2016-11-24 09:33:00

Mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa vijana!


Sekretarieti ya Baraza kuu la Sinodi ya Maaskofu kuanzia tarehe 21- 23 Novemba 2016 limekuwa likifanya mkutano wake wa kawaida wa kumi na nne kwa uwepo na ushiriki wa Baba Mtakatifu Francisko. Mkutano ulianza kwa hotuba elekezi iliyotolewa na Kardinali Lorenzo Baldisseri aliyemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa uwepo na ushiriki wake. Amewakaribisha Makardinali wapya waliosimikwa hivi karibuni mjini Vatican.

Kati yao ni Kardinali Sèrgio Da Rocha na Kardinali Carlos Osoro Sierra. Mkutano huu pia umehudhuriwa na viongozi wakuu kutoka Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume; Baraza la Kipapa la Wakleri pamoja na Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha. Hii inatokana na ukweli kwamba, maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana yatayashirikisha Mabaraza haya kwa namna ya pekee kabisa.

Wajumbe wa Sekretarieti ya Baraza kuu la Sinodi za Maaskofu wamepembua kwa kina na mapana, huku wakisaidiwa na watalaam katika maisha na utume wa Kanisa kwa vijana kuhusu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Wajumbe wameridhishwa na muswada wa hati ya kutendea kazi pamoja na kuchangia mawazo, ili kuweza kuuboresha zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana. Pamoja na mambo mengine, muswada huu una maswali dodoso yatakayopelekwa kwenye Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali duniani, Sinodi za Makanisa ya Mashariki, Majimbo na Taasisi za Kikanisa.

Wajumbe waliweza kujigawa katika makundi madogo madogo kuliangana na jiografia na tamaduni za vijana, ili kuweza kuibua maswali dodoso yatakaokuwa na mchango mkubwa katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Mwishoni, mapendekezo yaliyowasilishwa yalikubaliwa bila kupingwa. Mwishoni, wajumbe  wameuchambua “Mwongozo wa Sinodi za Maaskofu” unaojulikana kwa lugha ya Kilatini “Ordo synodi espicoporum”.

Askofu Fabio Fabbene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu kwa kushirikiana na wataalam wa masuala haya wamechambua kwa kina na mapana kuhusu marekebisho ya Mwongozo huu kwa kubadilishana pia mawazo na wajumbe wa Baraza la Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Baada ya kazi hii nzito, Baba Mtakatifu Francisko amewashukuru wajumbe kwa uwepo na ushiriki wao, ushuhuda wa ari, umoja na mshikamano wa kidugu uliojidhihirisha wakati wa mkutano wao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.