2016-11-24 15:17:00

Kumbu kumbu endelevu ya Waebrania nchini Morocco!


Tarehe 14 Novemba 2016, katika mji wa Rabat, Morocco, kumetiwa saini makubaliano kati ya Makumbusho ya kitaifa ya Morocco na Taasisi ya Kumbukumbu ya Shoah ya Paris. Lengo ni kutengeneza tena kumbukumbu hai ya Waebrania kwa nchini Morocco. Habari ya maadhimio hayo ni ya muhimu kwa sababu kadha wa kadha. Kwanza kabisa, uwepo wa waebrania katika nchi ya Morocco ni jambo la kihistoria na la maana sana, likiwa limesheheni utajiri mkubwa wa kitamaduni. Imebaki kuwa jambo la kihistoria sababu baada ya kusimama tena kwa taifa la Israel mnamo 1948, waebrania walibaki wachache sana nchini Morocco. Walibaki takribani 8,000 kati ya waebrania 300,000 waliokuwepo.

Sababu ya pili ya msingi ni ule uelewa na ushirikishaji wa tamaduni wa kiebrania nchini Morocco, nchi ambayo ni ya kiislamu. Umuhimu na utajiri huu unaonekana hata kwenye nyanja za siasa za nchi ya Morocco. Sababu ya tatu ni kazi ya utunzaji mzuri wa nyaraka. Nyaraka nyingi zinahusu waebrania, sio tu za mateso na nyanyaso za Nazi wakati wa vita ya pili ya dunia, ambazo hata hazimo kwenye kumbukumbu ya Shoah. Lengo kubwa ni lile la kupata na kutunza vizuri historia nzima ya tamaduni za Kiebrania nchini Morocco. Kuzipa uhai nyaraka zinazoshuhudia kumbukumbu ya uwepo wa waebrania kwa miaka ya nyuma, ni tukio la muhimu na ushuhuda wa pekee kwamba Morocco imekuwa na muingiliano na mbadilishano wa utamaduni na fadhila za maisha kutoka kwa waebrania, mataifa baadhi ya Afrika na mediterania.

Kadiri ya kumbukumbu za kihistoria nchini Morocco, inaonekana waebrania wamekuwepo maeneo ya fukwe za Afrika mediterania tangu karne ya pili kabla ya kuzaliwa Kristu. Kumbe, baadhi ya koo za kiebrania zimeishi maeneo hayo wakati wa utawala wa Kirumi, utawala wa kibizantini, mpaka uvamizi wa Waarabu na utawala wa kiislamu wa dhimma, ambao ulikuwa utawala wa ubaguzi wa kuwalipisha kodi wasio Waislamu, hali iliyopelekea Wakristo na Waebrania wengi kubadili dini. Historia ya Waebrania wa Morocco inaendana na historia ya Waebrania wa Hispania kwa karne ya 15, hasa baada ya kufukuzwa kwa Waebrania kutoka penisula ya iberia. Utambuzi fulani wa haki sawa kwa waebrania ulipatikana mwaka 1864 wakati wa utawala wa Sultan Muhammad IV, ingawa bado Waebrania walidharaulika na kuonekana wa chini hata kisheria.

Sultan Muhammad V alirudisha sheria za ubaguzi za Vichy kwa nchi ya Morocco. Baadae kwa kupinduliwa kwake, sheria hizo ziliondolewa Morocco mnamo 1942, kwa kuhofia waebrania kukimbilia Marekani kama walivyofanya Waebrania waliokuwa Ulaya. Historia inakuja kunoga pale swali linapoibuka kutaka kujua waislamu wa Morocco waliwachukulia vipi Waebrania wakati wa vita ya pili ya dunia. Swali hili ni muhimu sababu ya mtandao wa kuvutia uliokuwepo katika kupeana bega kati ya waislamu na wanazi. Morocco ilianzisha harakati dhidi ya ukoloni, na Hitler aliwaunga mkono Morocco dhidi ya waingereza na wafaransa. Wakati huo Mufti wa Yerusalemu aliunga mkono sera za Hitler za Unazi, huku wakipania kukitokomeza kizazi cha waebrania.

Utamu na ukakasi wa sakata hili umefanya wanahistoria wengi kushindwa kutatua kitendawili cha iwapo Morocco walikuwa upande wa waebrania kubaki nchini humo, au waliridhia kutokomezwa kwao. Kitendawili hicho kinaweza kufumbuliwa kwa zawadi ya kumpa mji mwenye kitendawili, na mji uliohitajika, ndio makubaliano kati ya Makumbusho ya kitaifa ya Morocco na Taasisi ya kumbukumbu ya Shoah ya Paris, Ufaransa.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.