2016-11-23 09:38:00

Silaha za kibaiolojia ni hatari kwa usalama wa Jumuiya ya Kimataifa!


Itifaki ya Silaha za Kibaiolojia, ni chombo cha kwanza cha mshikamano kilichofanikiwa kupambana dhidi ya siraha tokomezi, kwa kuweka sheria madhubuti ya kimataifa dhidi ya silaha za kibaiolojia, sheria ambayo inapaswa kulindwa na kuimarishwa. Hii ni sehemu ya Hotuba ya Askofu mkuu Ivan Jurkovic, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican, kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yenye makao mjini Geneva, Uswisi, akizungumza katika kikao cha nane cha Itifaki ya siraha za Kibaiolojia kilichofanyika tarehe 7 Novemba, 2016.

Pamoja na mafanikio yaliyofikiwa mpaka sasa, Itifaki hiyo inakumbwa na changamoto za kukabili, katika utekelezaji wa madhumuni yao, ndani ya mpango mzima wa usalama kimataifa. Changamoto zinazotokana na mianya katika fani ya sayansi, kupamba moto kwa matishio ya kitamaduni na yasiyo ya kitamaduni, ongezeko la uzalishwaji, ununuzi na matumizi ya vifaa vya kibaiolojia kwa upande wa magaidi, mlipuko wa magonjwa pia ni tishio kwa afya na usalama wa dunia.

Ujumbe wa Vatican unaamini kwamba Itifaki hiyo ni mhimili wa kimataifa katika kutokomeza matumizi ya siraha na kuleta usalama kati ya watu. Kanuni-Endeshi za Itifaki hiyo zimeweka wazi kwamba: ni jambo lisilokubalika kwa dhamiri ya mwanadamu, kutoweka juhudi za kupunguza hatari ya siraha hizo. Askofu mkuu Ivan Jurkovic anasema: ni kinyume na utu wa mwanadamu, kutumia uhai kiubaguzi kuharibu uhai, kutumia sayansi kusambaza kifo badala ya kuponya magonjwa na kupunguza mateso.

Uhalisia na lengo kuu la Itifaki ya siraha za kibaiolojia, ni kutoa nafasi kuweka msisitizo na kuelewa uwiano wa moja kwa moja uliopo kati ya utokomezwaji wa siraha na maendeleo ya mwanadamu, na mahusiano ya nguvu yaliyopo kati ya dhana hizo mbili. Ni haki ya wote kushirikishana na kubadilishana kikamilifu vifaa, vitu, na taarifa za sayansi na teknolojia katika matumizi ya vitu vya kibakteriahai na madawa au kemikali kwa nia njema na ya amani; huku usalama, kinga na uhai vinapewa kipaumbele cha kwanza. Iwapo makubaliano hayo yatazingatiwa kwa kina na kufanyiwa kazi, itakuwa ni bakshishi nzuri kwa kupata ushiriki mkubwa wa wajumbe wa Itifaki ya siraha za kibaiolojia kidunia.

Magonjwa yaliyolipuka hivi karibuni, ni mfano tosha wa uwiano na mahusiano yaliyopo kati ya utokomezaji siraha na maendeleo. Milipuko hiyo imepigia mstari mipaka ya kitaifa na kimataifa katika kukabiliana na masuala ya namna hiyo. Inaeleweka jinsi gani milipuko hiyo yaweza kusambaa kwa urahisi kwenye mipaka ya nchi moja hadi nyigine, na namna gani afya ya jamii imo hatarini hasa kwa nchi maskini sana. Jibu gumu zaidi kutoa ni: nini kitatokea iwapo siraha za kibailojia zitarushusiwa, hasa ikitokea katika mafarakano ya kijeshi!

Kufuatia hatari hizo, Asofu mkuu Ivan Jurkovic anawaalika nchi wanachama wa Itifaki ya siraha za kibailojia kuendelea kuweka nguvu ya kutosha kwa ushirikiano wa kimataifa, huku wakijenga madaraja kati ya Mashirika ya kimataifa na ya mikondo, pamoja na wadau wote, ili kutokomeza kabisa matumizi ya siraha hatari. Kwa uhalisia wake, magonjwa hayaheshimu mipaka, hivyo kila mmoja anapaswa kuzingatia kwamba jirani zake wana mifumo thabiti ya afya. Kwa namna hii, inaonesha wazi kabisa kwamba; jina jingine la maendeleo ni amani na haki, anasema Askofu mkuu Ivan Jurkovic. Kutokuwepo kwa utaratibu wa kitaasisi katika Itifaki ya siraha za kibailojia, pale linapohitajika jibu au msaada kwa wahanga, ni changamoto ambayo inapaswa kutazamwa tena na kukabiliwa kwa makini. Changamoto hii ikabiliwe na kuwekewa mfumo unaofaa, ikikumbukwa kwamba hakuna utatuzi wa moja kwa moja kwa wahanga wa mashambulio ya kibailojia.

Maendeleo makubwa na ya haraka kwa upande wa sayansi na teknolojia, yamegusa mpaka fani za chembechembe hai za viumbe, kemikali na madawa. Kwa upande mmoja ni jambo la kheri, lakini pia ni rahisi kutumia maendeleo na uvumbuzi huo kwa wenye nia mbaya kusababisha majanga. Kwa kuwa kuna faida na hasara zake, Askofu mkuu Ivan Jurkovic anaialika Itifaki ya siraha za kibaiolojia kupitia na kukagua mara kwa mara maendelo na uvumbuzi huo, ili kuchukua hatua madhubuti za kinga pale wanapogundua hatari fulani.

Katika kufanikisha hilo, elimu ipewe kipaumbele. Maadili ya kitaifa na malezi bora ya tunu yaendelezwe na kuheshimiwa. Kila mmoja ashiriki katika kutetea maisha na maendeleo ya mwanadamu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko: kuna hitaji la kufikiri kila mara juu ya malengo, matokeo, mazingira na maadili ya utendaji wa binadamu, amao ni namna ya mamlaka yaliyo na hatari za kuzingatia (Rej., Laudato sì, 131). Ili kuzuia uzalishaji, ununuzi na matumizi ya siraha za kibaiolojia, inahitaji nguvu ya pamoja ya kimataifa. Hivyo Askofu mkuu Ivan Jurkovic, anawaalika wataalamu na wanachama wote wa itifaki ya siraha za kibaiolojia kuwa na mshikamano na lengo la pamoja ili kulinda uhai wa binadamu na kuheshimu utu wake.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican








All the contents on this site are copyrighted ©.