2016-11-19 15:13:00

Tatueni kero za wawekezaji kuharakisha maendeleo ya viwanda!


Waziri mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa ameliegiza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha lifanye maamuzi ya kupima ardhi haraka na kutenga maeneo kwa ajili makazi na viwanda ili kujiandaa na uwekezaji mkubwa. Ametoa agizo hilo Jumamosi, Novemba 19, 2016 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani mara baada ya kukagua kiwanda cha kutengeneza magari ya zimamoto na matrekta cha Equator SUMA JKT Limited kilichopo Ruvu JKT, wilayani Kibaha mkoani Pwani. “Jiji la Dar es Salaam limejaa, na Kibaha mjini pia hawana ardhi ya kutosha kwa kimbilio pekee hivi sasa ni Kibaha Vijijini. Baraza la Madiwani fanyeni maamuzi, pimeni ardhi na mtenge maeneo ya makazi, viwanda na taasisi za elimu ili mkipata wawekezaji iwe rahisi kuwapa maeneo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa kiwanda hicho utakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri nyingi nchini kwani zilikuwa zinashindwa kumudu bei ya kununua magari ya zimamoto. “Baadhi ya Halmashauri nyingi zilikuwa zinanunua gari moja kwa sh. milioni 500 na hiki ni kiasi kikubwa mno… kwa hiyo kiwanda hiki kitakuwa mkombozi kwa taasisi nyingi na halmashauri zetu,” amesema.

Amesema maeneo mengi nchini yanahitaji magari ya zimamoto lakini yalikuwa yanashndwa kumudu bei za magari hayo. Aliyataja maeneo hayo kuwa ni viwanja vya ndege, bandari, taasisi zilizo chini ya TAMISEMI kama vile shule za sekondari za bweni, Majiji, miji mikuu, Manispaa na Halmashauri za Wilaya. Amesema ameguswa kukuta kiwanda hicho pia kina uwezo wa kutengeneza matreka na zana za kilimo (farm implements) kwani asilimia kubwa ya Watanzania ni wakulima na wanategemea jembe la mkono. “Kupitia kiwanda hiki, matrekta mengi yataunganishwa na nina imani bei itakuwa ya chini ili wananchi waweze kumudu.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Equator SUMA JKT Ltd, Eng. Robert Mangazini alimweleza Waziri Mkuu kwamba asilimia 80 ya ujenzi wa kiwanda hicho imekamilika na kwamba hivi sasa wako kwenhye hatua ya kufunga mitambo. Hata hivyo, alisema wanaisubiri iwasili kutoka India. Alisema kiwanda hicho kikikamilika kitaweza kuunganisha matrekta 3,000 kwa mwaka na magari ya zimamoto 100 na kubainisha kuwa faida za kuunganisha magari hayo hapa nchini ni kuwa na uwezo wa kuzalisha vipuri ndani ya nchi. “Tukiweza kuzalisha vipuri hapa nchini kwa asilimia 60, umiliki wa magari haya na matrekta utakuwa ni wa Tanzania na siyo wa kampuni za nje tena. Pia tutakuwa tumefaulu kuhamisha teknolojia kwa vijana wetu,” alisema. Hadi sasa vijana 60 wamekwishapatiwa mafunzo ona wako tayari kuanza kazi mara uzalishaji utakapoanza Machi, 2017.  Kuhusu teknolojia ya utengenezaji wa magari ya zimamoto, Eng. Mangazini alisema kiwanda hicho ni cha pili kujengwa barani Afrika cha kwanza kikiwa huko Bassa, Afrika Kusini.

Mapema, akisoma risala mbele ya Waziri Mkuu, mwakilishi wa Equator SUMA JKT Ltd. Kapteni Farijala Mkojera alisema kiwanda hicho kinamilikiwa kwa pamoja na kampuni ya Equator Automech Ltd ambao wana hisa asimilia 70 na SUMA JKT inamiliki asilimia 30 ya hisa za kiwanda hicho. Akizungumzia ujenzi wa kiwanda hicho, alisema hadi sasa wamekwishatumia sh. bilioni 1.5 na kwamba hadi ujenzi utakapokamilika, wanatajia kuwa wametumia sh. bilioni mbili.“Ujenzi ukikamilika, tunatarajia kuajiri wafanyakazi 200 katika fani mbalimbali,” alisema.

Alisema wakianza uzalishaji, mbali ya magari ya zimamoto na matrekta, wataweza pia kuunganisha mabasi na zana za kilimo kama vile combine harvesters. “Tutakuwa tumefanikiwa kuhamisha teknolojia kutoka Russia (magari za zimamoto) na India na Poland (matrekta). Tuna uhakika wa soko hapa nchini katika Jumuiaya za EAC na SADC,” alisema.

Wakati huo huo, Waziri mkuu Kassim Majaliwa ametoa siku 18 kwa Mkandarasi wa umeme kwenye kiwanda cha Kiluwa Steel Group awe amemaliza kazi ya kuweka ume mkubwa ili kiwanda hicho kianze kazi. Ametoa agizo hilo lJumamosi, Novemba 19, 2016 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa Serikali na wa Mkoa wa Pwani waliofika kiwandani hapo eneo la Mlandizi wakati akikagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Julai 12, mwaka huu alipozuru kiwanda kwa mara ya kwanza.

“Nilipokuwa hapa mara ya kwanza niliagiza itengenezwe njia ya reli kutoka njia panda ya reli ya kati, lakini pia niliagiwa uwekwe umeme wa msongo mkubwa ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mapema mwakani. Nimefarijika kukuta maagizo haya yametekelezwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa hili la umeme,” amesema. “Mkandarasi ameomba siku 14, nimempa hadi tarehe 7 Desemba ahakikishe umeme unafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Sasa hivi wameanza test lakini muda ili transforma iweze kuhimili mzigo mkubwa… hili ni suala la kitaalamu kwa hiyo tuwape muda.” Waziri Mkuu pia amesema amefarijika kusikia kwa orodha ya watu wanaodai fidia sababu ya kuoisha njia ya reli ijengwe, imeshawasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na mwenye kiwanda yuko tayari kuwalipa maa taratibu zitakapokamilika.

Mapema, akiwasilisha taarifa fupi, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Eng. Evarist Ndikilo alisema haelewi ni kwa nini mkandarasi huyo anazidi kuomba siku 14 ili kukamilisha wakati aliahidi kuwa 14 za awali zingetosha kukamilisha kazi hiyo. Kuhusu fidia kwa wananchi na Halmashauri ya Wilaya hiyo, Mkuu huyo wa Mkoa alisema wananchi waliopisha njia wanadai fidia ya sh. milioni 95.76 na Halmashauri inadai sh. milioni 307.26 na kwamba jumla yote inafikia sh. milioni 403.

Alipopewa nafasi na Mkuu wa Mkoa huo ajieleze mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Dekan Group Ltd, Eng. Desderius Luhaga ambaye amepewa kazi ya kuweka umeme na transforma Mlandizi alisema anahitaji apewe siku 14 ili aweze kukamilisha kazi hiyo. “Kazi kubwa ya umeme tumeshaifanya na hii ni ya umeme wa msongo wa kilovoti 132, na tumeanza kutest umeme katika baadhi ya mitambo hapa kiwandani, lakini tunahitaji siku karibu tano ili transforma ipoe tangu tulipoifunga ndipo iweze kupokea mzigo mkubwa. Kisha tutaanza kuunganisha katika maeneo mengine madogo madogo humu ndani,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Reli Tanzania (TRL), Bw. Masanja Kadogosa amesema shirika hilo limetumia sh. milioni 863 kukamilisha ujenzi wa reli ya km.5 kutoka njia panda hadi kwenye kiwanda hicho ambapo kati ya hizo km.1.5 zimo ndani ya kiwanda. Amesema hadi sasa wameshaweka njia nne za reli, moja ikiwa ni mahsusi kwa ajili ya kubeba makaa ya mawe. “Tulilazimika pia kujenga culvert katika eneo moja kwa sababu pailikuwa na shimo kubwa. Tumetumia fedha kidogo kwa sababu tumetumia mafundi wetu badala ya wakandarasi,” ameongeza.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiluwa Steel Group, Bw. Mohammed Kiluwa alimweleza Waziri Mkuu kuwa anatarajia kuanza uzalishaji Januari, mwakani na kwamba ataajiri wafanyakazi wapatao 200. “Tunataraji kuanza uzalishaji Janruari, mwakani na uzalishaji utakuwa tani 2,000 kwa siku. Ila tumekubaliana na wawekezaji wenzangu tuweke pia viwanda vingine vitatu kwa sababu kutakuwa na umeme wa kutosha.” “Tunatarajia kufungua viwanda vine vya kutengeneza gypsum powder, pikipiki, nguzo na vifaa vya kufungia nyaya za umeme mkubwa pamoja na tissue. Tuna eneo lingine Mkuranga lakini kule hakuna umeme, kwa hiyo tumepanga kuweka hivyo viwanda hapa kwa sababu tuna eneo la kutosha.”

Hata hivyo, Bw. Kiluwa alitumia fursa hiyo kumweleza Waziri Mkuu kwamba wanapata taabu ya makaa ya mawe kwa sababu wanaletewa makaa yenye ukubwa wa milimita 10 hadi 15 badala ya milimita 35 – 40 ambazo wanahitaji kwa ajili ya kiwanda chao. “Tukiagiza tani 30, tunachambua mawe ya saizi inayotufaa na kujikuta tunabakia na tani saba tu. Kiasi kilichobakia ni vumbi tupu,” alisema. Waziri Mkuu alimwagiza Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, Eng. John Malongo awasiliane na Wizara ya Nishati na Madini ili afuatilie ni kwa nini watengenezaji wa makaa ya mawe hawafuati vipimo halisi vinavyotolewa na wawekezaji.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU.








All the contents on this site are copyrighted ©.