2016-11-19 11:51:00

Makardinali wako tayari kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake


Kardinali Mario Zenari, Balozi wa Vatican nchini Siria, Jumamosi, tarehe 19 Novemba 2016 kwa niaba ya Makardinali wapya, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwaona na kuwateua kuwa Makardinali alama maalum ya umoja wa Kanisa kutoka sehemu mbali mbali za dunia, ili kuonesha Ukatoliki wa Kanisa hata katika utofauti wake katika kuadhimisha imani moja ya Kanisa. Makardinali wapya ni watu wanaotoka katika huduma mbali mbali za Kanisa kama: wafanyakazi wa Vatican; wachungaji na mashuhuda wa wito na maisha ya Kipadre na Kikristo!

Makardinali kama ilivyo familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma “Misericordes sicut Pater”! Ni mwaliko wa kuendelea kuimba utenzi wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika uhalisia wa maisha ya watu, kielelezo cha imani tendaji!

Kanisa linatumwa kutoka kifua mbele ili kuwaendelea watu walioko pembezoni mwa mambo msingi ya kijamii, ili kutangaza na kushuhudia; imani na Injili ya Kristo; upendo wa kifamilia unaofumbatwa katika mafuta ya huruma ya Mungu, ili kuweza kuimba tena utenzi wa viumbe wote kwa kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; daima kwa kutembea katika mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene! Makardinali wapya wanaangalishwa kuwa ni mashuhuda wa imani, kiasi hata cha kuweza kujisadaka bila ya kujibakiza, kama wanavyoendelea kushuhudia mashuhuda wa imani kutoka sehemu mbali mbali za dunia, tangu mwanzo wa Ukristo!

Kardinali Mario Zenari anaendelea kusema, Kanisa la Kristo linaendelea na hija yake hapa ulimwenguni kwa kudhulumiwa lakini kwa kupakwa mafuta ya faraja kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama anavyosema Mtakatifu Agostino, Askofu na mwalimu wa Kanisa. Fumbo la Mwili wa Kristo,yaani Kanisa linaendelea kuteseka kutokana na udhaifu wake wa kibinadamu, lakini bado linapaswa kwa vito vya gharama na Kristo Yesu kama ilivyo kanzu nyekundu kwa Makardinali, alama ya ushuhuda wa imani hadi kifo! Kanisa ni Msamaria mwema anayetaka kusimama ili kuwaganga watu madonda yao na kuwafariji kwa mafuta na divai ya huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Zenari anasema, baadhi yao wanaotoka kwenye maeneo ya vita, migogoro, kinzani na mipasuko ya kijamii ambako watu wanakufa kama wanyama; watoto wanashindwa kwenda shule kutokana na vita na kwamba, athari zote hizi zinawakumba wananchi na raia wa kawaida, hali inayopelekea mateso na mahangaiko makubwa kwa watu. Baadhi ya maeneo duniani yamegeuka kuwa ni majukwaa ya matendo ya huruma ya Mungu: kiroho na kimwili na huko kuna Wasamaria kibao wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya jirani zao.

Makardinali wapya wanampongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuendelea kusimama kidete: kulaani na kupinga vita sehemu mbali mbali za dunia, kwa kuwataka wahusika kujikita katika mchakato wa upatanisho, haki na amani; ukarimu na upendo kwa wakimbizi na wahamiaji pamoja na mshikamano  wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu duniani! Baada ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wataendelea kumwimbia Mwenyezi Mungu fadhili zake za milele, chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.