazamo na fursa ambazo jamii yenyewe imezitengeneza. Mtazamo wa kutaka viburudisho na furaha ya muda isiyodumu, na fursa za kuweka viburudisho hivyo ambavyo vinaishia kuwaumiza watumiaji, kuwakatisha tamaa, kuwaharibia maisha, na kuvuruga mwenendo wa furaha ya kweli ndani ya familia zao na kwa jamii kwa ujumla.

Baba Mtakatifu Francisko kawaalika wajumbe wa mkutano huo kuchanganua na kufahamu upana wa mtandao wa dawa za kulevya na hasa sehemu za uzalishaji wake na mfumo wa usambazaji. Inafahamika kuwa uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya ni kosa kubwa kisheria, hata hivyo ni muhimu kudhibiti mfumo huu, kuanzia kwenye wafanyabiashara wadogo wadogo wa madawa ya kulevya.

Mafanikio ya kufunga breki za biashara ya dawa za kulevya yatapatikana kwa kuweka nguvu na juhudi za kutosha kwenye utaratibu na mfumo mzuri kijamii kuhusu afya, kuunga mkono maisha ya ndoa na familia, na zaidi kuwekeza kwenye elimu, ambayo ni nyenzo ya msingi. Hatari na athari ya dawa za kulevya inazidi kuwashambulia walio wanyonge zaidi hasa watoto na vijana. Elimu fumbata ya mwandamu ipewe kipaumbele, kwani ni nyenzo msingi ya uelewa, uchambuzi, tathimini na utendaji makini, wenye maadili na unaoleta mafanikio, na hivyo kutengeneza jamii yenye furaha ya kweli, na sio jamii inayofumbata mambo ya mpito yasiyoleta furaha ya kudumu.

Pamoja na tahadhari za kuepuka kusambaa kwa madhara ya dawa za kulevya, Baba Mtakatifu Francisko amewaalika wadau wote kuwasaidia wahanga wa madawa ya kulevya ili kuwasafisha na kuwaponya na athari ambazo zimewakumba. Watu hawa ingawa wanaonekana hawana cha kutoa, wanao uhitaji mkubwa wa kupendwa, kuthaminiwa, kuponywa na kutunzwa sababu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, kama vile binadamu wote, na sura hiyo ndani yao haififii kamwe.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.