2016-11-22 13:49:00

Matokeo ya Elimu ya Sayansi na Teknolojia kwa Jamii ya Mwanadamu na Mazingira yake


Taasisi ya Kipapa ya Sayansi itafanya mkutano wake mkuu kuanzia tarehe 25 – 29 Novemba 2016 ambapo tafakari na majadiliano yatalenga kwenye athari zilizopo au zinazotegemewa kutokea kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Athari zinazokabili maendeleo endelevu ya jamii ya mwanadamu pamoja na mazingira kwa ujumla. Hata hivyo tafakari na majadiliano yataenda mbali zaidi katika kutazama pia faida zinazotokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ingawa baadhi ya athari na faida vitakuwa ni vya muda mfupi, ni muhimu wakatilia maanani mchango wa maendeleo endelevu katika dunia na katika maisha ya mwanadamu, ili kuwepo na uwiano wa maendeleo kutokana na mabadiliko yanayotokea katika sayari dunia.

Mkutano mkuu wa taasisi ya Kipapa ya sayansi utajadili: wajibu na miradi ya taasisi hiyo; elimu na malezi kwa upande wa sayansi na magonjwa yanayoathiri mishipa; chanzo, asili, fursa na mabadiliko ya ulimwengu; nafasi ya Kemikali na Nishati; Maisha na mchango wa viumbe hai, ikiwa ni pamoja na uelewa mamboleo wa jinsia na madhara au faida zake katika jamii; ushirikiano wa sayansi, siasa na dini kwenye suala zima la kusaidiana viungo wakati wa ugonjwa na biashara ya viungo kwa upande mwingine; kilimo, chakula na lishe kwa maboresho ya viumbe hai.

Ulimwengu na vyote vilivyomo vinakabiliwa na changamoto nyingi sana leo kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Shukrani kwa maendeleo hayo kumekuwa na faida nyingi sana kwa mwanadamu na viumbe vingi ulimwenguni. Hata hivyo ni lazima kuona udhibiti wa makini ili kuepuka madhara ya maendeleo ya sayansi na teknolojia yanayokuwa na maumivu makubwa kwa jamii ya mwanadamu na kuharibu zawadi ya ulimwengu na viumbe vyake ambavyo Mwenyezi Mungu amemtunukia mwanadamu avitumie na kuvitunza.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.  

 

 

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.