2016-11-24 12:15:00

Vatican na Vietnam kuendeleza umoja na ushirikiano!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano jioni tarehe 23 Novemba 2016 amekutana na kuzungumza na Rais Tran Dai Quang wa Jamhuri ya Kisoshalisti ya Vietnam ambaye baadaye amekutana pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican.

Katika mazungumzo baina ya viongozi hawa wawili, wamejadili kuhusu uhusiano mwema wa kidiplomasia uliopo kati ya Vatican na Vietnam, unaofumbatwa katika moyo wa majadiliano sanjari na kutafuta nyenzo muhimu zitakazoziwezesha nchi hizi mbili kuweza kushirikiana zaidi. Viongozi hao wamegusia pia kuhusu ushirikiano mwema uliopo kati ya Kanisa na Serikali ya Vietnam katika huduma kwa familia Mungu nchini humo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.