2016-11-21 15:30:00

UNICEF yaadhimisha miaka 70 ya uwepo na utendaji


Tangu kuanzishwa kwa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, baada ya vita vya pili vya dunia, limejikita kwenye kusaidia watoto walio katika hali ngumu na changamoto kimaisha, kusaidia familia zao zinazoishi katika hali ya umaskini, kuhudumia watoto wanaoteseka kwa athari za vita na majanga, machafuko, uonevu, nyanyaso na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Bwana Sergio Mattarella, Rais wa Italia, kapeleka ujumbe wake huo kwa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, linapoadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.

Palipo na manyanyaso, dhuluma, na utelekezaji, wenye kuteseka zaidi ni watoto. Huduma inayotolewa na UNICEF kwa watoto imepelekea Shirika hilo kujipatia ushindi, kujitwalia heshima, na kuvutia wengi katika harakati za kulinda na kutetea haki za mtoto. Ni dhahiri kwamba, ukandamizaji na udharirishaji wa utu wa mwanadamu leo, unaathiri sana ujengaji wa maisha bora kwa siku za usoni.

UNICEF kwa mikakati yake, na juhudi za kuamsha fahamu kwa wadau wengi, limefanikiwa kuzigusa dhamiri za watu na kushawishi mataifa, watawala wa serikali na rai wengi katika kutetea na kulinda haki za mtoto. Suala la haki za mtoto na kumhakikishia maisha stahiki, sio tu wajibu wa mshikamano wa wanadamu, bali pia ni uwekezaji kwa ajili ya amani na maendeleo endelevu.

Lengo la kila taifa, hata kwa zile nchi zilizoendelea sana, ni kuziba mgawanyiko na mpasuko kati ya jamii na kati ya watu. Mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na machafuko hayana mipaka, na ni lazima mapambano hayo yawasukume wote kupunguza utengano, matabaka, na kuzuia kusukumizwa  pembezoni mwa jamii, hasa watoto.

Rais Sergio Mattarella katoa pongezi za dhati kwa watumishi wa Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF na kwa wadau wote wa kutetea na kulinda haki za mtoto. Kawatakia maadhimisho mema ya miaka 70 ya kuanzishwa kwa UNICEF.

Na Padre Celestine Nyanda

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.