2016-11-22 14:52:00

Mwilisheni matunda ya mwaka wa huruma katika maisha halisi!


Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwachi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu imekuwa ni fursa ya kutafakari mafundisho makuu ya Kanisa kuhusu huruma ya Mungu kama yalivyochambuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, Uso wa huruma, Misericordiae vultus! Waamini kwa njia ya Kristo Yesu wameweza kugundua tena Uso wa huruma wa Baba wa milele katika maisha yao, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani.

Kimekuwa ni kipindi cha hija kwenye madhabahu mbali mbali ya huruma ya Mungu, lakini zaidi hija kwenye sakafu ya moyo wa mwamini mwenyewe, ili kuzama na kuangalia maisha yake, tayari kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu katika maishsa. Kauli mbiu ilikuwa “Wenye huruma kama Baba”. Lengo ni kuwapelekea wengine huruma na upendo wa Mungu na Kanisa katika maisha ya watu wote wanaohitaji huruma na upendo huu.

Hiki kimekuwa ni kipindi maalum cha katekesi ya kina, ambayo kwa mwaka mzima, Baba Mtakatifu Francisko amepembua kwa kina na mapana taalimungu ya huruma ya Mungu; Yesu Kristo ufunuo wa Uso wa huruma ya Baba; Matendo ya huruma kiroho na kimwili; toba na wongofu wa ndani; msamaha na upatanisho kama sehemu muhimu sana ya majiundo ya dhamiri ya waamini kuhusiana na mambo msingi ya maisha ya imani inayomwilishwa katika matendo. Imekuwa ni nafasi ya kuzama na kutafakari tena na tena Sakramenti za huruma ya Mungu, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha ya kila siku!

Askofu mkuu Ruwaichi anakaza kusema, imekuwa ni fursa ya kuimarisha Injili ya familia na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kwa kutambua kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani; Kanisa la msingi ambalo linakabiliwa na matatizo, changamoto na fursa mbali mbali zinazopaswa kufanyiwa kazi, ili kweli familia zenyewe ziweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma, upendo, haki, amani, msamaha na upatanisho. Ni wakati muafaka wa kuendelea kuimarisha makundi mbali mbali ndani ya Kanisa, ili yaweze kutazamwa kwa jicho la huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa wale wanaokabiliwa na matatizo, changamoto, furaha na matumaini yao mbali mbali watambue na kuonja uwepo endelevu wa huruma ya Mungu katika maisha yao; Mungu anayependa kuwapokea na kuwakumbatia jinsi walivyo, kwa kuwaganga na kuwaponya kwa mafuta na divai ya huruma na upendo wake usiokuwa na mwisho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.