2016-11-22 14:23:00

Jiandaeni vyema kukutana na Kristo Hakimu mwenye haki na huruma


Katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Mtakatifu Cecilia, Bikira na Shahidi inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 22 Novemba, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican amesema, uaminifu wa Mungu kamwe hauwezi kumhadaa mwamini wakati wa kifo au atakapokuwa mbele ya kiti cha hukumu. Waamini wanapaswa kujikita katika mambo msingi ya maisha na kuachana na yale ambayo hayawezi kuwasaidia katika maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila mtu anahatima ya maisha yake, atakapokutana na Kristo Yesu, Hakimu mwenye haki. Mambo ya nyakati ni tafakari inayoletwa na Mama Kanisa wakati huu wa kufunga Mwaka wa Liturujia ya Kanisa. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya tafakari ya kina kwa kuchunguza maisha yao, ili kuwa na kumbu kumbu hai ya mambo msingi waliyotenda katika kipindi cha mwaka mzima. Ni vyema, waamini wakawa makini kwa mambo ambayo wanayaacha nyuma yao baada ya kukabiliana na kifo na wakati watakapokuwa mbele ya hukumu kama inavyofafanuliwa kwenye Kitabu cha Ufunuo.

Waamini wafanye tafakari ya kina kuhusu karama na mapaji ambayo Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha yao. Waangalie ni kwa jinsi gani Neno la Mungu lilivyokuwa na kushamiri katika maisha yao, kiasi cha kuzaa matunda yanayokusudiwa au wameelemewa na uchoyo pamoja na ubinafsi kiasi cha kuficha karama na mapaji yao na hivyo kushindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa macho na wala wasidanganyike, kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha; kwa kukumbatia malimwengu na kusahau mambo msingi ya imani! Wajiulize, Siku ya hukumu, Mungu atawakuta wakiwa katika hali gani ya maisha?

Baba Mtakatifu anakumbusha mambo makuu matatu: kifo, hukumu na maisha ya uzima wa milele au kutupwa motoni, ambako kuna kili ona kusaga meno. Huu ni ukweli wa kiimani na wala si kwa ajili ya kuwatisha watu, mwaliko wa kuhakikisha kwamba, kila mwamini anajitahidi kuboresha maisha yake ya kiroho, kwa kuwa karibu na Mwenyezi Mungu. Kwa waamini ambao wamekuwa waaminifu na waadilifu mbele ya Mwenyezi Mungu hawana sababu msingi ya kuogopa kifo! Waamini wawe waaminifu hadi kifo, ili waweze kuvikwa taji ya utukufu wa maisha ya uzima wa milele. Uaminifu kwa Mwenyezi Mungu kamwe hauwezi kumtupa mtu hata wakati wa kifo, licha ya udhaifu wa mwili na wingi wa dhambi, lakini watavikwa taji ya utukufu na hivyo kufurahia maisha ya uzima wa milele pasi na wasi wasi wa kifo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.