2016-11-20 10:42:00

Askofu msaidizi Timothèè Bodika Mansiyai ateuliwa kuwa Askofu wa Kikwit


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Edouard Mununu Kasiala, O.C.S.O wa Jimbo Katoliki la Kikwit nchini DRC la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu msaidizi Timothèè Bodika Mansiyai, P.S.S. kuwa Askofu  mpya wa Jimbo Katoliki la Kikwit, nchini DRC. Kabla ya uteuzi huu, Askofu Mansiyai alikuwa ni Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kinshasa.

Itakumbukwa kwamba, Askofu Timothèè Bodika Mansiyai, P.S.S. alizaliwa tarehe 1 Januari 1962 huko Kinshasa, DRC. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasi, kunako tarehe 1 Agosti 1990 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 2 Februari 2012 akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Kinshasa, DRC na kuwekwa wakfu hapo tarehe 15 Aprili 2012. Tarehe 19 Novemba 2016 wakati wa kufunga Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, amteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki Kikwit, nchini DRC.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.