2016-11-19 12:06:00

Makardinali ni washauri wakuu wa Khalifa wa Mtume Petro!


Makardinali wapya 17 waliosimikwa rasmi kwenye Ibada iliyoadhimishwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumamosi, tarehe 19 Novemba 2016 wanatoka katika mataifa 11 duniani. Ibada hii ni sehemu ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu anasema lengo la kuwa na wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia ni kuweza kushuhudia Ukatoliki wa Kanisa; kuendeleza umoja wa Kanisa na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na Makanisa mahalia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wanasema, kusudi uaskofu uwe na umoja usiogawanyika, Kristo Yesu alimweka Mtakatifu Petro, juu ya mitume wengine, na katika yeye akatia chanzo na msingi unaodumu na unaoonekana wa umoja wa imani na ushirika.

Kutoka Barani Afrika, kuna Kardinali Dieudonnè Nzapalainga, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Bangui, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, ambaye kwenye tukio hili la kusimikwa kuwa Kardinali amesindikwa na  ujumbe kutoka Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati uliongozwa na Rais Faustin Archange Touadera. Wengine ni Kardinali Maurice Piat, Askofu wa wa Jimbo Katoliki la Port Louis, tangu mwaka 1993. Kardinali Sebastian Koto Khoarai, ni Askofu mstaafu wa Jimbo Katoliki Mohale’s Hoek, nchini Lesotho.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Makardinali hawa wapya kwa sasa ni sehemu ya viongozi wa Kanisa la Roma na watashiriki katika huduma ya kitume. Makardinali wapya wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Kristo na Injili yake sehemu mbali mbali za dunia. Wanatekeleza dhamana na wajibu wao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Makardinali wapya wamekiri kanuni ya imani na kula kiapo cha utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro. Wamevikwa kofia nyekundu ya Kikardinali alama na kielelezo cha heshima ya Ukardinali. Lakini, ikumbukwe kwamba, alama nyekundu maana yake ni kwamba, wao wako tayari kujisadaka kiasi hata cha kumwaga damu yao kwa ajili ya imani na usalama wa watu wa Mungu; wako tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya uhuru na uenezaji wa Kanisa Katoliki.

Makardinali wamevikwa pete rasmi, alama ya upendo wao kwa Mtakatifu Petro, ili waweze kuimarisha na kudumisha upendo wao kwa Kanisa la Kristo. Mwishoni, Makardinali wapya wamepangiwa Makanisa ya huduma ndani ya Jimbo kuu la Roma, kwani tangu sasa wao ni sehemu ya familia ya Mungu Jimbo kuu la Roma. Hatimaye, kila Kardinali alipewa Waraka unaomwonesha kuteuliwa na hatimaye kusimkwa kama Kardinali na hivyo kuwa ni kati ya washauri wakuu wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.