2016-11-22 10:19:00

Matumizi haramu ya dawa za kulevya na madhara yake kwa jamii!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo kama vile kazi za suluba kwa watoto wadogo, biashara ya ngono, biashara haramu ya viungo vya binadamu; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni uhalifu dhidi ya utu na heshima ya binadamu. Mambo haya yanapaswa kutambuliwa kama yalivyo na viongozi wote wa kidini, wanasiasa, viongozi wa kijamii na watunga sheria wa kitaifa na kimataifa!

Taasisi ya Kipapa ya Sayansi kwa kutambua changamoto hii kubwa katika Jumuiya ya Kimataifa, kuanzia tarehe 23- 24 Novemba 2016 inaendesha warsha ya kimataifa mjinini na inahudhuriwa na  magwiji na wataalam wa mchakato wa mapambano dhidi ya biashara haramu ya dawa za kulevya duniani. Warsha hii inaongozwa na kauli mbiu “Dawa za Kulevya: Matatizo na suluhu ya kimataifa. Hii ni fursa makini kwa wataalam hawa kushirikisha mawazo na mang’amuzi yao kuhusu historia ya matumizi ya dawa za kulevya mintarafu tamaduni na jiografia ya watu. Aina mbali mbali ya dawa za kulevya na madhara yake katika afya ya binadamu; vituo maalum vya uzalishaji na usambazaji wa dawa haramu za kulevya na madhara yake ni kati ya mada zinazochambuliwa na mabingwa hawa, ili kusaidia kutoa mwanga, sera na mwelekeo mpya katika mchakato wa kupambana na dawa za kulevya duniani!

Askofu Marcelo Sànchez Sorondo, Rais wa Taasisi ya Kipapa ya Sayansi anasema waathirika wakuu wa janga la biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya ni vijana wa kizazi kipya wanaopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Takwimu zinaonesha kwamba, kumekuwepo na ongezeko la watu millioni tatu wanaotumia dawa haramu za kulevya duniani, ikilinganishwa na hali ilivyokuwa mwaka 2015. Watu millioni 27 kutoka sehemu mbali mbali za dunia walitambuliwa kuwa ni waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya na kwamba, ni idadi ndogo sana ya waathirika wanaopata fursa ya kupata tiba, ili kuondokana na hali hii tegemezi katika maisha yao.

Askofu Marcelo Sànchez Sorondo anakaza kusema, warsha hii ya kimataifa inalenga pamoja na mambo mengine kuchambua janga hili kwa kutumia miwani ya kisayansi, ili kubainisha na kuonesha athari zake pamoja na nguvu ya baadhi ya dawa zinazotumika katika tiba ya magonjwa ya binadamu. Mabingwa wanachambua pia maeneo maalum yanayozalisha na kutumia kwa wingi dawa haramu za kulevya pamoja na kuibua sera na mbinu mkakati wa kupambana na janga hili katika maisha ya kijamii.

Vijana na watoto wadogo wamekuwa wakitumiwa kama wakala katika mchakato wa kukuza na kudumisha biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kuna baadhi ya Serikali duniani zinataka kuhalalisha matumizi ya baadhi ya dawa za kulevya kama njia ya kupambana na biashara haramu ya dawa hizi. Ni nafasi pia ya kuangalia madhara ya maamuzi kama haya katika jamii husika. Majibu yanayotarajiwa kutolewa yana mwelekeo mpana zaidi katika masuala ya kijamii, kisiasa na kitiba. Lengo kuu zaidi ni kuendeleza mchakato wa kuwekeza katika elimu, kuzuia, kutibu na pale inapowezekana kufuta kabisa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya badala ya kuendelea na mtindo wa sasa wa kuwatia pingu wafanyabiashara na watumiaji wa dawa za kulevya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.